×
Tafsiri hii ya Qur’an Takatifu ambayo ni maarufu kwa jina la Tafsiri ya Ibn Kathir iliandikwa na AI-Hafidh Abu AI-Fida ‘Imad Ad-Din Ismail bin Umar bin Kathir AI-Quraishi Al-Busrawi (Aliyekufa Mwaka 744 H) ni tafsiri maarufu sana kati ya Tafsiri za Qur’an katika lugha ya Kiarabu, na Waislam wengi wanaiona kuwa ni yenye marejeo mazuri kwa mujibu wa Qur’an na Sunnah. Kazi hii ya .Kiarabu ina kurasa elfu tatu na mia mbili katika juzuu nne Darussalam ya Saudi Arabia walichagua jopo la Wanazuoni wa Kiislam kuandika muhtasari wa Tafsiri Ibn Kathir katika lugha ya asili ya Kiarabu. Sheikh Abu AI-Ashbal Ahmad Shaqif wa Rabitah AI-Alam AI-Islami, Makka, na Sheikh Safiur-Rahman Al-Mubarakfuri, Mkuu wa kamati ya Utafiti ya Darussalam waIifanya kazi na kikundi cha wanazuoni kwa takriban Miaka minne kufanikisha azma hiyo. Na Darussalam wakaja na toleo lililofupishwa katika lugha ya Kiarabu, kwa jina la Al-Misbah AI-Munir Fi- Tahdhib Tafsir Ibn Kathir. Tafsiri hii ya Kiswahili ni ya Kitabu hiki cha Kiarabu Al-Misbah AI-Munir Fi- Tahdhib Tafsir Ibn Kathir. .Fikra hii ilianza Mwaka 2005 na kutumia Miaka 17 takriban mpaka kukamilika Tarjama hii ni juhudi kubwa iliyoshirikisha Masheikh na wataalamu wetu wa fani mbalimbali za Dini ya Kiislamu na lugha zote husika. Katika kipindi cha miaka 17, Mradi huu wa Tarjama hii umepitia awamu mbalimbali, tutajitahidi kuzielezea hapa zile awamu muhimu tu na pia tutajitahidi kuwataja baadhi ya walioshiriki katika ,juhudi hii kwa njia moja au nyingine 1. Tarjama hii ya Kiswahili imehaririwa kwa kupitiwa mara tano na Ustadh Yassir Salim Awadh Masoud, Msimamizi Mkuu wa Mradi huu. 2. Tarjama hii ya Kiswahili kwa kulinganisha na Kiarabu imepitiwa mara moja kwa ukamilifu na mara ya pili kwa kupitia maeneo mengi kwa lengo la kuiboresha na kuifanyia uhakiki na Sheikh Seif Abubakar Ruga. 3. Katika kuipitia rasimu ya pili iliyohakikiwa, kwa lengo la kuiboresha na kuihakiki zaidi, ilibidi tuwashirikishe Wataalamu wetu wengine zaidi wa Dini ya Kiislamu. Kwa sababu tafsiri ina kurasa zaidi ya elfu saba (7000), si rahisi kazi hii ikafanywa na mtu mmoja wa enzi hizi, hivyo basi tukazigawanya sura na juzuu kwa kuwapa Masheikh kuzipitia na kuzihakiki kwa kulinganisha na Tarjama asili ya Kiarabu. Hivyo basi, baadhi ya Sura na juzuu zilipitiwa na Masheikh wafuatao, Al Marhum Sheikh Suleyman Amran Kilemile, Sheikh Muharram Juma Doga, Sheikh Seif Abubakar Ruga, Sheikh Khatib Mussa Giragiza, Sheikh Mohamed Ali Kibabu, Sheikh Ali Asaa, Sheikh Khamisi Liyenike, na Sheikh Said Bawazir. Na wengine wengi unaweza kurejea juzuu ya kwanza ya tafsiri hii.