FAIDA YA KUSAMEHE NA HASARA YA KUTOSAMEHE
Jamii ya vilivyomo
Full Description
FAIDA YA KUSAMEHE
NA HASARA YA KUTOSAMEHE
Imeandaliwa na:
Yunus Kanuni Ngenda
Imepitiwa na:
Abubakari Shabani Rukonkwa
بسم الله الرحمن الرحيم
Utangulizi
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote, na rehma na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad (s.a.w) na watu wake na Maswahaba wake wote. Amma baad:
Kusamehe ni jambo jepesi sana, lakini limekua ni tatizo kubwa katika jamii hasa jamii ya kiislam. Swali ni kwamba je! Wasiopenda kusamehe wanajua faida na kheri zinazo patikana kwa mtu mwenye kusamehe? Bila shaka hawajui! Basi ikiwa ni hivo tuziangalie kwa pamoja baadhi ya ya kheri na faida kama anavyo eleza Mwenyzi Mungu katika Qur’an tukufu:
Anasema Mwenyezi Mungu mtukufu:
}...Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda{. Surat Baqara: 263
Na anasema Mwenyezi Mungu:
}Kauli njema na usamehevu (kusamehe) ni bora kuliko sadaka inayo fuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha na Mpole{. Surat Baqara: 263
Na akasema tena Mwenyezi Mungu:
}Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa{. Surat Ash-Shuura: 43
Na kauli nyingine ya Mwenyezi Mungu anasema:
}...Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu{. Suratu Nur: 22
JAMBO LA KUPENDEZA
Kinacho vutia katika Aya hizo ni kitendo cha sisi kusameheana, kumbe kusamehe ni bora zaidi kuliko kulipiza kisasi. Maana kulipiza sio ubaya kama ulivyotendewa lakini kusamehe ni bora zaidi na unapata thawabu nyingi.
Japokuwa mtu amekudhulumu inafaa uitafute haki yako kwa njia zote zile za kisheria ili urudishiwe haki yako. Wala usichoke kufanya hivyo kwani kuachilia haki yako itamfanya mtu huyo awe na ujasiri wa kukudhulumu kwa mara nyingine tena na tena na haswa mtu huyo akiwa si mwenye aqida au tabia nzuri.
Unapo dhulumiwa kwa namna yoyote ile Uislamu umekupatia njia tatu ya kuliendea suala hilo:
A.Kulipiza kisasi.
B.Kumsamehe na kufanya subra.
C. Kumuachia Mwenyezi Mungu.
FAIDA ZA KUSAMEHE.
Hakika kusamehe ni bora, kwani kufanya hivyo kuna faida nyingi nitataja chache zifuatazo:
1. Kusamehewa madhambi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: { Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.}(Qur’an 24:22).
2. Kupandishwa daraja na kuwa miongoni mwa watu wema.
Anasema Mwenyezi Mungu : { Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu, }(Qur’ 3:133).
3. Kulipwa ujira kutoka kwa MwenyeziMungu.
Amesema Mwenyezi Mungu: { Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu. } (Qur’an 42:40).
4. Kuwa pamoja na MwenyeziMungu, na kulipwa ujira wa kusubiri.
Anasema MwenyeziMungu : { Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri (126) Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya MwenyeziMungu tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozifanya.} (Qur’an 16: 126 - 128).
Licha ya faida hizo ambazo Mwenyezi Mungu amezitaja kwenye Qur'an, vilevile kuna faida za kisaikolojia pale mtu anapo msamehe yule alie mkosea, kwa kisaikolojia kumfanyia uadui Muisilamu mwenzio hakuwezi kuondoa ubaya, ila nasaha na mawaidha ndio yanayoweza kumbadilisha mja kuwa mtu mwema.
Mwenyezi Mungu kaweka hukumu za kulipiza kisasi, ili tusidhuliane kwa kuona kuwa nikifanya jambo fulani basi namimi nitafanyiwa kama ilo.
Watu wengi wanashindwa kuelewa kwamba kupatwa na hasira sana ni dalili ya kutopevuka kiakili.
Hata hivyo tusikereke na watu wanaotukera na kutuudhi mara kwa mara, bali tuwafunike kwa shuka ya amani na upendo na upole kwa kuwapa nasaha njema.
Kwa sababu binadamu anapofanyiwa makosa, moyo wake hujaa hamaki na chuki kwa yule aliye mkosea, na hii hupelekea akili yake kuweka niya ya kulipiza kisasi, wakati huo huyo ndani ya mwili wake husambaa aina ya kemikali inayotokana na kumwagika kwa nyongo, ndio maana tunapo patwa na hasira au maudhi mioyo yetu upata maumivu na hata kuuguwa kwa kipindi kile ulichokasirika.
Hali hii ikiwa inajitokeza mara kwa mara basi mtu mwenye kukasirika anaweza kupata matatizo ya Moyo au vidonda vya tumbo, vilevile anakuwa hana utulivu kwenye nafsi yake na haswa kila anapo muona yule aliyemkosea.
NINI AFANYE MTU ALIE PATWA NA HASIRA?
1.Amlani Shetani.
2.Anatakiwa anyamanze kama aliuwa anaongea.
Kutoka kwa Ibn Abasi (ﷺ.a) alisema alisema: Alisema Mtume (s.a.w) :"Fundisheni dini na wafanyieni wepesi watu,na atakapo kasirika mmoja wenu basi anyamanze"
3.Ikiwa amesimama basi anatakiwa akae.
4.Ikiwa amekaa basi anatakiwa alale akiweza.
5.Atawadhe.
6.Afikilie malipo makubwa ya mwenye kuziwiya Hasira zake.
7.Akithirishe kumtaja Mwenyezi Mungu.
8.Afikile hatima ya Hasira.
Usipo samehe kuna mengi unayakosa kama nilivyo eleza faida nne hapo juu, Usipo samehe hutopata utulivu wa nafsi, kwa sababu unajirimbikizia machungu ambayo hukupelekea kupata maradhi ya saratani ya akili na kupelekea kuwa na maamuzi yasiyofaa na yaliojaa visasi na chuki.
walenga walisema : (Hasira Hasara).
Mifano tunayo ndani ya nafsi zetu wenyewe, ni vipi tunajisikia pale tunapo waona wale walio tukosea, ni vipi tunajisikia tunapokwenda kwenye shughuli mbalimbali, tukajumuika kwa furaha na mara akatoea au wakatokea wale tunao wachukia kwa kuwa tu walitukosea na hatukuwa samehe!!, je unajihisi vipi ndani ya nafsi yako?
Kiukweli huwa tunahisi tafrani na ile furaha tuliyokuwa nayo huyeyuka na nafasi yake huchukuliwa na maumivu ndani ya mioyo yetu, Kiasi cha kutaka hata kuondoka kwenye hizo sherehe au mialiko.
Lakini ikitokea kuwa tumesamehe, basi hata Mwenyezi Mungu naye hutusamehe pia na vilevile tunapata utulivu ndani ya nafsi zetu. Na darja zetu hupanda.
Lakini kusamehe kuliko bora ni pale ambapo uwezo wa kulipiza kisasi tunao, lakini tukasamehe, kwa sababu aliyekukosea unamuweza kwa kila hali.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe ni wenye kusameheana. Ameen!!