Fadhila za Tawhid
Jamii ya vilivyomo
Vyanzo
Full Description
بسم الله الرحمن الرحيم
Fadhila Za Tawhiyd.
Imeandaliwa na alhidaaya.com
Imepitiwa na Yunus Kanuni Ngenda.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa):
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ
Basi elewa kwamba laa ilaaha illa-Allaah (hapana mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki ila Allaah)[Muhammad: 19]
Maana ya Tawhiyd kama alivyosema ‘Allaamah ‘Abdir-Rahmaan Naaswir As-Sa’dy katika “Al-Qawlus-Sadiyd Fiy Maqaaswidit-Tawhiyd - Sharh Kitaab At-Tawhiyd”
“Tambua kwamba maana ya Tawhiyd haina mipaka. Ni maarifa na kukiri kumpwekesha Ar-Rabb (Mola) kwa Swifa za ukamilifu, na kuthibitisha kwamba Anapwekeshwa katika Sifa Zake Adhimu na Tukufu, na kumpwekesha katika ‘ibaadah zote”.
Kinyume cha Tawhiyd ni ‘Shirk’ ambayo ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) katika hayo yaliyotajwa yote yanayomuhusu Yeye Pekee.
‘Ulamaa wameigawanywa Tawhiyd katika sehemu tatu:
1 – Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah
Nayo ni kumpwekesha Allaah katika Uumbaji, Uendeshaji wa mambo yote katika Ulimwengu, Utoaji rizki, Uletaji uhai na Ufishaji, kwa kuamini kwamba Yeye Ndiye Aliyeumba kila kitu, Anayeruzuku na kuendesha mambo yote ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa). Hana mshirika, na kuamini kwamba Ufalme wote ni wake:
Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Anasema:
قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ
Sema: "Ni nani Mola wa mbingu na ardhi?" Sema: "Ni Allaah" [Ar-Ra’d:16]
Na Anasema:
قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ
Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa (aliye) hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka (aliye) uhai; na nani anayedabiri mambo (yote)? Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi na taqwa?” (Hamumkhofu Allaah?) [Yunus: 31]
2-Tawhiyd Al-Uluwhiyyah
Maana yake ni kumwepekesha Allaah katika 'ibaadah na kuzielekeza ‘ibaadah zote kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa).
Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Anasema:
قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾
Sema: “Hakika Swalaah yangu, na nusukiy (kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu) na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah (Pekee) Mola wa walimwengu.” Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (waliojisilimisha kwa Allaah). [Al-An’aam: 162-163]
3-Tawhiyd Asmaa wasw-Swifaat
Kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) kwa Sifa Zake Tukufu, na Majina Yake mazuri, bila kuzigeuza Sifa hizo maana zake, au kuzipinga, au kuzifananisha na viumbe au kuzipa unamna. Yeye Amejipa Majina mazuri mazuri na Sifa nzuri nzuri na Akawataka waja Wake wamuombe na kumtukuza kwa Majina na Sifa hizo.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Anasema:
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾
Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa (kwa kuharibu utukufu, kukanusha, kugeuza maana, kushabihisha) katika Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf: 180]
Qur-aan nzima imedhihirisha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); mfano Suwratul-Faatihah ambayo tunaisoma kila siku mara kumi na saba katika Swalaah zetu za fardhi na pia katika Swalaah zote nyinginezo, imejumuisha aina tatu zote za Tawhiyd.
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿١﴾ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣﴾ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٤﴾ إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾
Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaanir-Rahiym (Mwingi wa Rahmah - Mwenye kurehemu). AlhamduliLLaahi (Sifa njema zote ni za Allaah) Mola wa walimwengu. Ar-Rahmaanir-Rahiym (Mwingi wa Rahmah-Mwenye kurehemu). Maalik (Mfalme) wa siku ya malipo. Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada [Al-Faatihah: 1-5]
Na pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ ۚ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴿٦٥﴾
Mola wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake; basi mwabudu Yeye tu na dumisha subira katika ‘ibaadah Yake. Je, unamjua (mwengine) mwenye Jina Lake? (Bila shaka hakuna aliyefanana Naye kwa lolote, vyovyote, na wala hana mshirika!). [Maryam: 65]