SIFA ZA MWANAMKE WA KIISLAM
Jamii ya vilivyomo
Full Description
بسم الله الرحمن الرحيم
SIFA ZA MWANAMKE WA KIISLAM
Imekusanywa na: Idara ya Wanachuoni.com
Imepitiwa na: Yunus Kanuni Ngenda
1- Ni mwenye kushikamana na Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mipaka anayoweza juu ya ufahamu wa wema waliotangulia (Salaf-us-Swaalih).
2- Anatakiwa vilevile atangamane na Waislamu wenzake matangamano mazuri, bali hata makafiri [atangamane nao kwa uzuri]. Allaah (´Azza wa Jalla) Anasema:
وَقُولُوا لِلنَّاسِ
"Na semeni na watu kwa uzuri." (02:83)
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا
"Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe." (04:58)
وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا
"Na mnaposema [katika kushuhudia] basi semeni kwa uadilifu." (06:152)
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا
"Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu mtoapo ushahidi kwa ajili ya Allaah japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini Allaah Anawastahiki zaidi. Basi msifuate hawaa [matamanio] mkaacha kufanya uadilifu. Na mkipotoa [ushahidi wenu] au mkijitenga [kuepuka au kukataa kutoa ushahidi], basi hakika Allaah kwa myatendayo ni Khabiyraa (Mjuzi wa vilivyodhahiri na vilivyofichikana)." (04:135)
3- Anatakiwa kushikamana na mavazi ya Kiislamu na ajiepushe na kujifananisha na maadui wa Kiislamu. Imaam Ahmad amepokea kwenye "al-Musnad" yake kupitia Hadiyth ya ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Yule mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao."
Allaah (´Azza wa Jalla) Anasema kuhusiana na mavazi:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ
"Ee Nabii! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kuwa ni watu wa heshima, ili) wasiudhiwe." (33:59)
at-Tirmidhiy amepokea kwenye "al-Jaamiy´" yake kupitia Hadiyth ya ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Mwanamke ni ´Awrah. Anapotoka nje basi matumaini ya Shaytwaan huwa juu."
4- Tunamnasihi vilevile amtendee mume wake wema ikiwa kama anataka kupata maisha yenye furaha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:
"Mwanaume akimwita mke wake kwenye kitanda chake na akakataa, basi Malaika humlaani." (al-Bukhaariy na Muslim)
Kwenye "as-Swahiyh" ya Muslim imekuja:
"... isipokuwa yule aliyeko mbinguni humghadhibikia."
5- Awaangalie watoto zake kwa malezi ya Kiislamu. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwenye "as-Swahiyh" zao kupitia Hadiyth ya ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Nyote ni wachungaji na kila mmoja ataulizwa juu ya kile alichokichunga."
Akasema kuhusu mwanamke:
"Ni mchungaji kwenye nyumba ya mume wake na ataulizwa kwa kile alichokichunga."
Kwenye "as-Swahiyh" mbili kupitia Hadiyth ya Ma´qil bin Yasaar (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Hakuna mchungaji ambaye atachungishwa watu wake kisha asiwaangalie isipokuwa hatonusa harufu ya Pepo."
Da´wah isimshughulishe na kuwalea watoto wake.
6- Inatakiwa kwake kuridhia yale Aliyohukumu Allaah kwa kumfadhilisha mwanaume juu ya mwanamke. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Anasema:
وَلَا تَتَمَنَّوْا مَا فَضَّلَ اللَّـهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ
"Wala msitamani ambayo Allaah Amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine." (04:32)
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا
"Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya [matumizi] wanayotoa katika mali zao. Basi wanawake wema watiifu, wenye kuhifadhi [hata] wanapokuwa hawapo [waumezao] kwa Aliyoyahifadhi Allaah. Na wale [wanawake] ambao mnakhofu uasi wao, basi waonyeni na [wakiendelea uasi] wahameni katika malazi [vitanda] na [mwishowe wakishikilia uasi] wapigeni. Wakikutiini, basi msitafute dhidi yao njia [ya kuwaudhi bure]." (04:34)
Imepokelewa kwenye "as-Swahiyh" mbili kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Watendeeni wanawake wema. Hakika mwanamke ameumbwa kwa ubavu ulopinda. Kiungo kilichopinda zaidi kwenye ubavu wake ni kile cha juu. Ukienda kutaka kukinyoosha utakivunja, na ukikiacha kitabaki kimepinda. Hivyo basi, watedeeni wanawake weama."
Inatakiwa kwa mwanamke awe ni mvumilivu kwa yale Aliyomkadiria Allaah kwa kumfadhilisha mwanaume juu yake. Lakini hata hivyo hii haina maana mwanamke amuabudu mwanaume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema kama ilivo kwenye "al-Jaamiy´" ya at-Tirmidhiy:
"Watendeeni wanawake wema. Hakika wao ni kama wafungwa wenu. Hammiliki jengine kwao zaidi ya hilo. Tanabahini! Hakika nyinyi mna haki juu ya wanawake zenu. Tanabahini! Hakika wanawake zenu wana haki juu yenu. Haki zenu juu yao ni wao kutomwacha yeyote yule mnayemchukia akalala kwenye vitanda vyenu na wasimruhusu kwenye manyumba yenu yule mnayemchukia. Haki zao juu yenu ni kuwatendea wema katika kuwalisha, kuwavisha."
Kwenye "as-Sunan" na "al-Musnad" ya Imaam Ahmad kupitia Hadiyth ya Mu´aawiyah bin Haydah ya kwamba kuna mtu alimwambia:
"Ee Mtume wa Allaah! Ni zipi haki za mke juu ya mmoja wetu?"
Akasema:
"Ni umlishe pale utapokula. Umvishe pale utapovaa. Usimpige usoni na usimkebehi na usimhame isipokuwa nyumbani."
Inatakikana nyote kusaidizana katika kheri. Mwanaume atangamane na mke wake matangamano ya Kiislamu na amsaidie kusoma na kulingania katika Dini ya Allaah. Mwanamke vilevile atangamane na mume wake matangamano ya Kiislamu na amsaidie kusoma na kulingania katika Dini ya Allaah na kuendesha mambo ya nyumbani kwa uzuri. Allaah (´Azza wa Jalla) Anasema:
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ
"Shirikianeni katika wema na uchaji Allaah na wala msishirikiane katika dhambi na uadui." (05:02)
Mzungumzaji: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
Chanzo: "Majmuu´-ul-Fataawaa an-Nisaa-i-yyah"