×
Mada hii inazunguzia Bidaa za sherehe za mazazi ya Mtume(s.a.w)

    بسم الله الرحمن الرحيم

    BID'A YA MAWLIDI

    Imeandikwa na: Shaykh 'Abdullaah Swaalih Faarsiy

    Imepitiwa na: Abubakari shabani Rukonkwa

    1. Kusoma Mawlid

    Mawlid ni uzushi (Bid’ah) uliyozuka baada ya kupita hao watu mabora aliowasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama tulivyobainisha katika Dhikiri namba moja. “KUDHIKIRI” Hata mjukuu wa huyu aliyetunga Mawlid ya Barzanjiy akaifanyia sharh yake akiita “Al-Kawkabul-Anwaar” aliandika katika sahifa 4 maneno haya “Jua kuwa kusoma Mawlid ni bid’ah (uzushi) kwani halijapokelewa jambo hili kwa hao Ulamaa waliokuwa karne tatu tukufu za mbele huko zilizosifiwa na Mtume”. Basi inatosha shahada hii ya huyu mjukuu khasa wa huyu mwenye Barzanjiy. Imekuwa “Washahida shaahidun min ahlih” yaani akashuhudia shahidi wao wenyewe.

    Basi wacha kushughulikia mambo yasiyokuwa ndiyo, khasa ilivyokuwa yanatokea ndani yake mambo mabaya kabisa yasiyokuwa ndiyo. Kama mchanganyiko wa wanaume na wanawake unaotokea wakafanya mambo yasiyokuwa ndiyo. Na mambo haya si kificho, hakuna asiyejua.

    Na ubaya wake mkubwa zaidi kule kuwadhanisha watu kuwa hilo ni jambo zuri lilohimizwa na Mtume, kumbe kinyume nyume. Usitoe pesa lako kwa jambo lilokwenda kinyume na alivyosema Mtume.

    2. Zeffe (Zafa)

    Nani asiyejua namna Zeffe inavyoutia aibu Uislamu? Fujo la wanaume na wanawake, mbali fujo la wahuni. Fujo la wanaocheza ngoma za uchafu, na chakacha na dansa na nyinginezo. Yuko mwenye akili yake timamu akayaona mazuri haya?

    3. Kupiga Dufu (Daf) Na Mazumari

    Kupiga daf msikitini ni haramu kwa wanavyouni wote wanaotegemewa kama ilivyo sahifa 273 ya Juzuu ya tatu ya “I’anatut-Twalibyn” Alisema: “Halipigwi Daf msikitini, seuze kupiga mazumari” Ati Gasba; Gasba ndiye nduguye zumari na zumari ndiye nduguye Gasba. Ila huyu mfupi huyu mrefu.

    Ama kupigwa nje ya Msikiti kwa jambo la arusi na la furaha (kwa wanawake) haikatazwi maadam hapana mchanganyiko wa wanaume na wanawake.

    Ama kwa jambo linaloitikadiwa kuwa la Dini basi hakuna yeyote mwenye kutegemewa aliyesema ni jambo zuri hilo seuze kusema ni Sunnah. Mufti mkubwa wa Hadhramauti wa zama hizo – Sayyid ‘Abdur-Rahmaan Mashhuur - Alisema katika sahifa 322 ya kitabu chake: “Bughyatul-Mustarshidyn”: “Na kwa kila hali mambo hayo ima haramu au karaha au Sivyo ilivyo bora”.

    Basi uko wapi huo uzuri hapa? Seuze Usunnah? Si Sharifu wa Hadhramauti huyu? Na Mufti huko pia? Na ndiye Sheikh wa Sayyid Mansab, Sayyid Ahmad bin Sumeit na Shaykh ‘Abdallaah Bakathiyr na walimfuata vyema kwani ndiyo haki. Hawakuhudhuria kwenye matari wala hawakuya kubalisha mpaka wameondoka ulimwenguni.
    Na huyu mufti alizaliwa Hadhramaut mwaka 1250 akafa 1320.