WALIVYO OMBA MASWAHABA ILI WAKUBALIWE SWAUM YA MWEZI WA RAMADHANI
Jamii ya vilivyomo
Full Description
بسم الله الرحمن الرحيم
WALIVYOOMBA MASWAHABA ILI WAKUBALIWE SWAUM YA MWEZI WA RAMADHANI
Imeandikwa na: Imaam Swaalih Bin Fawzaan Al-Fawzaan
Imetafsiriwa na: Idara ya Wanachuoni.com
Imepitiwa na: Yunus Kanuni Ngenda
Salaf-us-Swaalih (Rahimahumu Allaah) walikuwa wakimuomba Allaah miezi sita Awafikishe katika Ramadhaan, kisha wanamuomba tena kwa miezi sita Awakubalie Swawm ya Ramadhaan. Walikuwa wakitilia umuhimu wa matendo kukubaliwa zaidi kuliko utekelezaji. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema:
إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ
“Hakika Allaah Anatakabalia wenye uchaji Allaah”. (05:27)
Allaah Anakubali kutoka kwa wachaji Allaah ambao wanamcha Allaah, wanamukhofu, wanamuogopa na wanamuabudu ukweli wa kumuabudu. Wameitwa ´wachaji Allaah` kwa kuwa wamechukua kinga inayowakinga na adhabu na khasira za Allaah kwa kumtii, kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.
Salaf (Rahimahumu Allaah) walikuwa wakiogopa matendo yao kurudishwa kwa sababu ya upungufu wake, ima kwa sababu ya kutotakasa nia kwa kuingiliwa ndani yake na Riyaa au Sum´aa. Hii ni khatari kubwa ambayo inayoweza kumsibu mwanaadamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Hakika ya kila ´amali inalipwa kwa nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”
Nia ndio msingi wa ´amali. Inaweza kuingiwa ndani yake na kitu katika Riyaa au Sum´aa au ´amali inayofanyiwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jalla) na hivyo ´amali hiyo iwe ni yenye kurudishwa kwa mwenye nayo. Kuna khatari vilevile ´amali ikawa sio yenye kuafikiana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hivyo ikawa ni yenye kurudishwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenye kufanya ´amali isiyokuwa humo Amri yetu itarudishwa.”
Vilevile wanaogopa kuwa wamewadhulumu watu na hivyo matendo yao wakapewa wale waliowadhulumu. Inawezekana wakawa wamemdhulumu mtu katika mali yake au heshima yake au wamemfanyia uadui. Katika hali hii siku ya Qiyaamah yule mdhulumiwaji atapewa matendo mazuri ya yule mdhulumaji. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Yule aliyemdhulumu ndugu yake basi amrudishie haki yake leo kabla [ya Siku] ambapo hakutokuwa dinari wala dirhamu. Ikiwa alifanya matendo mazuri yatachukuliwa na apewe yule aliyemdhulumu na ikiwa hana matendo mazuri yatachukuliwa madhambi ya yule rafiki yake na apewe yeye.” (al-Bukhaariy (2317)
Imesimuliwa katika Hadiyth ya kwamba kuna watu watakuja siku ya Qiyaamaha na matendo mfano wa jibali katika Swalah, Swadaqah na Swawm, lakini amemdhulumu huyu, amempiga huyu na amechukua mali ya huyu. Wote hawa watachukua sehemu ya matendo yake mazuri. Yakiisha kabla ya kuhukumiwa yatachukuliwa madhambi yao na kuongezewa. Baada ya hapo atupwe Motoni. Hii ni khatari kubwa. Kwa ajili hiyo ndio maana Salaf walikuwa wakitilia umuhimu mkubwa katika ´ibaadah na hata hivyo wakiogopa isije kukubaliwa.