Fadhila za mwezi wa Rajab na yaliyozuliwa ndani yake
Jamii ya vilivyomo
Full Description
بسم الله الرحمن الرحيم
Mwezi Wa Rajab:Fadhila Zake Na Yaliyozuliwa Ndani Yake
Muhammad Baawazir
Imepitiwa na Abubakari shabani Rukonkwa.
Tunamshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa Kutupa umri wa kufika katika mwezi mtukufu wa Rajab, na Atujaalie uzima na afya tukutane tena na kipenzi chetu kitukufu Ramadhaan.
Anasema Allaah:
((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ)).
((Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo)) [At-Tawbah: 36]
عن أبي بكرة - رضي الله عنه - أن النبي صلى الله عليه وسلم خطب في حجة الوداع وقال في خطبته إن ((الزمان قد استدار كهيئة يوم خلق السماوات والأرض السنة اثنا عشر شهرا منها أربعة حرم ثلاث متواليات ذو القَعدة وذو الحجة والمحرم ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان )) رواه البخاري
Kutoka kwa Abu Bakrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alitoa Khutbah yake ya mwisho akasema: ((Wakati umemaliza mzunguko wake kama vile siku Allaah سبحانه وتعالى Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka ni miezi kumi na mbili, ambayo ndani yake kuna minne ni mitukufu, mitatu inafuatana, Dhul-Qa’dah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab upo baina ya Jumaada na Sha'abaan))
[Al-Bukhaariy[
Na Anasema Allaah:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُحِلُّواْ شَعَآئِرَ اللّهِ وَلاَ الشَّهْرَ الْحَرَام))
((Enyi mlioamini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Allaah wala mwezi mtakatifu)) [Al-Maaidah: 2]
Hapana shaka kutokana na Aayah hizo kwamba miezi hii minne mitukufu hutakiwa kutukuzwa inavyopaswa, kwa kutokufanya maasi na kudhulumiana, kwani malipo ya kufanya madhambi katika miezi hii mitukufu huwa ni makubwa zaidi. Katika kuiheshimu pia ni kumcha Allaah zaidi kwa kila aina ya ibada. Lakini sio kwa kuchagua siku maalumu ambazo watu wametenga kwa ajili ya kusherehekea na kumshukuru Allaah kutokana na kuaminika utukufu wa siku hizo au matukio yake ya kihistoria.
Mifano ya mambo yanayotendeka katika mwezi huu ambayo hayana uthibitisho kutoka katika Qur-aan wala Sunnah Sahihi:
· Kuitukuza siku inayosemwa ni ya Mi’iraaj au Israa na Mi’iraaj (ambayo inadaiwa na wengi kuwa ilikuwa katika mwezi huu wa Rajab, na kudaiwa ni tarehe 27) kwa kufunga hasa siku hii pekee.
· Baadhi ya watu wameanzisha Swalah ambayo wameiita Swalaat Ar-Raghaaib, ambayo huswaliwa mwanzoni mwa mwezi huu. Hii ni kama ile hali ya mwezi wa Sha'abaan na haswa katikati yake ambayo watu wamezusha jina liitwalo Laylatul Baraat (wakisema ni usiku wa ahadi na kusamehewa waliokufa au ni usiku wa kuwekwa mbali na madhambi) ambapo watu hufanya ni usiku wa ibada na kuswali sana na kufunga mchana wake.
· Watu wametunga du'aa na aina ya Istighfaar na dhikr mbali mbali kuwa ni maalumu zisomwe katika mwezi huu wa Rajab.
· Kuzuru makaburi.
· Watu kujumuika na kufanya mihadhara na kupeana mawaidha ya kuelezana historia ya tukio la Israa na Mi'iraaj.
Hizi ni sherehe na mipangilio ya ibada ambayo hayamo katika shari'ah katu, na wala hazijathibiti katika ushahidi sahihi sehemu yoyote katika vyanzo vya kutegemewa. Ni mambo ya uzushi ambayo baaadhi ya watu wameyazusha kwa ajili ya kuzitukuza siku hizo kutokana na kudhani kufanya hivyo kutawapatia ujira na kuwaongezea daraja yao ya Dini.
Ukifanya utafiti na kupitia katika maandiko yenye kutegemewa, utakuta hakuna uthibitisho wa kusherehekea na kufanya ibada zozote maalum katika siku hiyo na usiku huo. Pia hakuna ushahidi sahihi wa kufunga Swawm katika siku hiyo ya tarehe 27 ya mwezi wa Rajab. Kama ambavyo hakuna kitu kiitwacho Laylatul Baraat ambayo baadhi ya watu wameiita hiyo siku ya katikati au tarehe 15 ya mwezi wa Sha'abaan, ambao ni usiku wa masiku yenye fadhila ambao Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:
((Allaah Anawatazama viumbe wake katika usiku wa kumi na tano wa Sha'abaan na kisha huwasamehe ila wale washirikina au wale wenye kuwa na Uadui))
Hakuna ushahidi na ukweli halisi wa kuwa usiku huo wa safari tukufu ya Mtume wetu صلى الله عليه وآله وسلم ya Israa na Mi'iraaj, kuwa ulikuwa ni katika siku hii ya tarehe 27 ya Rajab, na hata kama ikisemwa kuwa ilikuwa ni siku hiyo na wasio na ushahidi, bado hakuna mafundisho yoyote yenye kutueleza kuwa tunapaswa kufunga katika siku hii. Bali tutakapofanya hivyo, tutakuwa tumezua jambo lililo nje ya shari'ah. Hata hivyo, haikatazwi kwa mtu aliyezoea kufunga Jumatatu na Alkhamiys kufunga Swawm yake ikiwa imeeangukia katika siku hii ya tarehe 27 ya Rajab, au Swawm ya masiku meupe au kulipa madeni yake n.k.
Na kama kuna masiku yenye kushukuriwa na ambayo yamepaswa kukumbukwa kwake kwa kufunga Swawm, basi ni ile siku ya tarehe kumi ya mwezi Muharram au 'Aashuraa ambayo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaamrisha Maswahaba zake kuifunga kwa ajili ya kumshukuru Allaah kwa Kumuokoa Nabii Muusa عليه السلام kutoka katika balaa la Fir'awn na jeshi lake. Na lisingekuwa jambo gumu au kushindikana kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kutufundisha sisi au kutuamrisha kufunga katika siku hii ya 27 ya Rajab kama angetaka, kama alivyotuamrisha kufunga Swawm ya 'Ashuraa na siku kabla yake au baada yake. Lakini hakufanya hivyo! Na maadam hakutuelekeza kufanya hivyo, na yeye hakufanya hivyo, basi hakuna maana ya sisi kuwa mahodari na mafundi wa kujipangia mambo ambayo mbora wetu hakuyaonea umuhimu kwetu kuyafanya.
Ama ya kukusanyana katika siku hiyo ya tarehe 27 Rajab, kwa ajili ya kupeana mawaidha na kuelezana historia ya tukio hilo, ni bora liepukwe na ni vizuri kuwahimiza watu kuhudhuria madarsa Misikitini na mihadhara ili waweze kuyajua hayo na mengi mengine ambayo ni muhimu zaidi katika Dini yao. Kuwepo kwa minasabaat kama hiyo ya kukusanyana kila linapotokea tukio, kunafungua milango ya uzushi na kuifanya Dini kuwa na mambo mengi na mazito hadi yale ya muhimu na yenye faida zaidi yakaachwa na kuendekezwa hayo ya mpito. Leo hii tuna mifano mingi ya matukio sampuli hii kama vile sherehe na mikusanyiko ya Mawlid, sherehe za nusu Sha'abaan, sherehe za mwaka mpya wa Kiislam n.k.
Hata kwenye baadhi ya kalenda kumewekwa siku hizo kama ni siku za sikukukuu. Na tunaona leo hii hata baadhi ya nchi zetu zisizo na dini kama zinavyodai, zimeweka sikukuu rasmi ya Mawlid, na kuwapa Waislam mapumziko! Waislam wengi wamefurahi kuona kuwa wametambulikana na 'kuthaminiwa', lakini hakika ni kinyume na hivyo. Serikali hizo janja zimefanya hivyo makusudi kuwalewesha Waislam na hayo yasiyo na msingi ili yazidi kuwabana na kuwanyima zile haki zao za msingi. Ikiwa serikali hiyo hiyo inamuua Muislam na kuwajeruhi wengine kwa kuswali Swalah ya 'Iyd kwa kuonekana mwezi popote duniani, na huku inajifanya kumpa Muislam siku maalum ya kusherehekea Mawlid, je, ina lengo gani? Je, inaathirika na nini kwa Waislam kutangulia au kuchelewa kuswali 'Iyd, kama sio kutafuta fursa na upenyo popote pale ya kumnyanyasa Muislam na kumdhalilisha.
Ikiwa inamwekea Muislam sheria na kudai ni za kigaidi, na katiba za kumnyima haki zake na kumnyanyasa na kubana uhuru wake wa kuabudu na kutangaza Dini ya Allaah, je, inakutakia kheri gani Muislam kwa kukupa siku ya ziada kwa kusherehekea mazazi ya Mtume? Ikiwa ndio hiyo hiyo iliyowapiga virungu, risasi na kuua Waislam na kuwadhalilisha Waumini Msikitini bila kuwastahi kinamama, leo itakuwa inakuthamini vipi wewe? Suala ni kuwafumba Waislam macho kwa yasiyo ya msingi na kuwashughulisha nayo ili wabaki wamelala na wasidai haki zao au kuzipigania. Na kwa masikitiko makubwa, Waislam wengi wametumbukia katika hila hizo ndogo sana zinazosukwa na serikali hizo zikisaidiwa kwa upana na taasisi za 'Kiislam' zilizoundwa na serikali hizo.
Amiyrul-Muuminiyn ‘Umar رضي الله عنه alikuwa akikataza watu kufunga mwezi huu kwa sababu ilihusiana na kushabihiana na Ujahiliya.
Inaelezwa Kwamba Kharashah ibn al-Harr alisema: "Nimemuona ‘Umar akiwachapa mikono wale waliokuwa wakifunga Rajab walipokuwa wanafikia chakula chao na alikuwa akisema, huu ni mwezi walioufanya mtukufu katika Ujahiliya" [al-Irwaa’, 957; Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Sahihi].
Imaam Ibnul Qayyim رحمه الله amesema katika kitabu chake cha Zaadul Ma'ad:
''Hakuna ushahidi ulio wazi wa kuwa ni mwezi au tarehe gani tukio hili lilitokea. Kuna taarifa nyingi kuhusiana na jambo hili (kuwa lilifanyika mwezi huu wa Rajab) lakini hakuna hata moja katika taarifa hizo yenye uamuzi kamili na sahihi. Na hakuna ibada zozote maalum zenye kufungamana nayo.''
Kwa ujumla siku zote za Muislam ni nzuri na bora kwa kuwa Allaah سبحانه وتعالى Huwa Anashuka kila usiku katika fungu la tatu la usiku kama Hadiyth inavyoeleza:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له)) البخاري
Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وسلم amesema: ((Allaah سبحانه وتعالىHuteremka kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfira Nimghufurie? )) [Al-Bukhaariy]
Kuna masiku mengi yenye fadhila kama masiku ya mwezi wa Ramadhaan ambao unatukaribia, masiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah ambapo ibada ya hija inaanza, na haswa zaidi siku ya 'Arafah, pia siku ya tarehe kumi ya mwezi wa Muharram ambayo tumeitaja hapo juu. Siku za Jumatatu na Alkhamiys, Ayyamul-Biydhw (masiku meupe au masiku ya usiku ung'aao -tarehe kumi na tatu, kumi na nne na kumi na tano za kila mwezi). Miezi minne mitukufu (ambayo ni Dhul Qa'adah, Dhul-Hijjah, Muharram na Rajab). Masiku hayo hapo juu ni siku zenye kupendeza kufunga (ila sio kuihusisha siku maalum kama hiyo ya tarehe 27 kufunga katika mwezi Rajab na hali haina uthibitisho kufanya hivyo) Kufunga siku ya 'Arafah inapendezewa sana kwa yule ambaye haitekelezi ibada ya Hijjah kwa wakati huo. Masiku kumi ya Dhul-Hijjah yana fadhila zaidi kuliko masiku mengine. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn 'Abbaas رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا amesema:
((Hakuna matendo mazuri yafanywayo katika masiku mengine yakawa bora kuliko yafanywayo katika masiku haya (ya mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah)''. Kisha baadhi ya Maswahaba wakamuuliza: ''Kuliko hata Jihaad?'' Akawajibu: Kuliko hata Jihaad, isipokuwa tendo la mtu atakayefanya kwa kujiingiza hatarini yeye na mali yake (kwa ajili ya Allaah) na harejei na chochote katika hivyo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Masiku kumi ya mwisho ya mwezi wa Ramadhaan ni matukufu zaidi kuliko michana kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah na masiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah ni matukufu zaidi kuliko michana ya mwezi wa Ramadhaan. Haya ni maoni yenye nguvu ya Maulamaa. Ama siku iliyo bora kuliko zote basi ni siku ya 'Arafah, kwani imesimuliwa kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisema:
((Hakuna siku iliyo na fadhila kuliko zote mbele ya Allaah kama siku ya 'Arafah))
Mifano hiyo ni kuonyesha kuwa masiku yaliyotajwa hapo juu ni bora kwa Muislam na yaliyo munasibu kwa kumwabudu Allaah سبحانه وتعالى. Na Allaah سبحانه وتعالى Kazipa ubora baadhi ya nyakati kuliko zingine kwa kumpa tu mtu fursa ya kufanya zaidi matendo mema kwa kadiri awezavyo, na matendo hayo ni muhimu kwa Muislam kwa maisha yake ya hapa duniani na Akhera. Na ukitazama utakuta yote yamewekwa wazi na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na jinsi ya kutekeleza ibada katika masiku au nyakati hizo. Ama zile ambazo hazijatajwa na kuwekwa wazi basi ni bora na vizuri tuziache na kujiepusha na kufanya matendo ndani yake ambayo hatukufundishwa. Nako kutakuwa bora katika Dini yetu na hadhi yetu, kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika Hadiyth iliyosimuliwa na An-Nu'uman bin Bashiyr رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا kuwa:
عَنْ أَبِي عَبْدِ اللَّهِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وآله وسلم يَقُولُ: (... فَمَنْ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ فَقَدْ اسْتَبْرَأَ لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ ... ) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
((...atakayekaa mbali na utata, basi atakuwa ameilinda (ameitakasa) Dini yake na heshima yake...)).
[Al-Bukhaariy]
Wa Allaahu A'alam