×
Hiki ni kitabu kilichotayarishwa kwa lengo la kuwapatia wasomaji, suluhisho la matatizo wanayoyapata watu wengi wanapotaka kufahamu ni ipi Dini ya Haki.

 RISALA FUPI YA KUMUWEZESHA MTU KUPAMBANUA NI IPI DINI YA HAKI

RISALA FUPI

copyright © Hidaya Creativity, publishing Department.

P.O. BOX 44799, 00100, GPO, NAIROBI-KENYA.

Haki ya kunakili imehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga,

Kunakili, kutafsiri, kupigisha chapa au kukitoa kitabu

Hiki kwa jinsi au namna yoyote ile bila ya idhini ya

Hidaya Creativity kwa maandishi.

Mwandishi: Saleh M. Kyambo.

  

 

 RISALA FUPI

 YA KUMUWEZESHA MTU KUPAMBANUA

 NI IPI DINI YA HAKI

 UTANGULIZI

Kama inavyojulikana, katika dunia kunazo Dini nyingi sana lakini katika Dini hizo zote, kunazo tatu (mashuhuri) ambazo zinao uhusiano.

Dini zenyewe ni UYAHUDI, UKRISTO na UISILAMU.

 SEHEMU YA KWANZA

WAISLAMU NA WAKRISTO NI KAMA NDUGU.

UHUSIANO WAO NI UPI?

Kwanza: Mungu wao, aliyetajwa katika vitabu vyao, ni MUNGU WA MBINGUNI.

(hivi kwamba, hata akisikika yeyote katika wafuasi wa Dini hizi akisema “Mungu wangu” au “Mungu wetu ni fulani wa fulani,” itabaki katika vitabu vyao kwamba, Mungu wa mbinguni ndiye pekee Mungu wa kweli.)

MWANZO 24:7

Bwana Mungu wa mbinguni, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na akasema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akasema Nitawapa uzao wako nchi hii

.

MATHAYO 22:35-38

Mmoja wa wao (Wayahudi, wafarisayo), Mwanasheria akamwuliza (Yesu) akimjaribu, (36) Mwalimu katika Torati ni Amri ipi iliyo kuu? (37) (Yesu) akamwambia, mpende BWANA Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote (38) Hii ndiyo Amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

KUTOKA 20:1-4

Mungu akanena maneno haya yote akasema 2.Mimi ni BWANA Mungu wako, Niliyekutoa katika nchi ya Misr, katika nyumba ya utumwa 3. Usiwe na miungu mingine ila mimi 4. usijifanyie Sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala majini chini ya dunia, usivisujudie wala kuvitumikia;

MWANZO 24:48

Nikainama nikamsujudia BWANA, nikatukuza BWANA Mungu wa bwana wangu Ibrahimu.

.

 SEHEMU YA PILI

MUNGU MMOJA NA MITUME WANADAMU.

Uhusiano wa pili: Upo katika Mitume wa Mungu ( huyu wa Mbinguni ).

Yaani, Mitume wa Wayahudi ndio pia Mitume wa Wakristo na vile vile ndio pia Mitume wa Waisilamu

Kwa mfano, utaona katika mafundisho ya Dini hizi, Adam na mkewe Hawa wametajwa kwamba ndio watu wa kwanza.

Mtume Nuhu, kwa mfano mwengine, utaona ametajwa kote kote kwamba, alitengeneza Safina kwa amri ya Mungu na Watu wa enzi yake wakaangamizwa kwa mvua kali na mafuriko, kwa sababu ya kumuasi Mungu, na kutoamini maneno ya Nuhu.

Mitume wengine kama vile Nabii Ibrahim pia wametajwa, na Nabii Lut ambaye watu wa enzi yake waliangamizwa kwa sababu ya kumuasi Mungu, kwa kuwa walikuwa wakizini baina ya wanaume kwa wanaume wenzao, na walikataa pia kumtii Mtume wao Lut.

Mitume kama vile Yakubu (anayeitwa pia Israeli) ametajwa na wanawe akiwemo Yusuf (Joseph) na Benyamin (Benjamin). Kisa cha Yusuf kimetajwa tangu alipouzwa kama Mtumwa nchini Misri (kutokana na wivu wa ndugu zake) hadi akafikia kuwa kiongozi katika viongozi wa nchi hiyo.

Mtume Musa (Moses) na Daudi (David) na vile vile Suleiman (Solomon) wametajwa katika mafundisho ya Dini zote hizi, na Mitume wengineo.

JE TOFAUTI ZAO ZIPO WAPI?

 SEHEMU TA TATU

WAYAHUDI WAVUNJA AMRI YA KWANZA.

Wayahudi ndio wa kwanza kufanya makosa, kwa kutengeneza Ndama wa Ngombe (wa Dhahabu) na kisha wakamuabudu kama anavyoabudiwa Mungu wa Mbinguni. Na pia walikuwa hawayaamini maneno ya Musa kikamilifu.

Kumbukumbu la torati 9:16

Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu, mmefanya ndama ya ngo’mbe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru BWANA.

Isaiya 43:10-11

Ninyi ni mashahidi wangu, Asema BWANA, na mtumishi wangu niliyemchagua; mpate kujua, na kuamini na kufahamu ya kuwa Mimi Ndiye; kabla yangu hakuumbwa mungu awaye yeyote wala baada yangu Mimi hatakuwapo Mwingine 11. Mimi, naam, Mimi, ni BWANA, zaidi yangu Mimi hapana mwokozi.

Je! walikuwa na sababu gani ya kuabudu sanamu?

Sanamu kama tunavyomjua anayo macho lakini je! anaona chochote kwa hayo macho? La! Na pia anayo masikio, je! anasikia chochote kwa hayo masikio? La! Na pia anao mdomo, je! anatamka chochote? La!

Sanamu akianguka kwa mfano, je! anaweza kujisaidia kwa kurudi alipokuwa? La!

Kwa hivyo, ikiwa tunajua kwamba sanamu hawezi hata kujisaidia mwenyewe, je! wanaomuabudu wakitaka awasadie huwa wanataraji sanamu ataweza kuwasaidia vipi?

 SEHEMU YA NNE

KOSA LA KUABUDU SANAMU.

Kosa la kuabudu Sanamu ndilo kosa kubwa kuliko makosa yote, kwa sababu linalomtoa mtu katika Dini ya Mungu, kwa kuwa (anayefanya kosa kama hilo huwa) amevunja Amri ya kwanza ya Mungu, (yaani anakuwa kafiri) MSHIRIKINA.

 Walawi 19:4

Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyie miungu ya kusubu, mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

 Nehemia 9:16-17

Lakini wao na baba zetu wakatakabari (wakafanya kiburi) wakafanya shingo zao kuwa ngumu (hawaswali, hawasujudu) wala hawakusikiliza amri zako 17. ila wakakataa kutii wala hawakuyakumbuka maajabu yako uliyoyafanya kati yao lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu.

 SEHEMU YA TANO

WAYAHUDI WAUWA MANABII

Basi (kizazi cha) Wayahudi hawa hawa walifanya na makosa mengine ya kuwa wanawauwa Manabii (waliotumwa na Mungu), mmoja baada ya mwengine, hadi mwisho wakafanya na kosa kubwa sana, kosa la kumkataa Mtume wa Mungu, Yesu kristo (Nabii Isa Mwana wa Mariam), na hali ya kuwa alikuwa ametumwa kwao. Na wao pia ndio waliopanga kumuuwa. (Ikiwa walifaulu au hawakufaulu kumuuwa, hayo tutayaona baadaye.)

Nehemia 9:26

Walakini hawakukutii wakaitupa sheria yako nyuma yao wakawauwa manabii wako.....

Luka 19:47-49

Naye (Yesu) akawa anafundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu (viongozi wa kiyahudi) walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza;

Yohana 7:19

(Yesu akasema) Je! Musa hakuwapa Torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye Torati. Mbona mnatafuta kuniua?

Yohana 7:1

Na baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya, maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta (ili) kumwua.

Makosa ya Wayahudi hadi hapa tunaona kwamba, kwanza ni kuvunja Amri ya kwanza ya Mungu, kitendo kinachompelekea aliye kitenda kupata Laana kubwa, Laana ya Mungu, kama ilivyoandikwa katika Biblia,

kumbukumbu la torati 27:15

Na alaaniwe afanyae sanamu, watu wakajibu Aamiin.

Kumbukumbu la torati 28:15

Lakini itakuwa usipotaka kusikiza sauti ya BWANA Mungu wako usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na Amri zake Ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata, utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani,

Kumbukumbu la torati 27:26

Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya Torati hii kwa kuyafanya na watu wote waseme Aamiin

Makosa ya pili ni kuwauwa Manabii waliotumwa na Mungu, kama kwamba Wayahudi hawa wanawaambia, “Maneno mliyokuja nayo, mkisema ni kutoka kwa Mungu, sisi tutawauwa kwa sababu maneno yenu (tunavyoyaelewa sisi) ni uwongo.”

katikaYohana 7:12

Wayahudi wasema Yesu ni muwongo anadanganya watu

Watu waliopata Laana ya Mungu, hujulikana kwa maneno yao au kwa vitendo vyao.

Luka 11:43

(Yesu akasema) Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. 44. Ole wenu kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana (yaliyokificha), ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.

 SEHEMU YA SITA

WAYAHUDI WAKATAA KUIPOKEA INJILI.

Warumi 2:17

Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea Torati, na kujisifu katika Mungu, 18. na kuyajua mapenzi yake; na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika Torati, 19. na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, 20. mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika Torati; 21. basi wewe umfundishaye mwengine, je! Hujifundishi mwenyewe?

Luka 19:47

Naye (Yesu) akawa akifundisha kila siku Hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza.

Walipokataa Wayahudi kuipokea Injili ya Yesu, waliichukua Waroma kiasi walichoweza kuipata, kwa sababu wao ndio waliokuwa wakiwatawala Wayahudi enzi hizo.

Waroma kabla ya hapo walikuwa Makafiri (yaani watu wanoabudu sanamu na pia miungu wengi, hawafuati Mila ya Nabii Ibrahim, na kwa hivyo hawatahiri.) na wao ndio walioanzisha Dini ya ROMAN CATHOLIC.

Roman maana yake ni watu wa nchi ya Italia, yaani Wataliano. Na Catholic maana yake UNIVERSAL au INTERNATIONAL (UROMA WA KIMATAIFA).

Nehemia 5:8

Nikawaambia, sisi kwa kadiri ya uwezo wetu tumewakomboa Ndugu zetu Wayahudi, waliouzwa kwa Makafiri;

Matendo ya Mitume 15:1

Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.

Swali: je! Waroma waliendelea na kuhubiri Dini aliyokuwa akihubiri Yesu?

Au walichanganya mila yao na Dini hiyo mpya?

Je! Roman Catholic inamaanisha sote tuwe Wataliano?

Kama ni hivyo je! Ni ki-lugha au ki-tabia au ki-Ibada?

Mathayo 5:17-18

 (Yesu akasema) Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au manabii; La! Sikuja kuitangua bali kuitimiliza 18. Kwa maana, amin nawaambia, Mpaka Mbingu na Nchi zitakapoondoka, yodi moja au nukta moja ya Torati, haitaondoka hadi yote yatimie.

 SEHEMU YA SABA

WAKRISTO WAFUATA NYAYO.

Wakristo nao walifanya kama walivyofanya Wayahudi, kwa kumkataa Mtume wa mwisho Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, alipotumwa, na hali kuja kwake kumetabiriwa katika TAURATI ya Wayahudi na INJILI.

 Kumbukumbu la Torati 18:17-19

Bwana akaniambia wametenda vyema kusema walivyosema 18 Mimi Nitawatolea Nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe (Musa) Nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayowaamuru 19 hata itakuwa mtu asiyesikia maneno ya yangu atakayosema yule (Nabii) kwa jina langu, nitalitaka kwake.

Yohana 1:19-21

19 Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake Makuhani na Walawi kutoka Yerusalem ili wamuulize wewe u nani? 20 Naye akakiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye kristo. 21 Wakamuuliza Ni nini basi? ﷻ‬ Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe ﷻ‬ Nabii yule? Akajibu La

Qur’an 7:158

Sema (Ewe Nabii Muhammad): “Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote; (Mungu) ambaye anao ufalme wa mbingu na mbingu na ardhi; hapana aabudiwaye ( kwa haki )ya kuabudiwa ila yeye; yeye ndiye ahuishaye na ndiye afishaye. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, aliye Nabii Ummy, (asiyejua kusoma na wala kuandika) ambaye humuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka.”

Yohana 15:26

(Yesu akasema) Lakini ajapo huyo msaidizi nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba yeye atanishuhudia

Matedo ya Mitume 7:37

Musa huyo ndiye aliye waambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni Nabii, katika ndugu zenu kama mimi; msikieni yeye.

Mathayo 21:42-45

Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko,

Jiwe walilokataa waashi (mafundi) hilo ndilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? 43 Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu (Wayahudi) nao (huo ufalme) watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake

45. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake walitambua ya kuwa anaongea juu yao.

Sababu walizotoa viongozi wa kikristo za kumkataa Mtume Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, zinafanana na zile walizotoa Wayahudi za kumkataa Yesu kristo. Na kama walizotoa viongozi wa Umma (yaani Generation) zote zilizo wapinga Mitume wao. (Yaani kumtangaza Mtume wa Mungu kuwa Muwongo, kumkadhibisha.)

Angalia Yohana 7:12

Utaona kwamba Wayahudi hawakuona kule kusema Yesu (Nabii Isa) ni muwongo, kuwa ni jambo kubwa au kuwa ni la ukafiri. Pamoja na ushahidi wote aliouleta na hasa kitabu cha Injili.

Wakristo nao walisema imeandikwa katika kitabu chao kwamba kutakuja mitume wa uwongo na wakawa wanasema Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, ni mmoja wao.

 SEHEMU YA NANE

JE! MUHAMMAD NI MTUME WA UWONGO?

Sasa nasi hebu tuone, vipi tunaweza kumtambua Mtume wa kweli na wa uwongo katika hali kama hii?

Jawabu: hebu tazama mfano kama huu ufuatao;

Je! Akija leo mtu kwako na kusema kuwa yeye ni Polisi na kwamba unatakiwa uandamane naye hadi kituoni, wewe utafanya nini?

Utamwambia atoe kitambulisho cha kudhihirisha kuwa yeye ni Polisi au sivyo?

Kitambulisho cha Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, ni QUR’AN.

Ambayo kama ingelitoka kwa asiyekuwa ALLAH (jina ambalo maana yake kwa lugha za mashariki ya kati, ni MOLA WA ULIMWENGU) ingepatikana ndani yake makosa mengi.

Na kwa sababu Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, hajawahi kwenda shule na alikuwa hajui kusoma wala kuandika, vipi anaweza yeye kutunga kitabu, na hali ya kuwa utunzi wa vitabu ni kazi ya wasomi?

 SEHEMU YA TISA

JE! NI MUHAMMAD ALIYETUNGA QUR’AN?

Qur’an 2:1-4

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo.

1. Alif Lam Mym

2. Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu.

3. Ambao huyaamini yasiyoonekana (maadamu yamesemwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake). Na husimamaisha sala na hutoa katika yale tuliyowapa.

4. Na ambao wanaamini yaliyoteremshwa kwako, na yaliyoteremshwa kabla yako na wanaamini ( kuwa iko ) Akhera.

Kitabu cha Qur’an kinatumika kumuongoza mtu hadi akafaulu kuishi maisha mema Duniani na Akhera (maisha ya baadaye). Kama kinavyotumika kuongoza Familia na hata kabila (Tribe).

Kisha kinatumika pia kuongoza nchi nzima, kwa kuwa kinatumika kama vile katiba.

Na pia kinao uwezo wa kuongoza Dunia yote, ki- jamii, ki- siasa, ki-uchumi, ki-utamaduni, ki-masomo, ki-mahakama, ki-ulinzi, na ni uongozi kwa kila aina ya mahitaji ya mwanadamu.

Kitabu hiki ni kidogo sana kwa umbo lake, lakini (amini au usiamini) ndicho kinachotumiwa (kama vile katiba) na baadhi ya nchi ambazo zimepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kijamii, ki-uchumi, ki-elimu na ki-siasa duniani.

Je! Wewe mwenyewe umeona katiba ya kuongoza nchi inavyohitaji watu wengi (Ma-Profesa) ili kutayarisha, na kila baada ya miaka fulani, inasemekana hiyo katiba inayo makosa, inahitaji katiba mpya. Na hali walioitengeneza wote ni wataalamu waliomaliza muda mwingi kusoma.

Qur’an 2:23-24

23. Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia Mtumwa Wetu ( kuwa hakuteremshiwa na Mwenyezi Mungu ), basi leteni sura moja iliyofanywa na (mtu) aliye mfano wake, na muwaite waungu wenu bighairi (wasiokuwa) Mwenyezi Mungu (wakusaidieni); ikiwa mnasema kweli.

24. Na msipofanya - na hakika hamtafanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri.

  

 SEHEMU YA KUMI

MUUJIZA WA MUHAMMAD.

Je! Si muujiza mtu anayelisha kondoo jangwani, asiyejua kusoma na kuandika, awe na uwezo wa kutunga katiba ya ulimwengu mzima?

katiba ambayo kwa miaka - sasa zaidi ya 1,400 - haijawahi kupatikana na makosa, wala kubadilishwa, wala kupunguka uwezo wake na hali yakuwa ni katiba ambayo mlinzi wake (kutokana na uadui wa binadamu) anakuwa ni ALLAH, hadi siku ya kiama?

Je! Kuna kitabu cha mtaalamu yeyote kimeshawahi kubadilisha fikra za watu ulimwenguni kama kilivyofanya kitabu cha Qur’an?

Biblia, pamoja na hali ya kuwa imeathiri watu wengi Duniani, lakini Je! inazo vitabu vya waandishi wangapi?

Kwa hivyo Qur’an ndio muujiza mkubwa wa Mtume Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam. Na ni muujiza mkubwa kuliko miujiza ya Mitume wote waliotangulia kwa sababu, ni muujiza wa kudumu hadi mwisho wa Dunia.

 SEHEMU YA KUMI NA MOJA

DINI YA MITUME WOTE WA MUNGU NI ISLAM.

Kutokana na walivyofunza Mitume wa Mungu tangu wa mwanzo, yaani kuwapo Mungu mmoja, Mola wa ulimwengu wote, inaeleweka kutokana na mafunzo yao kwamba, Dini ya Adam, ndio pia Dini ya Nuhu, na ndio pia Dini ya Ibrahim na ndio Dini ya Mitume wote, (Amani ya ALLAH iwe juu yao).

Kwa hivyo Dini ya Muhammad, ndiyo pia Dini ya Adam na Hawa na ndiyo pia Dini ya Mitume wote. Kwa sababu hawezi mtu kuwa Muislamu hadi atakapokubali moyoni na kutamka kwa ulimi wake ukweli wa kuwapo Mungu mmoja, na kuamini Mitume wote.

Maana ya Islam ni pale Mtu anapoamua kuamini na kutii Amri zote za Mola wa Ulimwengu, kwa kupenda kwake (mwenyewe) bila kulazimishwa. Kwa hivyo mafunzo ya Muhammad hayapingani na mafunzo ya Mtume yeyote wa Allah, hata mmoja.

Kilichowapelekea viongozi wa Kikristo kumpinga Mtume Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, ndicho hicho hicho kilichowapelekea viongozi wa kiyahudi kumpinga Yesu kristo ( Nabii Isa).

Kila Nabii wa Mungu alipata wapinzani kutoka kwa viongozi wa Watu wa enzi yao. Mahubiri yao yakawa yanakanushwa, na kufanyiwa kejeli, na matusi wametukanwa na baadhi yao wamepigwa na hata kuuawa.

 SEHEMU YA KUMI NA MBILI

SABABU YA KUPOTOKA VIONGOZI.

Haya huwa yanatokana na Laana ya Mungu, wanayoipata viongozi hawa kwa sababu ya kuvunja amri ya Mungu ya kwanza na kutowaamini Mitume.

Kisha wakawa wanayapindua maneno ya Mungu, yakawa sio vile yalivyokuwa wakati wa Mitume. Kwa kuyaongeza, kuyageuza na kupachika maneno wayapendayo wao kisha wakasema, “Haya ndiyo maneno ya Mungu.”

Ikiwa kunapatikana ubishi kuhusu jambo hili, kwa kuwapo anayedai kwamba Biblia yote ni maneno ya Mungu na imetakasika, inafaa atazame mfano ulio wazi baina ya Biblia wanayoitumia Wakatoliki na ile ya Waprotestanti.

Kila mmoja wao hudai kwamba Biblia anayoitumia ndiyo takatifu.

Mkatoliki humlaumu Mprotestanti kwa kusababisha kupunguzwa maneno anayodai kuwa ni ya Mungu katika Biblia. Naye Mprotestanti hujitetea kwa kudai kwamba Biblia ya Mkatoliki inazo vitabu vingi ambavyo sio naneno ya Mungu.

Kwa hivyo ikiwa Biblia zinatofautiana hivyo, zitakuwa vipi zote takatifu?

Je! Ni nani huwa anayaongeza maneno ya Mungu, na ni nani huwa anayapunguza?

Haya mambo ya kujitafutia laana ya Mungu huwa yanawapelekea kusema na kutenda vitendo vilivyokosa muelekeo.

Kwa mfano, utamwelewa vipi Mtu ambaye anakusimulia kisa cha Mtu ambaye (msimuliaji asema) alikuwa ni mrefu kisha aseme pia alikuwa ni mfupi? Au Mtu mweupe lakini kwa hakika ni mweusi?

Muhubiri wa Kikristo huanza mahubiri yake kwa kusema kuwa “Mungu ni Mmoja.”

Kisha pale pale anasema, “lakini hasa ni watatu”. Yaani anaamini Mungu ni mmoja mwanzoni mwa maneno yake, kisha pale pale anakanusha imani hiyo, kwa kusema (pia) anaamini ni watatu.

Kisha anakanusha hata hayo maneno yake kwa kusema, “ Yesu ni mtoto wa Mungu.”

Kisha atakanusha hata hayo kwa kusema, “Yesu ndiye Mungu Pekee”. (Yaani maneno ya ujanja, ya Mtu kigeugeu.)

 SEHEMU YA KUMI NA TATU

SIFA YA YESU.

Unapomuuliza kwa nini anamsifu Mungu kwa sifa ya Binadamu (sifa ya Kuzaa Mtoto), na hali Mitume wa Mungu, tangu hapo zamani, walimsifu Mungu kwa sifa zilizo bora kabisa?

Anasema, “kwa sababu Yesu alizaliwa bila ya Baba.”

Lakini tunapoangalia maumbile ya Adam, kwa mfano, tunaona kuwa ameumbwa bila ya Baba wala Mama.

Na mkewe Hawa ametolewa katika mbavu za Adam. Kwa hivyo anaye Baba, yaani Adam, lakini hana Mama.

Na Yesu kristo anaye Mama lakini hana Baba.

Kwa hivyo muujiza wa kuzaliwa Yesu bila Baba sio mkubwa kuliko wa Adam, wala wa Hawa.

Kwa hivyo ukweli ni kwamba Yesu ni mwana wa Mariam, kwa sababu maneno ya kusema Yesu mtoto wa Mungu, yanayo hatari ya binadamu kuwa anamtusi Mungu, kwa kumsifu kwa sifa ya upungufu, sifa za viumbe wake na hali ya kuwa Mungu ni mkamilifu, ahitaji Mtoto wala chochote. Kwa kuwa anajitosheleza bila mke wala chakula wala hewa.

 SEHEMU YA KUMI NA NNE

 JE! MUNGU ANA WATOTO?

Hebu tujiulize, vipi anafikia mtu kuitwa mtoto wa fulani?

Je! Wewe unaweza kumwita mtu yeyote anayepita “ Mtoto wangu?” La!

Kwa nini?

Kwa sababu mtoto kuwa ni wako, sharti kwanza utimize masharti fulani kadha wa kadha.

Kama vile; uwe umemuowa mama yake, na uyafanye naye yanayofanywa, au sivyo?

Kwa hivyo, ikiwa tunafahamu kwamba aliyeumba Mbingu na Nchi, sifa zake lazima ziwe ni zile bora (mwisho wa ubora), matusi kwa Mola yatapatikana atakapojaribu mwanadamu kusema au kumaanisha (hata kama hakusema) kwamba Mola wa ulimwengu (na Mola atuepushe mbali na maneno kama hayo) kuwa ana Mtoto, kwa sababu ikiwa hukumuowa mama yake, vipi itasemwa kuwa mtoto atakayezaliwa (wewe) ndiye baba yake?

Kwa hivyo Yesu ni mwana wa Mariam, kama inavyosema Qur’an. Na kwamba yeye ni Mtume wa Mungu, aliyezaliwa kwa miujiza ya Mungu bila baba, yaani kama Adam na hawa.

 SEHEMU YA KUMI NA TANO

WAHUBIRI WACHANGANIKIWA.

Hebu angalia wanavyosema (viongozi wa kikristo) wanapohubiri;

Kama ulivyotangulia kuona, Muhubiri anaanza kwa kusema “Mungu ni mmoja.”

 Kisha anaendelea na kusema “lakini ni watatu,” maana yake, anaamini mwanzo wa maneno yake kuwa, Mungu yupo na kwamba ni mmoja.

Kisha pale pale anayakanusha aliyoyasema (mwanzo).

Na hapa ndio anapoanza mtindo wake wa kuwa kigeugeu kwa sababu anasema, “Lakini (kusema ukweli) ni watatu.”

Na anaendelea kuyakanusha hata hayo kwa kusema, “Lakini Yesu ni Mtoto wa Mungu.” Yaani (sasa anamini kuwapo) Mungu wawili na mmoja asiyekuwa kamili bado?

Kisha anaweza hata kuendelea na kusema Yesu ndiye Mungu!

Kama kungekuwa na Mungu zaidi ya mmoja, kila mmoja angetaka mambo yake (yaende) tofauti na (huyo anayedaiwa ni) mwenzake, na ingepatikana hata ugomvi kati yao.

Roho takatifu ni Malaika Jibril (Gabriel). Kwa sababu yeye anayo majina mawili. Jibril au Roho Takatifu.

 SEHEMU YA KUMI NA SITA

SIFA ZA MUNGU.

Kwa hivyo ikiwa Yesu ni Mungu, hebu tuone yale Mitume wote wa Mungu waliyowafahamisha watu wa enzi yao kuhusu alivyo Mungu wa kweli (How the Messengers of God described the Lord of the Universe.)

Kwanza maneno ya Mitume wote yanakubaliana kwamba, Mungu anao uhai wa milele, au sivyo?

Maana yake, hawezi kupatwa na mauti. Je! Mungu anaweza kufa?

Kisha muhubiri anayesema Yesu ni mungu hamalizi mahubiri yake ila atasema,“Yesu alikufa Msalabani.”

Kwa hivyo, maneno yake hayo yatakuwa yanamaanisha (hata kama hakusema) kwamba sifa yake (Yesu) hailingani na sifa ya Mungu. (yaani Yesu anaweza akapatwa na Mauti na Mungu hapati Mauti milele.)

Kwa sababu ikiwa kutakuwa na wakati Mungu alipatwa na mauti, basi sifa ya kuwa anao uhai wa milele itakuwa hakuna. Na hiyo ndiyo sifa mwanadamu huyu anayojaribu kuondoa katika akili za watu ili (watu) wawe na shaka kuhusu uhai wa Mola wao.

Sifa nyengine anayosifika nayo ni kwamba, Mungu halali.

Kwa sababu moja katika sifa zake ambazo ni nzuri sana, ni kwamba anajua kila kitu. Maana yake, yeye siyo sawa na Binadamu.

Kwa sababu ikiwa Mungu atalala, je! Atakuwa bado na sifa ya kuwa anajua kila kitu?

Je! Enyi Wahubiri, Yesu alilala?

Ikiwa mtasema kuwa alilala, basi maana ya maneno hayo ni kuwa Yesu sio Mungu, (hata kama hamkusema hivyo), kwa kuwa alikuwa analala, na hivyo hajui kila kitu, na kutokana na hayo atakuwa hana sifa ya Mungu, kwa sababu Mungu hajawahi kuonja usingizi wala kusinzia.

Zaburi 121:2

2 Msaada wangu u katika

BWANA.

Aliyezifanya mbingu na nchi

4. Naam, Hatasinzia wala Hatalala

Usingizi

 SEHEMU YA KUMI NA SABA

JE! YESU NI MUNGU?

Mungu ana sifa ya kuwa hali chakula. Je! Mungu anakula?

Hebu tuone kwa nini Mungu hali chakula na hali ya kuwa yeye ndiye aliyeumba kila aina ya chakula. Matunda mazuri mazuri, Nafaka, Nyama na Maji.

Na tunapoangalia binadamu anavyokipenda chakula, tunaona vile yeye huwa anapigana kwa sababu ya hiki chakula. Ndugu anamuuwa nduguye kwa sababu ya shamba. (Na hutokea pia) Waziri wa nchi (anashawishika hadi) anaiba Mali ya umma, ili aweze kuwa na Nyumba Ng’ambo, apate huko chakula kizuri. Na jambazi linaiba mobile ili liweze kununua chakula. Je! Mungu anakula?

 Mitume walisema La! Kwa nini? Kwa sababu Mungu anayo sifa ya Utakatifu. Na yeyote anayekula, baada ya masaa machache, lazima ataenda kwa choo - au sivyo?

 Kwa hivyo Mungu, haistahili kumsifu kwa sifa mbaya, kama hii ya kula chakula!

Wahubiri, je! Yesu alikula?

Ikiwa alikuwa anakula, sifa yake ya kula inamaanisha hata chooni alikuwa anaenda. Na hivyo sifa ya utakasifu aliyonayo Mungu, Yesu (ni Mwanadamu) hana.

Hayo pia yanathibitisha kwamba hata yule wanayemwita Baba mtakatifu, ikiwa anakula chakula, utakatifu utapatikana vipi?

 SEHEMU YA KUMI NA NANE

YESU APASHWA TOHARA.

Maandiko yanasimulia kwamba Yesu alitahiriwa. Kwa hivyo wanaposema wahubiri kwamba Yesu alitahiriwa, watakuwa wanamaanisha nani aliyemtahirisha, na ni nani mtahiriwa?

Je! Wahubiri hawa huwa na fikra gani wanaposema Yesu alitahiriwa – kisha waseme Yesu ni Mungu?

Kama Yesu ni Mungu na iwe ndiye ametoa amri ya watu kutahiri, itakuwaje yeye atahirishwe na mwanadamu?

Je! Mungu – Mungu sio cheo anachopewa yeyote tunayemtaka akipate – kwa hivyo nani aliye na ujasiri wa kusema maneno makubwa kama hayo wanayosema wahubiri hawa?

Maandiko yasema Yesu alitahiriwa, Je! Wewe waonaje? Yesu ni Mungu?

Qur’an 4:172

Masihi (Nabii Isa) hataona unyonge kuwa mja (mtumwa) wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika waliokaribishwa (na Mwenyezi Mungu, hawataona unyonge kuwa waja wa Mwenyezi Mungu). Na watakaouona unyonge uja wa Mungu na kutakabari; basi Atawakusanya wote kwake (awatie Motoni).

Isaiya 43:10-11

Ninyi ni mashahidi wangu, Asema BWANA, na mtumishi wangu niliyemchagua; mpate kujua, na kuamini na kufahamu ya kuwa Mimi Ndiye; kabla yangu hakuumbwa mungu awaye yeyote wala baada yangu Mimi hatakuwapo Mwingine 11. Mimi, naam, Mimi, ni BWANA, zaidi yangu Mimi hapana mwokozi.

Kwa hivyo kama tunavyoona, kwa ushahidi wa maneno ya Mungu, Mitume wote na Manabii wa Mungu ni Wanadamu waliochaguliwa kumtumikia Mola wa Ulimwengu. Na Yeye ndiye Amewaita Watumishi au Watumwa wake kama walivyo viumbe wote Watumwa Wake.

 SEHEMU YA KUMI NA TISA

HERODE ATAKA KUMUUA YESU

Mungu ana sifa ya kuwa mwenye Nguvu zote, asiyeshindwa na chochote.

Wahubiri Wakristo wanasema Yesu alipokuwa mdogo, Mfalme alikuwa anawauwa watoto wa kiume hadi Yeye na Mama yake na Yusuf (baba wa kambo) ikawabidi kuhama kwa siri, kwenda Misr, hadi alipokufa Herode.

Kwa hivyo ikiwa wahubiri wanasema Yesu ni Mungu, maneno yao hayo yatakuwa yanamaanisha kwamba Mungu alikuwa anaenda Misri kwa kuogopa Nani? Askari wa Waroma?

Je! Mungu anatoroka kwa khofu? Je! Mungu anayo sifa ya uwoga? Kisha khofu ya kuwaogopa askari wa kiroma?

 SEHEMU YA ISHIRINI

MUHAMMAD NI MTUME WA ALLAH.

Kwa hivyo maneno ya Mtume Muhammad, Swalla Allahu alaihi wa sallam, ndiyo ya kweli kuwa HAKUNA ALIYE NA HAKI YA KUABUDIWA ILLA ALLAH na KWAMBA HAKIKA MUHAMMAD S.A.W. NI MTUME WA ALLAH.

 NA KUWA ISSA MWANA WA MARIAM SIO MWANA WA MUNGU BALI NI MTUME WA ALLAH ( aliyetumwa kwa Wayahudi, ambao walimkataa).

Maneno haya ndiyo (Itiqadi) anayotamka Mtu ili kuingia katika Uisilamu.

Sio kama wanavyoeneza maadui wa hii Dini kwamba, mtu huvunjiliwa nazi kichwani au hufedheheshwa wakati wa kujiunga kwake katika Dini ya Allah.

Hayo ni maneno ya uzushi wanayoyasema, ili kuwavalisha watu hatamu za ki-fikra kwa lengo la kuwatia (walio dhaifu kati yao) khofu au chuki ili kuwazuilia wanaotaka kujiunga au kujisalimisha kwa amri ya Mola wao. Mola Ambaye ndiye mwenye uwezo wote, na ndiye mlinzi asiyeshindwa.

Kwa hivyo ikiwa umeyafahamu hayo yaliyo katika makala haya na ungependa kuwa Muisilamu, nasi tunakunasihi (tunakushauri) usipoteze muda wako, kwa ubishi au uzushi wala upuuzi na watu wale wanaopenda mambo kama hayo.

Na badala yake ufanye haraka kuamini kwamba Mungu yupo, na kwamba Yeye ni Mmoja. Na hakuna Mungu mwengine ila Yeye. Hana Mshirika katika Ufalme Wake, wala hafai kuabudiwa asiyekuwa Yeye.

Na kuamini kwamba Allah Anazo sifa nyingi, zote za ukamilifu na wala hana hata sifa moja ya upungufu kama wanavyomsifu kwa sifa kama hizo baadhi ya Wahubiri kwa lengo la kupotosha Watu kuhusu itiqadi zilizo sahihi ili wafaulu kuchuma mali yao bila kujali kwamba matokeo ya kutenda mambo kama haya, kwa wote wanaopotoka na kupotasha ukweli wa maneno ya Allah, ni kuingia katika Moto wa Jahannam.

Kisha uamini na Mitume wa Mungu wote bila kuwabagua, kama walivyofanya (Wayahudi) kumhusu (Yesu) Nabii Issa. Na kama walivyofanya (Wakristo) kumhusu Mtume wa Mwisho, Muhammad, (Swalla Allahu alayhi wa Sallam).

Na mwisho tunakupasha habari njema (mapema), kwamba unakaribishwa, kwa moyo mkunjufu, na sisi ndugu zako katika IMAAN.

ASSALAAMU ALAYKUM WA RAHAMATULLAHI WA BARAKAATUH.

Risala hii imekamilika

Tarehe 27/3/2007 yaani 8/3/1428 H,

kwa Uwezo wa Allah, Sub-hanahu wa Taala. Naye Ndiye anayestahiki shukrani zote.

Mwandishi: SALEH M. KYAMBO

email : risala fupi @ tala.yahoo.com

Mobile : +254727 253 993

Or +966594370352