MILANGO YA KHERI KATIKA RAMADHANI
Jamii ya vilivyomo
Vyanzo
Full Description
بسم الله الرحمن الرحيم
Imeandaliwa na Alhidaya.
Imepitiwa na Abubakari shabani Rukonkwa.
Ingia Katika Milango Mingi Ya Kheri Ramadhaan
Mwezi mtukufu wa Ramadhaan unakaribia kutufikia. Chukua fursa ya kujichumia thawabu nyingi kwa sababu malipo ya amali inayotekelezwa humo yanaanzia mara kumi mpaka mara mia saba. Juu ya hivyo, kuna malipo maalum yatokayo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ فَرْحَةٌ عِنْدَ فِطْرِهِ وَفَرْحَةٌ عِنْدَ لِقَاءِ رَبِّهِ وَلَخُلُوفُ فِيهِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ"
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu): ((Kila amali njema ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema: Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa.
Ameacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Kwa aliyefunga swawm atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Mola wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk))
[Muslim na Ahmad]
Kwanza kabisa inatupasa kutia niyyah ya ikhlasi moyoni (si kuitamka) kwa sababu ni sharti mojawapo la kutakabaliwa amali yoyote, na ili kupata Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) kama Anavyosema:
وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَة
Na hawakuamrishwa (chochote kile) isipokuwa wamwabudu Allaah mukhliswiyn (wenye kumtakasia) Dini, hunafaa[1] na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.
[Al-Bayyinah:5]
Weka azimio la nguvu kutekeleza amali zifuatazo katika mwezi wa Ramadhaan.
1-Kufunga Swawm kwa imaani na matarajio ili kufutiwa madhambi
قال صلى الله عليه وسلم: (( من صام رمضان إيماناً و احتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم
Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia ))
Al Bukhaariy na Muslim.
2-Qiyaamul-Layl (Kusimama usiku katika Swalah); Tarawiyh na Tahajjud
قال صلى الله عليه وسلم: ((من قام رمضان إيماناً واحتساباً، غفر له ما تقدم من ذنبه)) أخرجه البخاري ومسلم
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema: ((Atakayesimama [kwa Swalah ya usiku] kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
3-Kutoa sadaka
قال صلى الله عليه وسلم: ((أفضل الصدقة صدقة في رمضان))
أخرجه الترمذي عن أنس
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema:
((Sadaka bora kabisa ni ile inayotolewa katika mwezi wa Ramadhaan))
[At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas]
4-Kumfuturisha aliyefunga Swawm:
قال صلى الله عليه وسلم: ((من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema: ((Atakaye mfuturisha aliyefunga Swawm, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga))
[Ahmad, An-Nasaaiy – Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا ﴿٨﴾ إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا ﴿٩﴾ إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا ﴿١٠﴾ فَوَقَاهُمُ اللَّـهُ شَرَّ ذَٰلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا ﴿١١﴾ وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا ﴿١٢﴾
Na wanalisha chakula juu ya mapenzi yao (kwa hicho wanacholisha) masikini na mayatima na mateka. “Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Allaah, hatutaki kwenu jazaa na wala shukurani. “Hakika sisi tunakhofu kwa Mola wetu siku inayokunjisha uso ngumu nzito. . Basi Allaah Atawakinga na shari ya siku hiyo, na Atawakutanisha na mng’ao na furaha. Na Atawalipa Jannah na (nguo za) hariri kwa kusubiri kwao.
[Al-Insaan: 8-12]
Vile vile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
()أيما مؤمن أطعم مؤمناً على جوع أطعمه الله من ثمار الجنة ومن سقى مؤمناً على ظمأ سقاه الله من الرحيق المختوم )) رواهالترمذي بسند حسن .
((Muumin yeyote atakayemlisha Muumin mwenzake mwenye njaa, Allaah Atamlisha katika matunda ya Peponi, na atakayemnywesha Muumin mwenye kiu Allaah Atamnywesha kutoka katika 'Rahiyqul-Makhtuum' [Kinywaji safi kilichofunikwa kwa kizibo madhubuti])) [At-Tirmidhiy na Isnaad yake ni nzuri]
5-Kusoma Qur-aan kwa wingi na kujifunza maana yake.
Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَان
Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hidaaya kwa watu na hoja bayana za Hidaaya na Al-Furqaan (Upambanuzi). [Al-Baqarah: 185]
Jitahidi ndugu Muislam uzidishe kusoma Qur-aan na ujitahidi kukhitimisha japo mara moja katika mwezi huu. Jibriyl (‘alayhis-salaam) alikuwa akimfikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kumsikiliza na kumfundisha Qur-aan katika mwezi wa Ramadhaan. Vile vile Maswahaba na Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) walikuwa wakijihimiza sana kusoma Qur-aan katika mwezi wa Ramadhaan; 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akikhitimisha Qur-aan kila siku moja. Na baadhi ya Salaf wakikhitimisha Qur-raan kila siku tatu katika Qiyaamul-layl. Wengineo walikuwa wakikhitimisha siku saba, na wengine siku kumi. Na walikuwa wakiisoma katika Swalah na nje ya Swalah.
6-Kukaa kwa kumdhukuru Allaah baada ya Swala ya Alfajiri hadi jua litoke
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم، أنه قال: ((مَنْ صَلَّى الفَجْرِ في جَماعَةٍ ثُمَّ قَعَدَ يَذْكُرُ الله تَعالى حتَّى تَطْلُعَ الشَمْسُ، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ كانَتْ كأجْرِ حَجَّةٍ وَعُمْرَةٍ تامَّةٍ تامةٍ تامةٍ)) أخرج الترمذي وصححه الألباني
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili))
[Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy].
(Kuswali Jama'ah kumesisitizwa kwa wanaume, ama mwanamke anaweza naye kupata ujira wa thawabu zilizotajwa akiswali nyumbani kwake)
Thawabu hizo za kama Hajj na ‘Umrah ni katika siku za kawaida ndugu Muislamu, seuze mwezi wa Ramadhaan? Usiache fursa hii ikupite. Ukishindwa kuitekeleza kila siku, basi jitahidi japo wiki mara moja, hapo utakuwa una thawabu za Hajj na 'Umrah mara nne kwa mwezi, na ukiendelea hivyo miezi yote kumi na mbili basi utakuwa na thawabu za Hajj na 'Umrah mara 48 kwa mwaka.
7- Kubakia Masjid kwa ajili ya Itikaaf:
عن عائشة – رضي الله عنها- قالت "كان النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً - أخرجه البخاري
Kutoka kwa 'Aashah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)alikuwa akikaa Itikaaf kila Ramadhaan katika siku kumi za mwisho, na mwaka ambao aliondoka duniani alikaa Itikaaf siku ishirini.
[Al- Bukhaariy]
Unapokuwa umo katika I'itikaaf utaweza kutekeleza amali nyingi zitakazokufanya ubakie katika taqwa na iymaan kuzidi moyoni. Utaweza kusoma Qur-aan kwa wingi, kuswali Swalaah za Sunnah, kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kuomba du’aa na maghfira. Fadhila za I’tikaaf zinazidi inapokuwa katika kumi la mwisho kwa sababu ya usiku mtukufu unaojulikana kama ni: ’Laylatul-Qadr’.
8-'Umrah katika mwezi wa Ramadhaan
Ukiwa na uwezo, tekeleza ‘Umrah. Imethibiti katika Hadiyth ya Mtume (walla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba thawabu za kutekeleza 'Umrah katika Ramadhaan ni sawa na thawabu za kutekeleza Hijjah.
((عمرة في رمضان تعدل حجة)) أخرجه البخاري و مسلم
(('Umrah katika Ramadhaan ni sawa [kwa thawabu] na Hijjah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
9-Kupata Baraka za Suhuwr (Daku)
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( تسحروا فإن في السحور بركة )) رواه البخاري ومسلم
((Kuleni daku kwani katika huko kula daku, kuna baraka)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
10-Kuomba Du'aa
Ramadhaan ni mwezi wa Du'aa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anataja kuhusu kumuomba du’aa baada ya kutufaridhisha Swawm:
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ
Na watakapokuuliza (Ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Qariyb (Yu karibu daima kwa elimu Yake); Naitikia maombi ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka.
[Al-Baqarah:186]
Zinaendelea Aayah za kuhusu Swawm baada yake.
11-Kuomba maghfirah na tawbah:
Omba maghfira na tawbah kabla ya alfajiri. Kufanya hivi utakuwa miongoni mwa waja wema Anaowasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
وَبِالأَ سْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ
Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira
[Adh-Dhaariyaat: 18]
Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Huteremka nyakatii hizo kuweko katika mbingu ya kwanza:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له)) رواه البخاري ومسلم
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’ala Huteremka kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfira Nimghufurie?))
[Al-Bukhaariy Na Muslim]
12-Kuunga undugu na jamaa:
Jambo muhimu kulitekeleza siku zote. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha kwa anayekata mawasiliano na ndugu au jamaa:
((الرحم معلقة بالعرش، تقول: من وصلني وصله الله ، ومن قطعني قطعه الله )) رواه البخاري ومسلم
((Fuko la uzazi linaning'inia katika 'Arshi linasema: “Atakayeniunga, Allaah Atamuunga, na atakayenitenga Naye Allaah Atamtenga [Atamkatia]”))
[Al-Bukhaariy na Muslim]
13- Kukesha siku kumiza mwisho:
Utaweza kudiriki Laylatul-Qadr, usiku ambao ‘ibaadah yake ni bora kuliko ‘ibaadah utakazoifanya miezi elfu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ ﴿٢﴾ لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾
Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatil-Qadr (usiku wa cheo). Na nini kitakachokujulisha ni nini huo (usiku wa) Laylatul-Qadr? (Usiku wa) Laylatul-Qadr ni (usiku) mbora kuliko miezi elfu Wanateremka humo Malaika na Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri (jambo). (Usiku huo ni) Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 97]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atujaalie tawfiyq kutekeleza yote hayo na Atutakabalie. Aamiyn.
1- Wakielemea haki na kujiengua na upotofu