×
Mada hi inazungumzia sharti za kuswihi kwa funga na baadhi ya maswali na majibu katika mambo muhimu ambayo yanawatatiza baadhi ya waislam.

بسم الله الرحمن الرحيم

SHARTI ZA KUSIHI KWA FUNGA - SEHEMU YA KWANZA


Makala imeandaliwa na Raudhwah islamic Group

Imepitiwa na Abubakari Shabani Rukonkwa.

Ili swaum isihi kuna sharti zake zitimizwe ndipo funga hiyo itasihi. Na sharti hizi zisipokamilika basi funga haitosihi au funga itabatilika na itamlazimu mwenye kufunga aje kuilipa funga hiyo.

Hivyo hatutokuja kueleza yanayofunguza. Bali makala hii in shaa Allah itamtosheleza msomaji kujua sharti za kusihi kwa funga na kubatilika kwa funga. Pia katika baadhi ya vitabu wametumia neno NGUZO ZA FUNGA zote hizo ni sawa na wanakusudia kukieleza kitu hicho hicho.

1-KUTIA NIA KILA SIKU
Ni lazima kwa mwenye kufunga atie nia kwa kila siku anayofunga. Iwe funga hiyo ya sunna au faradhi kama Ramadhan. Na hatokuwa na funga yule atakaekuwa hajatia nia. Kwani katika hadithi kutoka kwa Sayyidina Omar (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “Nimemsikia Mjumbe wa Allah akisema: “ Hakika kila jambo huambatana na nia na kila mtu atalipwa kutokana na kile alichokinuwia … .” ]Bukhari na Muslim[.

Na inamuwajibikia mwenye kufunga Ramadhan atie nia kabla ya kuanza kwa alfajiri ya kweli. Na endapo mwenye kutaka kufunga hatotia nia kabla ya wakati huo basi hatokuwa na funga. Na itamuwajibikia kwake yeye kuja kuilipa funga hiyo. Kwa ushahidi wa Hadithi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam): “Yeyote ambae hatoweka nia ya kufunga kabla ya alfajiri hatokuwa na funga.” Imepokewa na Imam Ahmad na An-Nasai.

Hivyo inamlazimu atie nia kwa kuzingatia kabla ya kuanza kwa funga na nia hiyo iwe kwa kila siku atakayoifunga. Ama mwenye kufunga sunna anaweza kutia nia kabla ya kupambazukwa kwa jua,mpaka wakati wa zawali (kabla ya Adhuhuri)

Kwa nini mtu atie nia kila siku ndani ya Ramadhani? Swala humalizika kwa mtu kutoa salam. Na anapotaka kuingia katika swala nyengine basi analazimika kutia nia ya swala nyengine. Hivyo hivyo kwa mwenye kufunga, swaumu humalizika kwa kuzama kwa jua hivyo basi anaetaka kufunga siku ya pili lazima atie nia nyengine. Kwani anakuwa ameanza swaumu nyengine. Na hii ndio kauli yenye nguvu.

Imethibiti hadithi ya mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) akisema:

قال صلى الله عليه وسلم: "لا صيام لمن لم يبيت النية من الليل"[رواه الإمام مالك في الموطأ ج1 ص288 من حديث عبد الله بن عمر موقوفًا.

Alisema mtume (swalla Allahu alayhi wasallam):Hana funga yoyote ambae alie lala bila kuweka nia usiku.

]Imepokelewa na imamu maliki katika kitabu chake cha muwatwaa 1/288[

Je kutia nia ni kwa kutamka au moyoni tu inatosha?
Kwanza ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa nia mahali pake ni moyoni. Ama suala la kutamka kwa kauli za maulamaa wengi ni jambo ambalo halikuthibiti katika dini. Hivyo basi mwenye kufunga atatia nia moyoni mwake kwani Allah anajua yale yote yaliyomo ndani ya nafsi zetu na hakifichiki kwake kitu chochote.

Nakauli iliyo sahihi nikwamba kutamka niya ni BIDAA kwasababu nia nikatika matendo ya moyo.

2- KUJIZUIA KULA NA KUNYWA

Ni lazima kwa mtu mwenye kufunga ajizuie kula na kunywa kuanzia kuingia kwa alfajiri ya kweli hadi kuzama kwa jua.

Kwa kauli ya Allah (subhanahu wata‘ala): “Na kuleni na kunyweni mpaka kubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku, Kisha timizeni saumu mpaka usiku.” (Suratul Baqara : 187).

Nini hukmu ya kula kwa kusahau

Yule ambae atakula kwa kusahau iwe kidogo au sana basi haitobatilika funga yake kwa ushahidi wa hadithi ya Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema : Amesema Mtume (Swalla Allahu alayhi wa sallam): “Mwenye kusahau nae amefunga, basi akala au akanywa na aikamilishe funga yake.”

]Al Bukhariy na Muslim[.

Na katika riwaya nyengine “Kwani hakika Allah amemlisha na amemnywisha.” Ila Muislamu azingatie asije kujiigiza kuwa amesahau kwani ataweza kuwadanganya watu lakini Allah hawezi kumdanganya hata kidogo.

Je kupiga mswaki ndani ya Ramadhan kwa kutumia dawa inasihi?

Ama Kupiga mswaki ndani ya funga hilo linasihi kwani Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akipiga mswaki nae amefunga. Ama suala linakuja kwenye kupiga mswaki kutumia dawa.

Dawa ya mswaki haibatilishi swaum ikiwa wakati anasafisha meno atatema na wala hamezi. Ama ikiwa atakusudia kumeza, swaumu yake itabatilika.

Na yule ambae anakhofia anaweza kumeza basi bora asitumie dawa. Na kilichopendekezwa zaidi na maulamaa mtu apige mswaki kwa kutumia dawa kabla ya kuanza kwa saumu na itakapoingia saumu apige mswaki bila ya kutumia dawa ili asije kutumia dawa na kuimeza.

Je kuonja chakula wakati mtu amefunga inasihi?

Kuonja chakula wakati mtu amefunga inasihi kwa sharti ahakikishe kuwa hamezi kile alichokiweka kwenye ulimi kwa ajili ya kuonja.

Je kukoga katika mchana wa Ramadhan inasihi?

Kukoga au kukosha uso ikiwa mtu yumo kwenye funga inasihi. Ila ahakikishe maji hayaingii katika matundu ya mwili kama masikioni nk.

Ama yakiingia bila ya kukusudia hilo halina tatizo. Na yakiingia kwa kusudia basi atakuwa amefungua.

Ni ipi hukmu ya mwenye kufunga kutia dawa kwenye macho?
Anaruhusika kutumia na haitobatilika funga yake.

Nini hukmu ya kuchoma sindano wakati mtu amefunga?

Ikiwa sindano ni ya dawa tu basi haifunguzi. Ila sindano ikiwa imewekewa kitu chochote ambacho ndani yake kitampa mwenye kufunga nguvu kama glucose basi hapo itakuwa amefungua. Allah ni mjuzi zaidi.

3-KUJIZUIA NA KUJITAPISHA KWA MAKUSUDI

Pia ni wajibu kwa mwenye kufunga kujizuia na kujitapisha kwa makusudi. Ama akitapika bila ya kukusudia basi ataendelea na funga yake kama kawaida. Na akijitapisha kwa makusudi ni lazima ailipe funga hiyo.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu anhu) amesema: Amesema Mtume (Swalla Allahu alayhi wa sallam): "... na mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa." Bukhari na Muslim.


4-KUWA MUISLAMU
Ikiwa mtu sio Muislamu basi kwake yeye haimuwajibikii kufunga. Na akija kusilimu basi hatolipa kwa zile siku ambazo hakufunga kwani alipokuwa sio Muislamu haikumuwajibikia kufunga.
Ama Muislamu ambae ataritadi wakati amefunga basi moja kwa moja funga yake itabatilika na akija kutubu na kuamua kurudi kwenye Uislamu basi inamuwajibikia kuzilipa siku zote ambazo aliziwacha wakati ametoka kwenye Uislamu.

5-KUWA NA AKILI KATIKA MCHANA MZIMA WA RAMADHAN
Pia ili swaumu isihi lazima mwenye kufunga awe na akili na ikiwa atarukwa na akili basi funga yake itabatilika. Na hakuna tatizo kwa mtu kuzimia kwa muda mchache katika mchana wa mwezi wa Ramadhan.

 SHARTI ZA KUSIHI KWA FUNGA- SEHEMU YA PILI

3 – KUJIZUIA KUFANYA TENDO LA NDOA KWA MAKUSUDI NA KUJITOA MANII

Ikiwa mtu atafanya jimai bila ya kukusudia basi mtu huyo atakuwa amesameheka. Kwa kauli ya Allah:

...{وليْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُمْ بِهِ وَلَكِنْ مَا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا}

''Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu''

(Suratul Ahzaab : 5).

Ama yule ambae atafanya jimai kwa makusudi basi huyo funga yake itabatilika na itamlazimu kwake yeye kuilipa funga hiyo pamoja na kutoa kafara.

Kafara kwa yule ambae atafanya tendo la ndoa katika mchana wa Ramadhani ni :

i. Kuacha huru mtumwa.
ii. Kufunga miezi miwili mfululizo.
iii. Alishe maskini 60 kila mmoja kibaba kimoja.

Ikiwa mke au mume mmoja wao amemlazimisha kwa nguvu mwenzake kufanya tendo la ndoa ndani ya mchana wa Ramadhan na wamo katika funga basi yule aliemlazimisha mwenzake ndio itamuwajibikia kutoa kafara.

Na mwanamke hatakiwi akubali kufanya tendo la ndoa wakati amefunga ndani ya Ramadhani. Na maulamaa wengine wakaengeza kwa kusema hata ikiwa anaweza kupigana na mume wake basi ampige, Kuonesha uzito wa funga.

Na wala mtu asitumie kivuli kuwa amelazimishwa kujitetea ajue kuwa Allah (subhanahu wata‘ala) anajua kila kilichomo ndani ya nafsi ya mja wake.

Ikiwa mtu atafanya tendo la ndoa hali ya kuwa amefunga ndani ya Ramadhani kwa siku mbili tofauti basi ni juu yake kafara mbili. Kila funga moja basi na kafara yake moja.

Pia ikiwa mtu anafanya tendo la ndoa na baadae ikambainikia kuingia kwa alfajiri basi kinachotakiwa ni kuacha tendo la ndoa hapo hapo akakoge janaba na aendelee na funga yake.

Je ni wakati gani jimai ya mchana wa Ramadhani inaruhusika?

Ikiwa mke na mume wote wana dharura za kisheria za kutofunga kwa mfano wote wamesafiri basi hakuna ubaya na hawatotoa kafara. Kwani ruhusa ya kutofunga ishakuwepo kwao wao.

Ikiwa mume amerudi safari na mke wake hakufunga siku hiyo kwa sababu ya hedhi na ametwaharika baada ya funga kuanza, basi tendo la ndoa kwao wao linaruhusika kwani mume hajafunga na mke hakufunga.

Ama kinyume na hali hizo wakifanya tendo la ndoa ndani ya mchana wa Ramadhani wakiridhia wenyewe basi kwa kila mmoja juu yake kafara ama mmoja amemlazimisha mwenzake basi yule aliyemlazimisha mwenzake ni juu yake kutoa kafara.

Kujitoa maniii kwa makusudi kunabatilisha funga. Hivyo basi yeyote ambae amefunga anatakiwa ajizuie na kujitoa manii kwa makusudi. Na mfano wa kujitoa manii kwa makusudi ni puunyeto, au kwa kumkumbatia au kumchezea mkewe au mwanamke mpaka akatokwa na manii.

1-SUALI
Walifanya jimai kabla ya kuanza kwa funga na baadae hawakuwahi kukoga janaba wakalala mpaka ikaingia alfajiri. Je nini hukmu ya funga yao?
JIBU
Ikiwa walitia nia ya kufunga basi funga yao itasihi. Kinachowalazimu ni kukoga janaba ili waweze kuswali na waendelee na funga yao.

Na hili ni kwa ushahidi wa hadithi ya Bibi Aysha na Ummu Salamah (radhiya Allahu anhuma) “kwamba Mtume (Swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akiamka na janaba kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anakoga na kufunga.”

(Al Bukhariy na Muslim).

2-SUALI
Alifanya jimai bila ya kujua kwamba alfajiri imeingia. Na baadae akajua kuwa alifanya jimai wakati tayari alfajiri ishaingia. Nini hukmu yake?

Ikiwa wakati anafanya hajui kama wakati umeingia basi atakoga na ataendelea na funga yake. Kwani hakuna kosa kwa mtu kutojua.Ama akifanya kwa kusudi basi funga itabatilika funga yake na itamlazimu kutoa kafara na kuilipa funga hiyo.

4-KUEPUKANA NA HEDHI NA NIFASI

Ni lazima kwa mwanamke anaetaka kufunga awe ametwaharika kutokana na hedhi na nifasi. Na pindi mwanamke anapokuwa na hedhi au nifasi basi huwa ni wajibu kwake kuacha kufunga. Na hii ni amri kutoka kwa Allah (subhanahu wata‘ala) na mwanamke akitwaharika ataendelea na kufunga.

Pia siku ambazo ameziacha kwa kutofunga atakuja kuzilipa baada ya Ramadhani.


SUALI
Bado muda mdogo sana kumalizika kwa funga. Mwanamke akapatwa na hedhi. Je itahesabika funga yake ile?

JIBU
Hapana, haitohesabika funga ile kwa sababu wakati haujatimia. Na itamlazimu mwanamke huyo aje kuilipa funga hiyo baada ya kumalizika kwa Ramadhani.

SUALI
Mwanamke amepatwa na maumivu au dalili nyengine za kuonyesha atapatwa na hedhi ila hakupata wala hakutokwa na damu. Nini hukmu yake?
JIBU
Hatowajibika kuilipa na funga yake itakuwa sahihi.

SUALI
Ikiwa mwanamke siku zake za hedhi zimekaribia. Akaona matone ya damu ila damu haikutoka. Nini hukmu ya funga yake?
JIBU
Lazima ailipe funga hiyo kwani matone hayo ya damu yatahesabika kama ni damu ya hedhi.

SUALI
Miaka yote Ramadhan napata kufunga siku 10 tu au 11. Na zinazobaki nakuwa katika siku za hedhi. Sipati kufanya ibada ambazo zina fadhila kubwa kuliko miezi mingine. Nakuwa mnyonge kutokana na hali hiyo.
Je naweza kutumia vidonge vya kuzuia hedhi ?


JIBU
Kuhusu hedhi muda wake wajuu kabisa ni siku kumi na tano, zikizidi hapo huwa ni ugonjwa, kwa maelezo yako unakuwa ukitokwa na damu kwa takriban siku 20, hii inaonesha una tatizo jitahidi kutafuta tiba ya ugonjwa huo.

Ama ikiwa zitabaki siku 15 au chini ya hapo tutaizingatia kuwa ni hedhi, na kipindi unachokua ndani ya hedhi kuacha yale sheria iliokutaka kuyaacha ni ibada, hivyo ibada iliyokuzuilia kufanya ibada nyengine fadhila zake ni kubwa zaidi kwa wakati huo.

Pili.
Kuhusu kutumia vidonge vya hedhi wako maulamaa wanasema kuwa haifai kutumia vidonge hivyo kwani vimethibitika vina madhara.

Ama tukisema havina madhara basi ushauri wetu ni bora kuiacha hedhi katika utaratibu wake ndio bora zaidi kiibada na kiafya pia. Kwani ndio maumbile yake mwanamke alivyoumbwa na Allah (subhanahu wata‘ala). Na Allah ndie mjuzi zaidi.

SUALI
Ikiwa mwanamke amemaliza nifasi kwa siku chache mfano siku saba je anaweza kufunga?
JIBU
Ikiwa kweli imesita damu ya nifasi mwanamke huyo anaweza kufunga. Na Allah ni mjuzi zaidi.

SUALI
Ni ipi hukmu ya funga kwa mwanamke aliyeharibu mimba?
JIBU
Ikiwa mimba imeharibika kabla ya mtoto kuumbika basi damu hiyo si damu ya nifasi na mwanamke atakoga kujisafisha na kuendelea na funga yake.
Ikiwa mimba imeharibika baada ya mtoto kuumbika basi damu hiyo itakuwa ni ya nifasi na itambidi ajizuie kufunga mpaka pale itakaposita damu ya nifasi. Na Allah ni mjuzi zaidi.

SUALI
Mwanamke ametoharika kabla ya kuanza kwa alfajiri ya kweli. Akatia nia ya kufunga ila akachelewa kukoga josho. Je anaweza kufunga?
JIBU
Ndio anaweza kufunga. Kitakachomlazimu ni kukoga josho kabla ya kutoka kwa swala ya alfajiri ili asiache swala na ataendelea na funga yake. Na Allah ni mjuzi zaidi.

Hayo ndio masharti ambayo yanalazimika kutimizwa ili funga ya Muislamu isihi. Na kinyume cha masharti hayo ni kubatilika kwa funga hiyo. Na kama tulivyoeleza itamuwajibikia mtu huyo kulipa. Ama yule ambae kwa sababu ya kufanya tendo la ndoa yeye itamuwajibikia kulipa pamoja na kafara. Na Allah ni mjuzi zaidi.