×
Mada hii inazunguzia ubora wa Mama kwa mwanae, katika jamii na hata mbele ya Allah (S.w)

    بسم الله الرحمن الرحيم

    NANI KAMA MAMA?

    Imeandiwa na Yunus Kanuni Ngenda.

    Imepitiwa na Abubakari Shabani Rukonkwa.

    Utangulizi:

    Kwa mara nyingine tena ndugu zangu katika imani tuogelee kwa pamoja katika bahari ya ndefu yenye kina kirefu sana, nayo ni bahari ya wazazi! Na leo hii tutamzungumzia MAMA.


    MAMA NI NANI?

    MAMA: ni yule ambae umekaa katika tumbo lake kwa kipindi cha miezi tisa, amekubeba katika tumbo lake shida juu ya shida, akawa ni sababu ya wewe kuwepo katika wigo wa dunia, alipokuzaa MAMA alikulea, alikunyonyesha na ilikua paja lake ndio godoro lako, maziwa yake ndio kinywaji chako na mgongo wake ndio pumziko lako. yuko wapi mwingine kama MAMA?.

    NAFASI YA MAMA MBELE YA ALLAH.

    Nafasi ya mama mbele ya Allah ni kubwa sana, na Allah ameusia katika Aya nyingi juu ya kumfanyia wema MAMA, na ni vema kumshukuru Allah kisha kumshukuru MAMA kutokana na majukum mazito aliyoyabeba mpaka ukapatikana.

    Anasema Allah (S.w)

    (ووصينا الإنسان بوالديه حملته أمه وهنا على وهن و فصاله في عامين أن اشكر لي ولوالديك إلي المصير) (لقمان14 )

    Na tumemuusia mwanadam kwa wazazi wake wawili, Mama yake ameichukua (ameibeba) mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu (tabu juu ya tabu) na akamwachisha ziwa baada miaka miwili. (Basi) Nishukuru Mimi (Allah) na wazazi wako, na kwangu mimi (Allah) ndio marejeo (yenu).


    Qur'an (31:14).

    NAFASI YA MAMA KWA MTOTO

    MAMA ana nafasi ya pekee kwa mtoto, na mama ni mlango kaka milango ya Peponi.

    الأم باب من أبواب الجنة، من برها دخل الجنة

    MAMA ni mlango katika milango ya Peponi mwenye kumfanyia wema ataingia Peponi.

    عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه و سلم: (رغم أنف رغم أنف رغم أنف، قيل من يا رسول الله؟ قال: من أدرك أبويه عند الكبر أو أحدهما ثم لم يدخل الجنة) (رواه مسلم)


    Kutoka kwa Abiy Hurayra radhi za Allah zimuendee kaesema: Amesema Mtume (s.a.w) Amepata hasara! Amepata hasara! Amepata! Pakasemwa nani Ewe Mtume wa Allah? Akasema: Mtu ambae aliwapata wazazi wake (Baba na Mama) wakiwa watu wazima (wazee) au mmoja wao akawa hakuingia Peponi).

    (Hadithi hii ameipokea Muslim.)

    Allahu akbar!! Ndugu zangu katika imani tazameni hiyo milango ya kuingilia Peponi! Tazama namna ambavyo Allah ametupendelea sisi ummat Muhammad (s.a.w).
    Hii ni fursa adhwim kubwa kwako ewe muislam usiipoteze kisha ukaenda kujuta mbele ya Allah, jinyenyekeze kwa wazazi wako kwa kuwafanyia ihsani ili uzipate radhi za wazazi na upate radhi za Allah (S.w). Kwasababu radhi za Allah zipo katika radhi za wazazi wawili kama alivyotufundisha Mtume (s.a.w).

    NAFASI YA MAMA KATIKA JAMII.

    MAMA ataendelea kuwa na nafasi na hadhi kubwa katika jamii yoyote hapa dunia kama ilivyokua kubwa hadhi mbele ya Allah (S.w).


    Siku moja aliulizwa Mtume (s.a.w) ni mtu gani! Mwenye kustahiki kufanyiwa ihsani na wema zaidi kuliko wengine? Mtume (s.a.w) alijibu kama ifuatavyo:-

    عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: جاء رجل إلى رسول الله صلى الله عليه و سلم فقال: يا رسول الله، من أحق الناس بحسن صحابتي؟ قال: أمك، قال: ثم من؟ قال: ثم أمك، قال: ثم من؟ قال: ثم أمك، قال: ثم من؟ قال: ثم أبوك)
    رواه البخاري و مسلم

    Kutoka kwa Abuu Hurayra radhi za Allah zimwendee anasema: Alikuja mpaka kwa Mtume (s.a.w) (akamuuliza) akasema: Ewe Mtume wa Allah katika watu ni nani mwenye haki zadi nimfanyie wema? (ihsani?) Mtume (s.a.w) (akamjibu) akasema: Ni Mama yako, (akauliza tena) akasema: kisha nani? Mtume (s.a.w) (akamjibu) akasema: Kisha Mama yako, (akauliza tena) akasema: kisha nani? Mtume (s.a.w) (akamjibu) akasema kisha Mama yako, (akauliza tena) akasema: kisha nani? Mtume (s.a.w) (akamjibu) akasema: kisha Baba yako.))


    Hadithi hii ameipoke Bukhar na Muslim.

    Katika Hadithi hii Mtume (s.a.w) anabainisha na kuweka wazi ubora na umuhim wa MAMA na kwamba katika watu wote duniani MAMA ndio wa kwanza anatakiwa kufanyiwa wema, ihsani na ukaribu mara tatu ya Baba.

    Masikini MAMA!!!! Leo hii MAMA amekua mtu wa kawaida sana hata kufikia hatu baadhi ya vijana wa zama hizi wa kiume na wa kike wanamuona MAMA si lolote si chochote! MAMA hujibiwa vibaya na watoto alio wazaa, MAMA hasaidiwi na watoto alio wazaa, MAMA hunyanyaswa na watoto alio wazaa, MAMA wakati mwingine huambiwa ni mchawi na watoto alio wazaa, kini MAMA huvumilia yote na mwisho wa siku husema mwanangu chakula hiki nimekuandalia.
    Nani mwingine kama MAMA?

    Jinyenyekeze kwa MAMA kwa kumfanyia ihsani ili upate radhi zake leo na kesho Akherah:

    Je unajua kama MAMA akikasirika na Allah anakasirika?

    Je unajua kama MAMA akikulaani na Allah anakulaani?

    Je unajua kama MAMA akikutenga na Allah anakutenga?

    Je unajua kama ukifa hali ya kua huna radhi za MAMA hata harufu ya Pepo huipati?

    Basi ogopa kumuasi MAMA kwasababu hakuna kama MAMA.

    KWANINI MAMA!

    Shekh mmoja mwenye hekima alisimlia kisa murua akasema:-

    Siku moja mtoto alimuuliza mama yake kwa nini unalia? Akajibu kwa sababu mimi ni mwanamke! Mtoto akasema
    mimi sifahamu, Mama akamkumbatia mtoto wake na kumwambia si rahisi kunielewa! kisha mtoto akamfuata babake na kumuuliza kwanini mama analia?

    Baba akajibu:
    Wanawake wengi wapenda kulia bila sababu.

    Mtoto alipokua akawa bado hajajua sababu hasa ya mwanamke kulia bila sababu kama alivyoambiwa na baba yake, mwisho akamuuliza shekh mwenye hikma:
    Kwa nini wanawake wapenda kulia bila sababu?
    Akajibu:
    Allah alipomuumba mwanamke alimpa mabega yenye nguvu sana kwa ajili ya kubeba mazito ya walimwengu.

    Na akamjaalia mikono mwiwili milaini na iliojaa upendo kwa ajili ya kuwapa watu raha na akampa nguvu ndani ya mwili wake ili kuweza kubeba mimba hadi kuzaa na vile vile kuvumilia pindi watoto wanapokua kisha wakamkataa.

    Pia kapewa uwezo wa kubeba aibu za nyumba yake na familia yake pamoja na kuwa na msimamo ktk kila jambo zito bila kutetereka.

    Na akampa mapenzi juu ya watoto wake yasoisha na wala kubadilika

    hata wakimkera na kumtukana na kumsababishia maumivu makali bado mapenzi yako pale pale.

    Na mwisho Allah kampa (machozi)


    yanayot oka kwa haraka pindi anapopata matatizo,
    Na huo ndio udhaifu wake.

    Kwa hiyo chunga na uheshimu machozi ya MAMA katika huu ulimwengu hata ikiwa wanalia bila sababu! Kimekatwa kitovu chako pindi ulipotoka katika hii dunia
    na hicho kitovu kikaacha athari (alama) kwenye mwili wako ili ukumbuke daima.

    Mwisho:

    Ewe mola wetu Tunakuomba kwa kadri ya mapigo ya mioyo yetu wajaalie MAMA ZETU wawe wanamke bora katika wanawake wa Peponi na uwasamehe na uwajaalie wote Pepo ya Firdausi yawe ni makaazi yao. Ameen!!