×
Kitabu hiki kinazunguzia kufichua (kuyaweka wazi) mambo yenye utata

 Kufichua Yenye Utata

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab

Mfasiri:

Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush

 Imepitiwa Na:

Abu Bilaal ´Uthmaan Nu´umaan

 Utangulizi wa mpitiaji

Bismillaah. Shukran zote zastahiki kuregea Kwake Yeye (سبحانه وتعالى) Muumba mbingu na ardhi na vilivyomomo ndani yake. Ni Yeye peke Yake Anastahiki kuabudiwa kwa haki na kutoshirikishwa na kitu chochote katika ´Ibaadah Zake, Asiyekuwa na mfano ambaye Hafananishwi na kitu chochote.

Na Swalah na salaam zimfikie Mtume Muhammad (صلى الله عليه وسلم) alosimama kuitangaza Tawhiyd tokea kutumilizwa kwake mpaka pumzi zake za mwisho za maisha yake, akafikisha ujumbe wa Mola Wake Aloamrishwa na Maswahabah wake na kila wenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah. Amma ba´ad:

Hakika Tawhiyd ndio msingi wa Uislamu uliyojengwa juu yake. Na hapana shaka ni jambo muhimu kwa kila Muislamu kuijua na kuitekeleza kwa kuwa haitokubaliwa ´Ibaadah ya Muislamu yoyote bila ya Tawhiyd na wala hazitokubaliwa ´amali ya Muislamu ikiwa haitokuwa ya kumpwekesha Allaah wala kwenda kwa kulingana na mafundisho ya Mtume Muhammad (صلى الله عليه وسلم) na wala hatopata Shafaa´ah (uombezi) wa Mtume Muhammad ila yule aliyekuwa katika msimamo wa Tawhiyd. Na katoa ahadi Mtume kuwa yoyote atakayekuwa neno lake la mwisho katika ulimwengu huu ni Kalimat at-Tawhiyd “laa ilaaha illa Allaah” ataingia Peponi. Twamuomba Allaah Atukhatimishe juu ya msimamo wa Tawhiyd.

Hakika umuhimu wa Tawhiyd ni mkubwa na ndio lengo kubwa walilotumilizwa nalo Mitume likawafanya Maswahabah wasafiri miji mbali mbali kwa ajili ya kufikisha Ujumbe huu wa Tawhiyd kwa watu mbali na mitihani mbali mbali iliyowapata, mpaka wakaja wanavyuoni ambao wamesimama kuitetea na kuifikisha. Mmoja wao akiwa ni Mujaddid wa karne, yeye ni Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Allaah Amrehemu) ambaye tarehe yake yajulikana na alivyoisafisha bara Arabu na ushirikina pamoja na vita alivyopigwa mpaka akaweza kufaulu. Na moja ya kazi aliyoifanya mbali na kulingania watu katika Tawhiyd, aliandika vitabu mbali mbali vya Tawhiyd vilivyopendwa na watu. Moja wapo ni Kitabu hiki cha Kashf-ush-Shubuhaat. Kitabu ambacho amefichukua na kuweka wazi shubuha (utata) wa washirikina walokuwa wakizitumia kuutetea ushirikina wao zama hizo. Kitabu ambacho kimeshereheshwa na kufafanuliwa na wanavyuoni mbali mbali.

Na leo tumshukuru kijana wetu mpendwa al-Akh Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush as-Salafiy Allaah amuhifadhi na kumuongoza yeye na sisi sote katika njia hii iliyonyooka kwa kazi nzuri aloifanya kukitafsiri kitabu hiki kwa lugha ya kiswahili, ili wanufaike ndugu zake Waislamu na elimu kama hii. Na twamuomba Allaah Ampe siha na afya azidi kufasiri vitabu vingine vya Tawhiyd ili Ummah uzidi kuijua Tawhiyd na aijaalie ´amali hii katika mizani ya ´amali yake siku ya Qiyaamah, amghufurie madhambi yake yeye na wazee wake na jamii ya Waislamu.

Wa Swalah Allaahu ´alaa Nabiyyinna Muhammad, wa ´alaa aalihi wa Aswhaabihi wa sallam.

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ ، أَشْهَدُ أَنْ لا إِلهَ إِلَّا أَنْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتْوبُ إِلَيْكَ

Imeandikwa na:

Abu Bilaal ´Uthmaan Nu´umaan

Jumada al-Awwal 6, 1434/18-04-2013

 Historia Fupi Ya Imaam Muhammad bin 'Abdil-Wahhaab

Asili yake

Jina lake ni Abul-Husayn Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab bin Sulyamaan bin ‘Aliy Musharrif Al-Wuhaybiy. Kabila lake ni Bani Tamiym. Amezaliwa mwaka 1115 H (1704 M) katika mji ya ‘Uyaynah kijiji cha Yamaamah ndani ya Najd, kaskazini Magharibi ya mji wa Riyadhw, Saudi Arabia. Ametoka katika familia ya Wanavyuoni kwani baba yake ‘Abdul-Wahhaab alikuwa ni Mwanachuoni maarufu wa Najd na Qaadhiy wa mji huo.

Elimu Yake

Alijifunza kusoma Qur-aan alipokuwa na umri mdogo na akaihifadhi akiwa chini ya umri wa miaka kumi. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Alimjaalia kuwa na uhodari na akili nzuri, wepesi wa kufahamu na kumaizi jambo au somo. Alipendezewa mno kusoma kazi za Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibnul-Qayyim (رحمهما الله).

Alifanya bidii kwenye masomo yake na kuendelea kujifunza chini ya usimamizi wa baba yake. Akajifunza elimu ya Dini chini ya Wanavyuoni walioko mjini mwake wakiwemo baba yake na ‘ami yake. Alisafiri kutoka kwenda Madiynah kusoma chini ya Wanavyuoni wakubwa wa huko wakiwemo; Shaykh ‘Abdullaah bin Ibraahiym bin Ash-Shamariyyi, na Mwanachuoni maarufu wa India Shaykh Muhammad Hayaat Al-Sindi.Alikwenda Makkah pia na alitekeleza Hajj. Hatimaye akaelekea Baswrah (Kaskazini Iraq) kutafuta elimu zaidi akasoma chini ya Wanavyuoni wa huko akawa maarufu kwa mijadala baina yake na Wanavyuoni.

Harakaat Na Mitihani

Watu wa Najd walikuwa katika shirki na bid’ah (uzushi). Walikuwa wakiabudu miungu mingi na kuabudu makaburi, miti, mawe, mapango, majini na mashaytwaan, waja wema waliojulikana kama ni mawalii. Uchawi na unajimu (utabiri wa nyota) ulisambaa pia. Hakuna aliyekataza ‘Ibaadah potofu hizo kwani watu walikuwa katika kuchuma manufaa na starehe za dunia zaidi na wakakhofia kuyapoteza hayo. Hivyo Shaykh akaona umuhimu mkubwa uliohitajika kuwarudisha watu katika msimamo wa Qur-aan na Sunnah. Akaanza kuwalingania watu katika Tawhiyd - kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kumshirikisha na lolote katika ‘Ibaadah. Akaazimia kujitumikisha peke yake kwa uvumilivu katika konde. Akajua hakuna lolote kitachofaulu kufanyika ila Jihaad katika Njia ya Allaah.

 Shaykh alikumbana na mitihani, misukosuko, na vitisho, lakini alikuwa ameshategemea hali hiyo kumfikia na alikuwa tayari kukabaliana nayo kwani alitambua kuwa hilo ni jambo lisiloepukika kwa kila mlinganiaji kwani ndio hali waliyokutana nayo Mitume wote, na Salafus-Swaalih (waja wema waliotangulia).

 Miongoni mwa mitihani aliyokumbana nayo ni kutokana na Wanavyuoni wadhaifu wasiokuwa na hoja ambao walimpinga na kumfanya akabiliane na misukosuko, vitisho na kukasirikiwa. Pia alikabiliana na misukosuko na mateso chini ya mikono ya madhalimu wa Huraymilaa. Na alipowashawishi watawala kuwahukumu wadhalimu kwa Shari’ah ya Kiislamu, ilisababisha baadhi ya watu kuyaweka maisha yake hatiani lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alimnusuru.

 Aliamua kurudi kwao ‘Uyaynah, ambako kipindi hicho kulikuwa chini ya utawala wa mtoto wa Mfalme ‘Uthmaan bin Muhammad bin Mu’ammar, ambaye alimpokea Shaykh kwa ukarimu na kumuahidi kumuunga mkono na kumsaidia kuwaita watu katika Uislam. Akaendelea kufundisha na kutoa da’wah hatimaye akashawishika kidhati na kwa vitendo kuondoa dini ya miungu mingi pale alipoona baadhi ya watu ni wagumu kurudi katika Uislamu. Aliweza kumshawishi gavana wa mji huo kulivunja zege lililojengewa juu ya kaburi la Zayd bin Al-Khattwaab ambaye alikuwa ni kaka wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنهما). Akavunjavunja mangome mengineyo, mapango, miti n.k. Akaamrisha Shari’ah ya Kiislamu itekelezwe kama kumpiga mawe hadi afe mwanamke aliyekiri kuwa amefanya zinaa. Shaykh aliendelea na harakati zake za vitendo na kauli ambazo zilimfanya azidi kuwa maarufu. Hatimaye akawa jaji (Qaadhiy) wa mji wa ‘Uyaynah. Lakini hakuweza kuendelea hapo kwani Mfalme alishawishiwa na viongozi wa miji ya jirani amuue Shaykh kwa vile hawakupendezewa na da’wah yake. Ikabidi afukuzwe katika mji huo.

Akakaribishwa mji wa ad-Dir’iyyah ambao ulikuwa ni jirani yake. Huko akakaribishwa ingawa kwanza alitiliwa shaka. Alifikia kwa mja mwema aliyempokea ila alimkhofia kutokukubaliwa na mtoto wa Mfalme Muhammad bin Sa’uud. Habari zikamfikia kwanza mke wa Ibn Sa’uud ambaye alikuwa mkarimu na mwenye taqwa. Akamfahamisha mumewe kwa kumwambia, “Hii ni bahati kubwa umeletewa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) mtu ambaye anawaita watu katika Uislamu, anawaita katika Qur-aan na Sunnah za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Bahati iliyoje? Mkimbilie haraka na umuunge mkono wala usimpinge au kumkataza kwa hayo”. Muhammad Ibn Sa’uud akakubali ushauri wa mkewe na akaenda kwa Shaykh na akafanya mkataba naye kwamba asiondoke nchini hapo. Ndipo Shaykh akaweka makazi yake hapo na kuendelea na da’wah. Aakaendelea na harakati za da’awah hapo Dar’iyyah. Akaheshimika na kupendwa mno na akaungwa mkono na watu. Da’wah yake iliwaathiri na kuwapendezea mno watu. Ikaenea katika nchi za Kiislamu na nyinginezo. Wakimiminika watu na Wanavyuoni kufika hapo Dar’iyyah kujifunza kwake.

 Kama ijulikanavyo kila jema halikosi mitihani. Wakatokeza wapinzani na waliokuwa na chuki naye. Kulikuweko waliompinga da’wah yake ya kuondosha shirki na bid’ah na kuwaita watu katika Tawhiyd. Na wengineo waliompinga kabisa ni kwa sababu ya kuhofu kufukuzwa katika nafasi au vyeo vyao vya kazi. Kwa hiyo wengine walimpinga kwa ajili ya Dini, na wengine walimpinga kisiasa. Wapinzani wake walimzushia ya kumzushia walifika hadi kudai kwamba Shaykh alikuwa ni mfuasi wa Khawaarij. Na mara nyingine wakimlaumu bure bila ya dalili na nje ya upeo wa elimu zao. Hivyo yakaweko malumbano na majibishano yaliyoendelea katika mijadala kadhaa. Shaykh aliwaandikia kuwajibu madai yao, na wao walimrudishia majibu na yeye akawa akiwathibitishia ufahamu wao mbya wa shari’ah na Dini kwa ujumla kwa dalili. Ndipo wingi wa maswali na majibu yakawajumuisha watu na wakazidi kuongezeka. Baadhi ya mijadala hiyo iliandikwa na kuchapishwa katika vitabu.

Athari Ya D’awah Yake

Da’wah yake ya takriban miaka 50 imedhihirika na kuleta athari kubwa kwanza kwa Waislamu wa zama hizo. Watu waliacha kuabudu makaburi, miti, mawe, majini, waliacha utabiri wa nyota na kila aina ya shirki. Imewatoa pia watu katika ujinga wa kufuata mila za mababu bila ya dalili. Maamrisho ya mema na makatazo ya maovu yakalinganiwa katika Misikiti. Na hapo msimamo wa Qur-aan na Sunnah ukahuishwa na shirki na bid’ah zikapotoka. Amani na utulivu ukawafunika watu kila mahali. Na mpaka sasa da’wah yake imekuwa na umuhimu mkubwa katika jamii ya Kiislamu. Vijana khasa kutoka nchi za Magharibi na zaidi wale wanaosilimu wamekuwa na hamasa na shauku kubwa ya kujifunza Dini iliyo sahihi na si ile iliyochanganywa na shirki na bid’ah. Kwa hiyo, mafundisho ya msimamo wake wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah ambao pia ndio mwendo wa Safafus-Swaalih yamekuwa kiupamble katika lengo la kutafuta elimu kwa Waislamu watakao na wapendao haki.

Kazi Zake

Ameandika vitabu vingi vya mafunzo mbali mbali lakini alitilia mkazo zaidi katika somo la Tawhiyd na ‘Aqiydah. Na alitumia hikma ya kuandika vitabu vidogo vidogo lakini vilivyokusanya nukta muhimu kabisa. Vilikuwa ni mukhtasari wa maudhui aliyotaka kuidhihirisha. Na vitabu hivyo vimekuja kufafanuliwa kwa kushereheshwa na Ma’ulamaa kadhaa na vimekuwa vina umuhimu mno katika vyuo vya Kiislamu vinavyofuata mwendo wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah.

 Vifuatavyo ni baadhi ya vitabu vyake maarufu. Vinne vya mwanzo ni ambavyo mashuhuri zaidi kwa umuhimu wa maudhui zake. Na vinginevyo vimekusanywa na kujumishwa katika ‘Maj’muu’at Mu-allafaatil-Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.

1. Kitaabut-Tawhiyd - kitabu hiki kimekuwa mashuhuri mno na kimeenea sana na somo lake limekuwa ni lenye kutoa mafunzo muhimu kuhusu kumpwekesha Allaah na kuepukana na shirki.

2. Al-Uswuul Ath-Thalaathah – kitabu kitoacho mafunzo kuhusu asili au misingi ya Uislamu.

3. Al-Qawaaid Al-Arba’h - kinatoa mafunzo ya kanuni za ufahamu wa shirki kwa ujumla.

4. Kashf Ash-Shubuhaat - kinakanusha hoja zinazojulikana na watetezi wa shirki na bid’ah.

5. Mukhtaswar Al-Inswaaf was-Sharh Al-Kabiyr

6. Mukhtaswar Zaad Al-Ma’aad

7. Mukhtaswar As-Siyrah

8. Mukhtaswar al-Fat-h

9. Masaail Al-Jaahiliyyah

10. Adaab Al-Mashiy ilaa as-Swalaah

Wanafunzi Wake

Alikuwa na wanafunzi wengi mno. Miongoni mwao ni watoto na wajukuu wake ambao waliendeleza kazi yake ya da’wah na Jihaad katika njia ya Allaah, walifungua vyuo karibu na kwao wakifunza watu masomo ya Dini. Kati ya watoto wake ni Husayn, ‘Aliy, ‘Abdullaah na Ibraahiym. Na kati ya wajukuu wake ni ‘Aliy bin Husayn, na pia ‘Abdur-Rahmaan bin Hasan aliyeandika kitabu cha ‘Fat-h Al-Majiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd. Wanafunzi wake wengineo ni ‘Abdul-‘Aziyz bin Muhammad bin Sa’uud, Hamad bin Naaswir bin Mau’ammar na ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Husayn.

Familia Yake

Alikuwa na watoto sita; Husayn, ‘Abdullaah, Hasan, ‘Aliy, Ibraahiym, ‘Abdul-‘Aziyz. Shaykh anatokana na kizazi kinachojulikana kwa ‘Aal-Shaykh’ ambacho kimetoa Wanavyuoni kadhaa akiwemo Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal-Shaykh aliyekuwa Mufti mkuu wa awali Saudi Arabia na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Aal-Shaykh ambaye ni Mufti mkuu wa sasa.

Kifo Chake

Alifariki mwaka 1206 H (1792 M) akiwa na umri wa miaka 91. Rehma za Allaah ziwe juu yake na Allaah Amruzuku Pepo ya Firdaws. Aamiyn.[1]

 Mlango Wa 1

 Lengo la kutumwa Mitume (´alayhimus-Salaam)

Jua – Allaah Akurehemu – ya kwamba (maana ya at-Tawhiyd) ni kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa ´Ibaadah. Na ndio Dini ya Mitume ambao Aliwatuma Mitume kwa Dini hiyo kwa waja Wake, na wa kwanza wao ni Nuuh (´alayhis-Salaam). Allaah Alimtuma kwa watu wake walipopetuka mipaka (kwa kuwaabudu) watu wema; Wadd, Suwaa´, Yaghuuth, Ya´uuqa na Nasra.

Na Mtume wa mwisho ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na yeye ndiye alivunja picha za watu hawa wema. Allaah Alimtuma kwa watu ambao wanaabudu, wanahiji, wanatoa Swadaqah na wanamdhukuru Allaah kwa wingi, lakini waliwafanya baadhi ya viumbe kuwa waasitwah wakati na kati baina yao (wao) na baina ya Allaah (Ta´ala). Wanasema: “Tunataka kutoka kwao sisi kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) na tunataka shafaa´ah uombezi wao Kwake (Allaah); kama mfano wa Malaika, ´Iysa, Maryam na wengineo katika watu wema.

Allaah (Ta´ala) Akawatumia Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awajadidie Dini yao, ambayo ni Dini ya baba yao (´alayhis-Salaam), na kuwaambia ya kwamba kujikurubisha huku na Itikadi hii ni haki ya Allaah peke Yake, haisihi kufanyiwa katika hayo (´Ibaadah hiyo) mwengine yeyote, si kwa Malaika Aliyekaribu, wala Mtume aliyetumwa tusiseme wasiokuwa hao (wawili). Vinginevyo, watu hawa washirikina wanashuhudia ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji Pekee asiyekuwa na mshirika, na kwamba hakuna anayeruzuku isipokuwa Yeye, na hakuna anayehuisha wala kufisha isipokuwa Yeye, na wala hakuna anayeendesha mambo isipokuwa Yeye. Na kwamba mbingu zote saba na vilivyomo ndani yake, na ardhi saba na vilivyomo ndani yake, vyote hivyo (walikuwa wanaamini kwamba) ni viumbe Vyake na viko chini ya uendeshaji na Uwezo Wake (Allaah).

 Mlango Wa 2

 Dalili ya kwamba washirikina ambao Mtume (´alayhis-Salaam) aliwapiga vita walikuwa wanakiri Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah

Ukitaka dalili ya kwamba watu hawa ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipigana nao vita walikuwa wanashuhudia hili (Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah), soma Kauli ya Allaah (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa (aliye) hai kutoka kwa aliyekufa, na anayemtoa aliyekufa kutoka (aliye) uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)? Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi wenye kumuogopa Yeye?” (Yuunus 10 : 31)

“Na kauli Yake Allaah (Ta´ala):

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

”Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo humo, mkiwa mnaelewa?” Watasema: “Ni ya Allaah Pekee” Sema: “Je, basi vipi mnadanganywa?” (al-Muuminun 23 : 84)

قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

”Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu, Naye Ndiye Alindaye, na wala hakilindwi chochote dhidi Yake, ikiwa mnaelewa?” Watasema: “Ni Allaah Pekee” Sema: “Basi vipi mnazugwa (akili zenu)?”(al-Muuminuun 23 : 86-87)

Ukishahakikisha ya kwamba (washirikina) walikuwa (wanakiri) wanakubali hili, na hili halikuwaingiza katika Tawhiyd ambayo aliwalingania kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na ukajua ya kwamba Tawhiyd waliyoipinga ni Tawhiyd al-´Ibaadah ambayo washirikina katika zama zetu wanaiita “al-I´itiqaad”.

Na walikuwa wakimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Usiku na mchana. Halafu katika wao kulikuwa wanaowaomba Malaika kwa ajili ya wema wao na ukaribu wao kwa Allaah (Ta´ala) ili (Malaika hao) wawaombee, au wanaomba mtu mwema; kama mfano wa Laat, au Mtume kama mfano wa ´Iysa.

Na umejua ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kapigana nao vita kwa Shirki hii na akawaita (lingania) kumtakasia ´Ibaadah Allaah Mmoja. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba Misikiti ni (kwa ajili) ya Allaah, basi msiombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

Na Kasema Allaah (Ta´ala):

لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ

“Kwake Anayo maombi ya haki. Na wale wanaoomba pasi Naye (masanamu, walioko kaburini, mizimu n.k.) hawawaitikii kwa chochote.” (Ra´d 13 : 14)

Na umehakikisha ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kawapiga vita ili Du´aa (Maombi) yote yawe kwa Allaah, kuchinja kote kuwe kwa Allaah, uwekaji wa nadhiri wote uwe kwa Allaah, kuchinja kote kuwe kwa Allaah, al-Istighaathah kuomba msaada, yote afanyiwe Allaah na jumla ya ´Ibaadah zote afanyiwe Allaah.

Na umejua kuwa kukubali kwao Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah hakukuwaingiza katika Uislamu. Na kwamba makusudio yao kwa Malaika, au Mitume, au mawalii walikuwa wanataka shafaa´ah maombezi yao na kujikurubisha kwa Allaah kwa hilo, Yeye (Allaah) ndiye Ambaye Kahalalisha damu yao na Dini na mali yao. Hivyo utakuwa umejua Tawhiyd waliyoilingania kwayo Mitume na wakakataa kuikubali washirikina.

 Mlango Wa 3

 Tawhiyd al-´Ibaadah ndio maana ya “Laa ilaaha illa Allaah”

Na Tawhiyd hii, ndio maana ya kauli (neno) lako: “Laa ilaaha illa Allaah.” Kwa hakika mungu kwao ni yule ambaye anakusudiwa kwa ajili ya mambo haya; sawa ikiwa ni Malaika, Mtume, walii, mti, kaburi au jini. Hawataki (hawamaanishi ya) kwamba Allaah ilaahah ni yule mwenye kuumba, mwenye kuruzuku na mwenye kuendesha mambo. Kwa hakika wao wanajua ya kwamba (Mwenye uwezo wa) hayo ni ya Allaah Mmoja, kama tulivyotangulia kusema. Isipokuwa wanachomaanisha kwa (kusema) Ilaah mungu, ni kile wanachomaanisha washirikina wa zama zetu kwa lafdhi (kusema) kwao Sayyid (Bwana). Akawajia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalingania katika kalimaat at-Tawhiyd, nayo ni Laa ilaaha illa Allaah. Na makusudio ya maneno haya ni maana yake na sio kuyatamka peke yake.

Makafiri wajinga walijua makusudio ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) kwa neno hili ni kumpwekesha Allaah (Ta´ala) kwa ´Ibaadah na kupinga kwa vinavyoabudiwa badala Yake na kujiweka navyo mbali kabisa, kwa hakika wakati walipoambiwa semeni laa ilaaha illa Allaah hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya miungu (wote) kuwa ni Ilaah (Mungu) Mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (Swaad 38 : 05)

Ukishajua ya kwamba makafiri wajinga walijua hilo, ni jambo la kushangaza ni kwa yue anayedai Uislamu na yeye hajui maana ya neno hili jambo ambalo walikuwa wanalijua makafiri. Badala yake anafikiria ya kwamba maana yake ni kutamka herufi zake bila ya kuiamini (kuitakidi) moyoni kwa kitu katika maana yake. Mjuzi katika wao anafikiria ya kwamba maana yake ni kwamba hakuna Mwenye kuumba, wala Mwenye kuruzuku, wala Mwenye kuendesha mambo isipokuwa Allaah. Hakuna kheri kwa mtu ikiwa wajinga makafiri wanajua zaidi yake maana ya Laa ilaaha illaa Allaah.

 Mlango Wa 4

 Neema ya Allaah kwa waja Wake juu ya Tawhiyd

Ukishajua (elewa) niliyokwambia na moyo wako umekinaika na ukajua kumshirikisha Allaah ambako Allaah Amekuzungumzia kwa kusema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah Hasamehi kushirikishwa na kitu chochote; na Husamehe isiyokuwa Shirki kwa Amtakae.” (an-Nisaa 04 : 48)

na ukajua Dini ya Allaah ambayo amewatuma kwa ajili yake Mitume, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, ni Dini ya kipekee ambayo Allaah Anaikubali kutoka kwa mtu, na ukajua jambo ambalo limekuwa halijulikani kwa watu wengi kutokana na hili, utapata faida mbili:

1. Faida ya kwanza: Ni kufurahi kwa fadhila za Allaah na kwa Rahmah Zake. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

”Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Kwa Fadhila za Allaah na kwa Rahmah Yake (Qur-aan, Uislamu, Iymaan), basi kwa hayo wafurahi.” Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya (mali na starehe za dunia).‏(Yuunus 10 : 58)

2. Faida ya pili: Umefaidika pia (kuwa na) khofu kubwa. Ukijua ya kwamba mtu anaweza kukufuru kwa neno analolitoa kwenye mdomo wake, na pengine amelisema na yeye ni mjinga (hajui) – lakini hapewi udhuru kwa ujinga. Na huenda amelisema huku akidhania ya kwamba yanamkurubisha kwa Allaah kama walivyodhania washirikina. Na khaswa Allaah Akikuongoza kwa yale Aliyoelezea kuhusu watu wa Muusa (´alayhis-Salaam) – pamoja na wema wao na elimu yao – walipomuendea na kumwambia:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi ilaaha (mungu) kama walivokwa (hawa) wana miungu.” (al-A´araaf 07: 138)

Hapo ndipo khofu na bidii yako itaongezeka na yatakayokuokoa kutokana na haya mfano wake.

 Mlango Wa 5

 Maadui wa Mitume (´alayhimus-Salaam) na Mawalii wa Allaah

Na jua kwamba Allaah (Subhaanah) kwa Hekima Yake Hakutuma Mtume kwa Tawhiyd hii isipokuwa Alimuwekea maadui. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا

”Na hivyo ndivyo Tulivyojaalia kwa kila Nabii (anao) maadui; (nao ni) shayaatwiyn katika watu na (shayaatwiyn katika) majini wakidokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba na ya udanganyifu.” (al-An´aam 06 : 112)

Na yawezekana maadui wa Tawhiyd wakawa na elimu kubwa, vitabu na hoja. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ

”Basi ilipowajia Mitume yao kwa hoja bayana, walifurahia (na kujivunia) kwa yale waliyokuwa nayo katika elimu.” (Ghaafir 40 : 83)

 Mlango Wa 6

 Wajibu wa kutafuta elimu

Ukishajua hilo, na ukajua ya kwamba ni lazima wawepo maadui ambao wamekaa katika njia ya Allaah (Ta´ala), ni watu wenye ufasaha, elimu na hoja. Basi hivyo ni wajibu kwako kujifunza Dini ya Allaah kile ambacho itakuwa ni silaha yako upigane vita na Mashaytwaan hawa ambao kasema kiongozi wao kumwambia Mola Wako (´Azza wa Jalla):

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

(Ibliys) akasema: “Basi kwa kuwa Umenihukumu kupotoka, nitawakalia (waja Wako) katika Swiratwakal-Mustaqiym (Njia Yako iliyonyooka.”). Kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao, na wala Hutopata wengi wao wenye kushukuru.” (al-A´araaf 07 : 16-17)

Lakini ukimuelekea Allaah (Ta´ala) na ukasikiliza hoja za Allaah na ubainisho Wake, hutokhofu na wala hutohuzunika.

نَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا إِ

”Hakika hila za shaytwaan ni dhaifu.” (an-Nisaa 04 : 76)

Mtu ambaye si msomi katika Muwahhidiyn watu wa Tawhiyd anashinda watu elfu katika wanachuoni wa washirikina. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ

”Na kwamba hakika jeshi Letu ndilo litakaloshinda.” (asw-Swaffaat 37 : 173)

Jeshi la Allaah ndio washindi kwa hoja na kwa ulimi, kama ambavyo wanashinda kwa panga na kwa mikuki. Khofu ni juu ya Muwahhid ambaye anapita katika njia bila ya kuwa na silaha. Na Allaah (Ta´ala) Katuneemesha kwa Kitabu ambacho Kakifanya ni bayana ya kila kitu, na ni mawaidha na Rahmah kwa Waislamu. Mtu wa batili hawezi kuja na hoja isipokuwa katika Qur-aan kuna (dalili) inayoivunja na kubainisha ubatili wake. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

”Na wala hawatakujia kwa mfano wowote (ule wa hoja ya kupinga au kutafuta kosa katika Qur-aan) isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri nzuri kabisa (dhidi ya mfano wao).” (al-Furqaan 25 : 33)

Wamesema baadhi ya wafasiri, Aayah hii ni jumla ya kila hoja ambayo watakuja nayo watu wa batili mpaka siku ya Qiyaamah.

 Mlango Wa 7

 Radd (Jawabu) kwa watu wa batili kwa jumla na kwa kina

Na nitakutajia kitu katika yale Aliyotaja Allaah katika Kitabu Chake jibu kwa maneno ambayo washirikina wa zama zetu wanatumia kama hoja dhidi yetu. Tunasema “Majibu kwa watu wa batili ni katika njia mbili: Mujmal la kijumla na mufasswal la kina.”

 Ama jibu la kijumla

Kwa hakika ni jambo kubwa na faida kubwa kwa yule mwenye kulifahamu. Nalo ni Kauli Yake Allaah (Ta´ala):

 هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ

”Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayah Muhkam (zilizo wazi maana yake) hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo ni mutashaabih (haziko wazi maana yake). Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zilizoshabihiana kutafuta fitnah na kutafuta tafsiri zake; na hakuna ajuae tafsiri zake isipokuwa Allaah. Na Ar-Raasikhuwna (wenye msingi madhubuti) katika elimu husema: “Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Mola wetu.” Na hawakumbuki ila wenye akili.” (a-´Imraan 03 : 07)

Imepokelewa Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Ukiwaona wale wanaofuata [Aayah za] Mutashaabih basi hao ndio wale ambao Allaah Kawasema (kwenye Qur-aan); hivyo tahadhari nao!”

Mfano wa hilo, ni pale baadhi ya washirikina wanaposema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii (vipenzi) vya Allaah (wanaoamini Tawhiyd ya Allaah, na kujiepusha madhambi na maovu yote yaliyokatazwa) hawana khofu juu yao, na wala hawatohuzunika.” (Yuunus 10 : 62)

Au anasema ya kwamba Shafaa´ah uombezi ni haki, au ya kwamba Mitume wana jaha mbele ya Allaah. Au akataja maneno kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analitolea dalili kwa kitu katika batili yake, ilihali wewe hufahamu maana ya maneno aliyoyataja. Mjibu kwa kusema: “Kwa hakika Allaah Kasema katika Kitabu Chake ya kwamba wale ambao moyoni mwao mna upotofu, wanaacha [Aayah za] Muhkaam na wanafuata [Aayah za] Mutashaabih. Na katika yale niliyokutajia ya kwamba Allaah Kataja ya kwamba washirikina walikuwa wanakubali Rubuubiyyah na kukufuru kwao ilikuwa ni kwa kujikurubisha kwao kwa Malaika, Mitume, mawalii kwa kusema kwao:

 هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10 : 18)

Hili ni jambo la Muhkam lililo wazi na wala hawezi yeyote kubadilisha maana yake. Wewe mshirikina! Sielewi maana ya uliyoyataja katika Qur-aan au maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini nina uhakika ya kwamba maneno ya Allaah hayagongani, na kwamba maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayaendani kinyume na maneno ya Allaah. Na hili ni jibu zuri sana, lakini halifahamu isipokuwa yule ambaye Allaah Kampa ufahamu. Hivyo, usilidharau. Kwa hakika Allaah (Ta´ala) Anasema:

وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

”Na hawatopewa (sifa hii) isipokuwa wale waliosubiri, na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu kubwa.” (Fusw-Swilat 41 : 35)

 Ama jibu la kina

Kwa hakika maadui wa Allaah wana vipingamizi vingi dhidi ya Dini ya Mitume, (vipingamizi) ambavyo wanawazuia kwavyo watu. Katika (maneno) yao ni pamoja na kusema kwao: “Sisi hatumshirikishi Allaah, bali sisi tunashuhudia ya kwamba hakuna Mwenye kuumba, wala hakuna Mwenye kuruzuku, wala hakuna Mwenye kunufaisha wala kudhuru isipokuwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika, na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamiliki katika nafsi yake si manufaa wala madhara, tusiseme ´Abdul-Qaadir au mwengine yeyote.

Lakini mimi ni mwenye kufanya madhambi na hawa watu wema wana jaha mbele ya Allaah. Na ninamuomba Allaah kwa kupitia kwao. Mjibu kwa yaliyotangulia, nayo ni: Wale ambao Mtume wa Allaah alipigana nao vita walikuwa wanakubali hayo uliyoyataja. Na walikubali ya kwamba waungu (masanamu) yao hayaendeshi kitu, isipokuwa tu walichokuwa wanataka ni jaha na shafaa´ah uombezi. Msomee Aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake na Kuyaweka wazi.

Akikwambia: “Aayah hizi ziliteremshwa kwa wale waliokuwa wanaabudu masanamu! Vipi mtawafanya watu wema ni kama masanamu? Au vipi mtawafanya Mitume ni kama masanamu?” Mjibu kwa yaliyotangulia.

Hivyo, ikiwa atakubali ya kwamba makafiri wanashuhudia kuwa Rubuubiyyah yote ni ya Allaah, na kwamba hawakutaka chochote kutoka kwao zaidi isipokuwa shafaa´ah uombezi. Lakini anachotaka ni kutofautisha baina ya kitendo chao na kitendo chake kwa tulichokitaja. Mkumbushe ya kwamba (miongoni mwa) makafiri kulikuwa wanaoabudu watu wema na masanamu, na miongoni mwao kulikuwa wanaowaomba mawalii. Ambao Allaah Anasema kuhusu wao:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ

”Hao wanaowaomba (kama ‘Iysaa, ‘Uzayr, Malaika, Mawalii na wingineo, wao wenyewe) wanatafuta kwa Mola wao Wasiylah (njia ya kujikurubisha kwa Allaah); (na hata) walio karibu sana miongoni mwao (kama Malaika wanafanya hivyo).” (al-Israa 17 : 57)

Na wanamuomba ´Iysa bin Maryam na mama yake. Allaah Kasema:

مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ۖ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَۗ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمُ الْآيَاتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ

”Al-Masiyh mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume (tu); bila shaka wamekwishapita kabla yake Mitume (wengine). Na mama yake ni swiddiyqah (mkweli). Wote wawili walikuwa wanakula chakula (na hivyo wakipata choo). Tazama jinsi Tunavyowabainishia Aayah, kisha tazama vipi wanavyogeuzwa (kuacha haki).” (al-Maaidah 05 : 75)

قُلْ أَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا ۚ وَاللَّـهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

”Sema: “Vipi mnaabudu asiyekuwa Allaah asiyemiliki (uwezo wa) kukudhuruni wala kukunufaisheni! Na Allaah Ndiye As-Samiy’ul- ‘Aliym” (Mwenye Kusikia yote daima – Mjuzi wa yote Daima).” (al-Maaidah 05 : 76)

Mtajie Kauli Yake Allaah (Ta´ala):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

”Na (kumbusha, taja) Siku Atakayowakusanya wote, kisha Atawaambia Malaika: “Je, hawa (ndio) waliokuwa wakikuabuduni nyinyi?” Watasema: “Subhaanak (Umetakasika)! Wewe ni Walii wetu sio hao!” Bali walikuwa wakiabudu majini, wengi wao wakiwaamini (hao majini).” (Sabaa 34 : 40-41)

Na Kauli Yake Allaah (Ta´ala):

وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ

” Na (Tahadhari) Atakaposema Allaah: “Ee ‘Iysaa mwana wa Maryam! Je, wewe uliwaambia watu (hivi): “Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu miwili asiyekuwa Allaah?” (‘Iysaa) Akasema: “Subhaanak (Utakaso ni Wako)! Hainipasi mimi kusema yasiyo kuwa haki kwangu.” (Maaidah 05 : 116)

Mwambie: “Umejua sasa ya kwamba Allaah Kamkufurisha yule aliyeyakusudia masanamu na watu wema na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Akapigana nao vita?” Ikiwa atasema: “Makafiri walikuwa wanataka (manufaa na madhara) kutoka kwao, na mimi ninashuhudia ya kwamba Allaah ndiye Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru na Mwendeshaji wa mambo. Sitaki (manufaa na madhara) isipokuwa kutoka Kwake. Na watu wema hawana katika hilo lolote. Lakini ninawaomba kwa kuwa natarajia kutoka kwa Allaah shafaa´ah uombezi wao.” Jibu ni kuwa, maneno haya na yale ya makafiri ni sawa sawa.

Msomee Kauli Yake Allaah (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Na wale waliojichukulia badala Yake awliyaa (wasaidizi, miungu; wakisema): “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.” (az-Zumar 39 : 03)

Na Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah”.” (Yuunus 10 : 18)

Jua ya kwamba shubuha hizi tatu ndio kubwa walionazo.

Ukishajua kuwa Allaah Katuwekea nayo wazi katika Kitabu Chake na ukazifahamu vizuri, yaliyo baada yake yatakuwa sahali zaidi kuliko hayo.

 Mlango Wa 8

 Radd (Jawabu) kwa mwenye kudai kwamba Du´aa sio ´Ibaadah

Akisema: “Mimi siabudu mwengine yeyote isipokuwa Allaah, na huku kutafuta kinga kutoka kwao (watu wema) na kuwaomba (Du´aa) sio ´Ibaadah. Mwambie: “Wewe unajua (unakubali) ya kwamba Allaah Kafaradhisha juu yako kumtakasia ´Ibaadah, na ni haki Yake juu yako?” Akisema: “Ndio”. Mwambie: “Nibainishie (nieleze) hili ulilofaradhishiwa juu yako?” Nalo ni Ikhlaasw kumtakasia ´Ibaadah Allaah Mmoja. Na ni haki Yake juu yako. Ikiwa hajui ´Ibaadah na wala aina zake (za hiyo ´Ibaadah) mbainishie kwa kauli yako. Kasema Allaah (Ta´ala):

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً

”Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa khofu.” (al-A´raaf 07 : 55)

Ukishamjulisha (muwekea wazi) hili, mwambie: “Unajua sasa kuwa hii ni ´Ibaadah?” Hana budi kusema: “Ndio” – na Du´aa ni kichwa cha ´Ibaadah. Mwambie: “Ikiwa umekubaliana na mimi ya kwamba ni ´Ibaadah na unamuomba Allaah usiku na mchana, kwa khofu na unyenyekevu, kisha ukaomba kwa haja hiyo Mtume au asiyekuwa yeye, je utakuwa umeshirikisha katika ´Ibaada ya Allaah asiyekuwa Yeye?” Hana budi kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Kwa hiyo unajua Kauli ya Allaah (Ta´ala):

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

” Basi swali kwa ajili ya Mola wako na (pia ukichinja) na chinja (kwa ajili Yake).” (at-Takaathur 108 : 02)

ukamtii Allaah na ukamchinjia. Je, hii ni ´Ibaadah?” Hana budi kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Ukimchinjia kiumbe; sawa awe ni Mtume, Jini au wasiokuwa hao. Je, utakuwa umeshirikisha katika ´Ibaadah hii asiyekuwa Allaah?” Hana budi kukubali na kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Washirikina ambao waliteremshiwa Qur-aan, je walikuwa wakiabudu Malaika, watu wema, Laat na wengineo?” Hana budi kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Je, ´Ibaadah yao (kuwaabudu) kwao ilikuwa ni katika Du´aa tu, kuchinja na kutafuta kinga kwao na mfano wa hayo?” La sivyo walikuwa wakikiri ni waja Wake, chini ya uwezo Wake na kwamba Allaah ndiye Mwenye kuendesha mambo, lakini waliwaomba na kutegemea jaha kutoka kwao na maombezi – na hili ni jambo liko wazi sana.”

 Mlango Wa 9

 Tofauti kati ya Shafaa´ah (Uombezi) wa Kishari´ah na Shirki (Ushirikina)

Akisema: “Je wewe unakataa (unapinga) shafaa´ah uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuikana?” Mwambie: “Siipingi na wala siikani, bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye muombezi wa waombezi na nataraji kupata uombezi wake.” Lakini uombezi wote (unamiliki) ni wa Allaah (Ta´ala). Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا

”Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Uombezi wote ni wa Allaah.” (az-Zumar 39 : 44)

Na wala haitokuwa (mtu hatoombea) ila baada ya idhini ya Allaah. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

 مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

”Nani huyu ambaye anashufai (anayeombea) mbele Yake bila ya idhini Yake.” (al-Baqarah 02 : 255)

Na wala hatoomwombea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeyote ila baada ya Allaah Kumruhusu. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

”Na wala hawamuombei shafaa’ah (yeyote yule) isipokuwa kwa yule ambaye (Allaah) Amemridhia.” (al-Anbiyaa 21 : 28)

Na Yeye (Subhaanah) Haridhii isipokuwa Tawhiyd. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

 وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ

”Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake.” (al-´Imraan 03 : 85)

Ikiwa uombezi wote ni wa Allaah na wala hautokuwa ila baada ya idhini Yake, na wala hatoombea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala mwengine yeyote mpaka Allaah Amruhusu - na wala Allaah Haridhii isipokuwa watu wa Tawhiyd – imekubainikia ya kwamba shafaa´ah uombezi wote ni wa Allaah. Hivyo naitafuta kutoka Kwake (Allaah). Ninasema: “Ee Allaah, usiniharamishie uombezi Wake”, ”Ee Allaah ninakuomba aniombee” na mfano wa hayo.

Akisema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kapewa shafaa´ah na mimi naomba kile Alichompa Allaah.” Jibu ni kuwa: “Ni kweli kuwa Allaah Kampa shafaa´ah uombezi, lakini Amekukataza hili (yaani kuomba mtu mwengine isipokuwa Yeye). Kasema ”Msiombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Allaah.”. Ikiwa utamuomba Allaah Akupe uombezi wa Mtume, tii Kauli Yake:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

”Msiombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

Isitoshe shafaa´ah uombezi umepewa wengine kuliko Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imesihi ya kwamba Malaika watawaombea, mawalii watawaombea na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe watawaombea. Utasema ya kwamba: “Kwa vile Allaah Kawapa uombezi hivyo nitaiomba kutoka kwao?” Ukisema hivyo, utakuwa umerejea katika kuwaabudu watu wema ambao Allaah Kawataja katika Kitabu. Na ukisema: “Hapana”, kauli yako inakuwa batili: “Allaah Kawapa shafaa´ah uombezi na mimi ninaomba kile Alichowapa Allaah.”

 Mlango Wa 10

 Uthibitisho ya kwamba kuwategemea watu wema ni Shirki

Akisema: “Simshirikishi Allaah na chengine chochote, kamwe, lakini kuwaelekea watu wema sio Shirki”. Mwambie: “Ukiwa kweli unakubali ya kwamba Allaah Ameharamisha Shirki na kwamba ni jambo kubwa kuliko Zinaa na unakubali ya kwamba Allaah Hatoisamehe, ni jambo gani sasa ambalo Allaah Kaharamisha na Kasema kwamba Hatolisamehe?” Kwa hakika hajui. Mwambie: “Vipi utajitakasa nafsi yako na Shirki na wewe huijui? Au vipi Allaah Atakuharamishia wewe hili na Kutaja ya kwamba hatolisamehe, wakati wewe huliulizii na wala hulijui? Wafikiria ya kwamba Allaah Atatuharamishia na wala Asitubainishie?” Akisema: “Shirki ni kuabudu masanamu, na sisi hatuabudu masanamu” Mwambie: “Na nini maana ya kuabudu masanamu? Unafikiria ya kwamba walikuwa wanafikiria kuwa miti ile na mawe yale, yanaumba na yanaruzuku na yanaendesha mambo kwa yule anayeviomba? Hili linakadhibishwa na Qur-aan!”

Akisema: “Ni yule mwenye kukusudia mti, jiwe au nyumba iliyojengwa kwenye kaburi n.k, anakiomba, kukichinjia na kusema: “Kinatukurubisha kwa Allaah na Allaah Anatulinda (na madhara) kwa baraka zake na Anatupa baraka Zake” Mwambie: “Umesema kweli. Na hichi ndio kitendo chenu kwenye makaburi na manyumba yaliyo kwenye makaburi na mengineyo.”

Hili amelikubali ya kwamba kitendo chao hichi ni kuabudu masanamu na ndio iliokuwa inatakikana. Mtu anaweza kumwambia pia: “Kauli yako, kwamba Shirki ni kuabudu (tu) masanamu; je unamaanisha ya kwamba Shirki ni khaswa (maalum) kwa hili, na kwamba kuwategemea watu wema na kuwaomba hayaingii katika hilo (Shirki)?”

Anaradiwa (anajibiwa) na Aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake kuhusu kukufuru kwa yule ambaye kamtegemea Malaika, ´Iysa na watu wema. Lazima akukubalie ya kwamba mwenye kumshirikisha katika ´Ibaadah ya Allaah miongoni kwa watu wema, ndio Shirki iliyotajwa kwenye Qur-aan, na ndio iliyokuwa inatakikana.

Siri ya masuala ni kwamba akisema: “Mimi simshirikishi Allaah”. Mwambie: “Nieleze, ni nini kumshirikisha Allaah?” Akisema: “Ni kuabudu masanamu” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kuabudu masanamu?” Akisema: “Mimi siabudu isipokuwa Allaah Mmoja” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kumuabudu Allaah Mmoja?” Akikueleza (kubainishia) kama ilivyoeleza Qur-aan, ndio kinachotakikana. Na ikiwa hajui, vipi atadai kitu na yeye hakijui?

Na akikubainishia kinyume na maana yake, mbainishie Aayah zilizo za wazi za maana ya kumshirikisha Allaah na ´Ibaadah kuabudu masanamu na kwamba ndio yale yale wayafanyayo leo, na kwamba ´Ibaadah kumuabudu Allaah Mmoja pasina mshirika, ndio yale wanayotupinga kwayo na wanasifu, kama walivyosifu ndugu zao pale waliposema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا

“Amewafanya miungu (wote) kuwa ni Ilaah (Mungu) Mmoja?” (Swad 38: 05)

Akisema: “Kwa hakika hawakukufuru kwa kuwaomba Malaika na Mitume, bali walikufuru waliposema: “Malaika ni watoto wa Allaah”, sisi hatusemi kuwa ´Abdul-Qaadir ni mtoto wa Allaah wala mwengine yeyote” jibu ni: “Kumnasibishia mtoto Allaah ni kufuru ya kivyake. Allaah (Ta´ala) Anasema:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ

“Sema: “Yeye ni Allaahu Ahad (Mmoja Pekee). “Allaah ni Asw-Swamad (Mwenye kukusudiwa kwa haja zote).” (al-Ikhlaasw 112 : 1-2)

Na kwamba Yeye ni Mmoja asiyekuwa na anayelingana Naye, na “asw-Swamad” mkusudiwa kwa haja. Atakayepinga hili, atakuwa amekufuru, hata kama hakupinga Suurah.” Allaah Anasema:

مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ

”Allaah Hakuchukua mtoto yeyote, na wala hakukuwa pamoja Naye ilaah (miungu yeyote mingine).” (al-Muuminuun 23 : 91)

Katofautisha baina ya sampuli mbili na Kafanya yote mawili ni kufuru ya kivyake. Kasema Allaah (Ta´ala):

وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ الْجِنَّ وَخَلَقَهُمْ ۖ وَخَرَقُوا لَهُ بَنِينَ وَبَنَاتٍ بِغَيْرِ عِلْمٍ

”Na (juu ya hivyo) wamemfanyia Allaah majini kuwa ni washirika Wake; na hali (Yeye Ndiye) Aliyewaumba. Na wakamsingizia bila ya ujuzi.” (al-An´aam 06 : 100)

Katofautisha baina ya kufuru hizo mbili. Dalili ya hilo pia ni kwamba waliokufuru kwa kumuomba Laat – pamoja na kuwa ni mtu mwema – hawakumfanya ni mtoto wa Allaah, waliokufuru kwa kuabudu Jini, hawakumfanya hali kadhalika. Hali hadhalika wanachuoni wa madhehebu yote manne wanasema katika: “Mlango: Hukumu ya mwenye kuritadi”, ya kwamba Muislamu akidai ya kwamba Allaah ana mtoto, ni murtadi, na wanatofautisha baina ya aina hizo mbili – na hili ni jambo liko wazi.

Akisema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii (vipenzi) vya Allaah (wanaoamini Tawhiyd ya Allaah, na kujiepusha madhambi na maovu yote yaliyokatazwa) hawana khofu juu yao, na wala hawatohuzunika.” (Yuunus 10 : 62)

Mwambie: “Hii ni haki, lakini hawaabudiwi.” Na sisi hatukutaja jengine isipokuwa tu kule kuwaabudu kwao pamoja na Allaah. La sivyo, ni wajibu kwako kuwapenda, kuwafuata na kukubali karama zao. Na wala hawapingi karama za mawalii isipokuwa Ahl-ul-Bid´ah wad-Dhwalaal (Wazushi na waliopotea). Na Dini ya Allaah iko kati ya mambo mawili, uongofu baina ya upotofu mbili na haki baina ya batili mbili.

 Mlango Wa 11

 Uthibitisho ya kwamba Shirki ya watu wa mwanzo ni khafifu kuliko Shirki ya watu wa zama zetu

Ukishajua waliitalo washirikina katika zama zetu hizi “Itikadi” ndio Shirki iliyoteremka katika Qur-aan na akapigana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu kwa ajili yayo, basi ujue kuwa Shirki ya watu wa mwanzo ni khafifu kuliko Shirki ya watu wa zama zetu kwa mambo mawili.

La kwanza: Watu wa mwanzo walikuwa hawashirikishi na wala hawawaombi Malaika, mawalii na masanamu pamoja na Allaah isipokuwa wakati wa raha. Ama wakati wa shida, walikuwa ni wenye kumtakasia Allaah Dini. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

”Na inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba (hamuwaiti wakati huo wa shida) isipokuwa (mnamwita na kumuomba Allaah) Yeye Pekee. Anapokuokoeni (na kukufikisheni salama) nchi kavu; mnakengeuka. Na binaadamu daima ni mwingi wa kukanusha (asiyekuwa na shukurani kwa neema za Allaah).” (al-Israa 17 : 67)

Na Kauli Yake:

قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ أَوْ أَتَتْكُمُ السَّاعَةُ أَغَيْرَ اللَّـهِ تَدْعُونَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ بَلْ إِيَّاهُ تَدْعُونَ فَيَكْشِفُ مَا تَدْعُونَ إِلَيْهِ إِن شَاءَ وَتَنسَوْنَ مَا تُشْرِكُونَ

”Sema: “Je mnaonaje ikikufikieni adhabu ya Allaah au ikakufikieni Saa (ya Qiyaamah); je, mtamwomba asiyekuwa Allaah (akuepusheni) mkiwa ni wakweli?” Bali Yeye Pekee Ndiye mtayemwomba, kisha Atakuondoleeni yale mliyomwomba (Atakuondoleeni) Akitaka; na mtasahau yale mnayoyashirikisha (pamoja Naye)”.” (al-An´aam 06 : 40-41)

Na Kauli Yake:

وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَا رَبَّهُ مُنِيبًا إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا خَوَّلَهُ نِعْمَةً مِّنْهُ نَسِيَ مَا كَانَ يَدْعُو إِلَيْهِ مِن قَبْلُ وَجَعَلَ لِلَّـهِ أَندَادًا لِّيُضِلَّ عَن سَبِيلِهِ ۚ قُلْ تَمَتَّعْ بِكُفْرِكَ قَلِيلًا ۖ إِنَّكَ مِنْ أَصْحَابِ النَّارِ

”Na inapomgusa binaadamu dhara, humwomba Mola wake akirudiarudia Kwake (Pekee) kutubia, kisha Akimtunukia Neema kutoka Kwake, husahau yale aliyokuwa akimwomba kabla, na kumfanyia Allaah (miungu) walinganifu (Naye) ili apotee (na apoteze watu) Njia Yake (Allaah). Sema: “Starehe kwa kufuru yako kidogo (tu); hakika wewe ni miongoni mwa watu wa motoni.” (az-Zumar 39 : 08)

Na Kauli Yake:

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

”Na yanapowafunika mawimbi kama vivuli (kwa machafuko ya bahari), humwomba Allaah wakimtakasia Dini Yake.” (Luqmaan 31 : 32)

Atakayefahamu masuala haya ambayo Allaah Kayaweka wazi katika Kitabu Chake – nayo ni kwamba washirikina ambao aliwapiga vita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakimuomba Allaah (Ta´ala) na wakiomba asiyekuwa Yeye (wengine) katika raha, ama wakati mgumu na wa shida hawamuombi mwengine isipokuwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika na wanawasahau bwana zao – umembainishia tofauti baina ya watu wa zama zetu na Shirki ya watu wa mwanzo. Lakini ni nani ambaye moyo wake unayafahamu mambo haya ufahamu wa ndani kabisa? Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada.

Jambo la pili: Watu wa mwanzo walikuwa wakiomba pamoja na Allaah watu waliokuwa karibu na Allaah. Ima Mitume, mawalii au Malaika. Na wanaomba miti au mawe vinavyomtii Allaah na havimuasi. Lakini watu wa zama zetu wanaomba pamoja na Allaah katika mafusaki ya watu. Na wale wanaowaomba ndio wanaowahalalishia maovu; Zinaa, kuiba, kuacha Swalah na kadhalika. Na yule anayemuamini mtu mwema au yule ambaye haasi, kama mfano wa mti na jiwe, ni uovu kidogo kuliko yule anayemuamini yule anayeshuhudia anafanya madhambi na ufisadi na akathibitisha hilo.

 Mlango Wa 12

 Jibu kwa anayedai ya kwamba mwenye kutimiza nguzo za Uislamu hawezi kuwa kafiri

Ukihakikisha (elewa) ya kwamba wale aliyowapiga vita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa na akili nzuri na Shirki kidogo kuliko watu hawa, basi jua kuwa hawa wana shubuha wanazozitaja kwa tuliotaja, na ni katika shubuha zao kubwa, hivyo sikiliza vizuri majibu yake. Wanasema: “Wale ambao Qur-aan iliwateremkia walikuwa hawashuhudii Laa ilaaha illa Allaah hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na walikuwa wanamkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanapinga kufufuliwa, wanakadhibisha Qur-aan na kuiona kuwa ni uchawi. Ama sisi tunashuhudia Laa ilaaha illa Allaah ya kwamba hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na tunaisadikisha Qur-aan, na tunaamini kufufuliwa, tunaswali na tunafunga. Vipi basi mtatufanya sisi ni kama wao?”

Jibu ni: “Hakuna tofauti baina ya wanachuoni wote, ya kwamba mtu akimsadikisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kitu na akamkadhibisha katika kitu kingine, ni kafiri ambaye hakuingia katika Uislamu. Hali kadhalika (ni kafiri) akiamini baadhi ya Qur-aan na akapinga baadhi yake, kama mwenye kukubali Tawhiyd na akakadhibisha (kupinga) uwajibu wa Swalah, au akakubali Tawhiyd na Swalah na akakadhibisha uwajibu wa Zakaah, au akakubali Tawhiyd na Swalah na akakadhibisha uwajibu wa Zakaah, au akakubali yote haya na akakadhibisha Swawm, au akakubali yote haya na akakadhibisha Hajj. Na wakati watu hawakulalamika katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Hajj, Allah Aliteremsha kuhusu wao:

 وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلً ¤ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ا

”Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni Ghaniyy (Mkwasi, Hahitaji lolote) kwa walimwengu.” (al-´Imraan 03 : 97)

Na mwenye kukubali yote haya na akakadhibisha kufufuliwa, anakufuru kwa Ijmaa´ na ni halali damu yake na mali yake. Kama Alivyosema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا ۚ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا

”Hakika wale waliomkanusha Allaah na Mitume Yake; na wanataka kufarikisha baina ya Allaah na Mitume Yake; na wanasema: “Tunaamini baadhi na tunawakanusha baadhi”; na wanataka kuchukua njia iliyo baina (kati kati) ya hayo. Hao ndio makafiri wa kweli. Na Tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.” (an-Nisaa 04 : 150-151)

Ikiwa Allaah Kaweka wazi katika Kitabu Chake ya kwamba mwenye kuamini baadhi na akakufuru baadhi, basi ni kafiri wa kweli na kwamba anastahiki Alichokitaja, shubuha hii itakuwa imetoweka. Na hiki ni kitu walichosema watu kutoka al-Ahsaaa katika kitabu chao walichotutumia.

Mtu anaweza kusema pia: “Ikiwa unakubali ya kwamba mwenye kumsadikisha Mtume katika kila kitu na akakadhibisha uwajibu wa Swalah, ni kafiri ambaye ni halali damu yake kwa Ijmaa´, hali kadhalika akikubali kila kitu isipokuwa kufufuliwa, hali kadhalika lau atakadhibisha uwajibu wa kufunga Swawm ya Ramadhaan, hakanushi isipokuwa haya ilihali mengine yote anayasadikisha - madhehebu mbali mbali wamekubaliana kwa hili na Qur-aan imeliongelea kama tulivyosema – mtu atafahamu (elewa) ya kwamba Tawhiyd ndio faradhi kubwa aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni kubwa kuliko Swalah, Zakaah, Swawm na Hajj. Vipi itakuwa mtu akikadhibisha kitu katika mambo haya anakufuru – hata kama atayafanyia kazi mambo yote aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na akikadhibisha (pinga) Tawhiyd ambayo ni Dini ya Mitume wote asikufuru, Subhaana Allaah! Ni ajabu ilioje ya ujinga huu.

Mtu anaweza kusema pia: “Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walipigana vita na Banuu Haniyfah, ilihali walikuwa Waislamu pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wao wanashuhudia Laa ilaaha illa Allaah hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, wa anna Muhammad ni Rasuulu Allaah Mtume wa Allaah, walikuwa wanaswali na wakiadhini.” Akisema: “Walisema: “Musaylamah ni Mtume”, mwambie: “Hili ndilo lililokuwa linatakikana. Ikiwa yule anayempandisha mtu katika daraja ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakufuru na mali yake inakuwa halali na damu yake, na wala haimfai Shahaadah mbili na wala Swalah, vipi kwa mwenye kumpandisha Shamsaan, au Yuusuf, au Swahabah, au Mtume katika daraja ya Al-Jabbaar wa mbingu na ardhi? Subhaana Allaah! Ni Ukubwa ulioje alonao.

كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ

”Hivyo ndivyo Allaah Anavyopiga muhuri juu ya nyoyo za wale wasiojua.” (ar-Ruum 30 : 59)

Yaweza kusemwa pia: “Wale ambao ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhu) aliwaua kwa kuwaunguza, wote walikuwa wakidai Uislamu. Walikuwa ni katika wafuasi wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhu) na walisoma elimu kutoka kwa Maswahabah, lakini walimuamini ´Aliy kama Imani kwa Yuusuf, Shamsaan na mfano wao. Vipi walikubaliana Maswahabah kuwapiga vita na kuwaona kuwa ni makafiri? Je, wadhania ya kwamba Maswahabah wanawakufurisha Waislamu au mnadhania ya kwamba Imani kwa Taaj na mfano wake haidhuru, wakati Imani (kumuamini) ´Aliy bin Abiy Twaalib ndio inakufurisha?

Yaweza kusemwa pia: “Banuu ´Ubayd al-Qaddaah, waliokuwa wanamiliki Magharibi na Misri katika zama za Banuu al-´Abbaas, wote walikuwa wakishuhudia Laa ilaaha illa Allaah hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah wa anna Muhammad Rasuulu Allaah Muhammad ni Mtume wa Allaah na wanadai Uislamu na wanaswali Ijumaa na Jamaa´ah. Ilipodhihiri kukhalifu kwao Shari´ah katika mambo duni ya ambayo tuliyomo, walikubaliana wanachuoni kwamba ni makafiri na kwamba inatakiwa kuwapiga vita na kwamba miji yao ni miji ya vita. Hivyo Waislamu wakawashambulia mpaka wakaokoa waliokuwa nayo katika miji ya Waislamu.”

Yaweza kusemwa pia: “Ikiwa (watu) wa mwanzo hawakukufuru, isipokuwa kwa kujumuisha kwao baina ya Shirki na kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Qur-aan na kupinga kufufuliwa na kadhalika, ni nini maana ya mlango uliotajwa na wanachuoni wa kila madhehebu “Mlango: Hukumu ya mwenye kuritadi”, naye ni yule Muislamu ambaye anakufuru baada ya Uislamu wake? Halafu wakataja aina nyingi; kila aina inakufurisha na kuhalalisha damu ya mtu na mali yake. Mpaka walitaja mambo ambayo yalionekana ni madogo kwa yule mwenye kuyafanya, kama mfano maneno yaliosemwa na mdomo wake bila ya kuyamaanisha (kuyakusudia) moyoni mwake au maneno aliyosema kwa njia ya mzaha na utani.

Yaweza kusemwa pia: “Wale ambao Allaah Kasema kuwahusu:

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

”Wanaapa kwa Jina la Allaah (kwamba) hawakusema (maneno maovu kuhusu Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na hali wamekwishasema neno la kufuru, na wakakufuru baada ya Uislamu wao.” (at-Tawbah 09 : 74)

Hamkusikia ya kwamba Allaah Kawakufurisha kwa maneno yao, pamoja na kuwa walikuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakipigana Jihaad pamoja naye, wakiswali pamoja naye, wakitoa Zakaah pamoja naye, kuhiji na wakimpwekesha Allaah?

Hali kadhalika wale ambao Allaah Kasema kuwahusu:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَلَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mjumbe Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09 : 65-66)

Watu hawa ambao Allaah Kaweka wazi ya kwamba wamekufuru baada ya kuamini kwao – pamoja na kuwa wako na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk – walisema maneno ambayo walisema kuwa waliyasema kwa mzaha tu.

Fikiria shubuha hii, nayo ni kauli yao: “Je, mnawakufurisha Waislamu ambao wanashuhudia Laa ilaaha illa Allaah hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na wanaswali na wanafunga?” Kisha fikiria jibu lake. Kwa hakika ni katika yamanufaa yaliomo kwenye waraka hii.

Na katika dalili ya hayo pia, Aliyosema Allaah (Ta´ala) kuhusu Banuu Israaiyl – mbali na Uislamu wao, elimu yao na wema wao – walimwambia Muusa: “Tujaalie (tufanyie) mungu kama wao walivyo na waungu”. Hali kadhalika walisema baadhi ya Maswahabah: “Tujaalie Dhaat Anwaat”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaapa ya kwamba hii inakumbusha kauli ya Banuu Israaiyl: “Tufanyie mungu”.

 Mlango Wa 13

 Hukumu ya Muislamu anaetumbukia kwenye Shirki bila ya kujua kisha akatubia

Washirikina wana shubuha nyingine ambayo wanajaribu kuijadili kwa kisa hiki. Wanasema: “Kwa hakika Banuu Israaiyl hawakukufuru kwa hilo na hali hadhalika waliosema “Tufanyie Dhaat Anwaat”, hawakukufuru. Tunawajibu kwa kusema: “Banuu Israaiyl hawakufanya hilo, na hali kadhalika waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakufanya hilo. Na wala hakuna tofauti ya kwamba Banuu Israaiyl hawakufanya hilo, na lau wangelifanya hilo wangelikufuru. Na wala hakuna tofauti ya kwamba wale aliowakataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lau wasingelimtii na wakachukua Dhaat Anwaat baada ya makatazo, wangelikufuru. Na hili ndilo linalotakikana.

Lakini kisa hiki kinafidisha ya kwamba Muislamu wa kawaida, bali hata mwanachuoni, anaweza kutumbukia katika aina ya Shirki bila ya kujua. Kinafidisha kujifunza na kuwa makini na kujua ya kwamba maneno ya mjinga “Tunajua Tawhiyd” ni katika ujinga mkubwa na hila za Shaytwaan. Kinafidisha pia ya kwamba Muislamu akitamka kwa neno la kufuru na yeye hajui, akajua hilo na kutubia moja kwa moja ya kwamba hakufuru, kama walivyofanya Banuu Israaiyl na wale waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na kinafidisha pia ya kwamba lau ikiwa hakukufuru, amkemee (aliyesema maneno hayo) kwa makemeo makali kabisa, kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

 Mlango Wa 14

 Radd (Jawabu) kwa mwenye kudai kukomeka na anayesema “Laa ilaaha illa Allaah” hata kama ataleta yanayoivunja

Washirikina wana shubuha nyingine. Wanasema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkataza Usaamah mtu aliyesema: “Laa ilaaha illaa Allaah”. Na akamwambia:

“Je, unamuua baada ya yeye kusema “Laa ilaaha illa Allaah”.”

Hali kadhalika kauli yake:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Laa ilaaha illa Allaah”.”

Na kuna Hadiyth zingine zinazozungumzia kukomeka (kumsalimisha) kwa mwenye kuitamka. Makusudio ya hawa wajinga ni kwamba mwenye kuitamka hawezi kukufuru wala hauawi, walau atafanya yakufanya.

Ndio maana inatakiwa kusemwa kwa hawa wajinga: “Ni jambo linalojulikana ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita Mayahudi na akawafunga na wao wanasema “Laa ilaaha illa Allaah”. Na Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walipigana vita na Baniy Haniyfah nao wanashuhudia “Laa ilaaha illa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah”, na wanaswali na kudai Uislamu. Hali kadhalika wale aliowaunguza kwa moto ´Aliy bin Abiy Twaalib. Na wajinga hawa wanasema yule mwenye kupinga kufufuliwa anakufuru na kuuawa, hata kama atasema “Laa ilaaha illa Allaah”, na yule mwenye kupinga chochote katika nguzo za Uislamu amekufuru na kuuawa, hata ikiwa ataitamka (Shahaadah). Vipi basi isimfai ikiwa kapinga kitu katika mambo ya Furuu´ matawi, lakini imfae akipinga Tawhiyd ambayo ni msingi na asli ya Dini ya Mitume? Lakini maadui wa Allaah Hawakufahamu maana ya Hadiyth.

Ama Hadiyth kuhusu Hadiyth ya Usaamah, alimuua mtu ambaye alidai Uislamu kwa sababu alidhani ya kwamba anadai Uislamu kwa khofu tu ya kuuliwa na mali yake. Na mtu akidhihirisha Uislamu, basi ni wajibu kukomeka naye mpaka ibainike yanayokhalifu hilo. Allaah Kateremsha kuhusiana na hilo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Mnaposafiri (kupigana jihaad) katika njia ya Allaah hakikisheni.” (an-Nisaa 04 : 94)

Yaani “hakikisheni”. Aayah inatoa dalili ya kwamba ni wajibu kukomeka naye mpaka mtu ahakikishe. Baada ya muda kukibainika kutoka kwake yanayokhalifu Uislamu, anauawa, kwa Kauli Yake (Ta´ala) “hakikisheni”. Na lau ingelikuwa hauawi akiisema (Shahaadah), kuhakikisha kungekuwa hakuna maana.

Hali kadhalika Hadiyth nyingine na mfano wake. Maana yake ni (haya) tuliyoyasema; ya kwamba mwenye kudhihirisha Tawhiyd na Uislamu basi ni wajibu kukomeka naye isipokuwa ikibainika kutoka kwake yanayokhalifu hilo. Dalili ya hili ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema:

“Je, umemuua baada ya yeye kusema “Laa ilaaha illa Allaah?”

Na kasema:

“Nimeamrishwa kupigana na watu mpaka waseme “Laa ilaaha illa Allaah”.”

Kasema kuhusu Khawaarij:

“Popote mtapokutana nao waueni. Lau nitakutana nao, nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad”,

pamoja na kwamba ni katika watu wenye kufanya sana ´Ibaadah, Tahliyl na Tasbiyh. Mpaka hata Maswahabah walikuwa wakizidharau Swalah zao wakilinganisha na zao. Pia wamejifunza elimu kutoka kwa Maswahabah, hata hivyo haikuwafaa “Laa ilaaha illa Allaah”, wala wingi wa ´Ibaadah wala kudai kwao Uislamu pindi ilipodhihiri kwao kukhalifu kwao Shari´ah.

Hali kadhalika kuhusu tuliyoyataja kupigwa vita Mayahudi na Maswahabah kuwapiga vita Baniy Haniyfah.

Hali kadhalika alitaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwavamia Baniy al-Mustalaq baada ya kuambiwa na mtu kutoka katika wao ya kwamba wamekataa kutoa Zakaah. Mpaka Allaah Akateremsha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Anapokujieni fasiki kwa khabari yoyote (ile), basi (kwanza) hakikisheni.” (Hujuraat 49 : 06)

Ikaonekana ya kwamba mtu huyo amewasemea uongo. Yote haya yanaonesha dalili ya kwamba makusudio ya Mtume (Swalla Allaah ´alayhi wa sallam) kwa Hadiyth ambazo wanatumia kama hoja, (haya) tuliyoyataja.

 Mlango Wa 15

 Tofauti kati ya kuomba msaada kwa aliye hai kahudhuria[2] na kuomba msaada kwa asiyekuwa huyo

(Washirikina) wana shubuha nyingine. Nayo ni yale aliyoyasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba watu siku ya Qiyaamah watamuomba msaada Aadam, kisha Nuuh, kisha Ibraahiym, kisha Muusa kisha ´Iysa. Wote watatoa udhuru mpaka watapoishia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanasema: “Hii ni dalili ya kwamba kuomba msaada mwengine asiyekuwa Allaah sio Shirki”. Tunajibu kwa kusema: “Ametakasika yule ambaye Amezipiga muhuri nyoyo za maadui wake. Kwa hakika kuomba msaada viumbe kwa yale (mambo) wayawezayo, hatulipingi. Kama Alivyosema (Ta´ala) katika kisa cha Muusa:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

”Akamsaidia yule ambaye katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.” (Qaswasw 28 : 15)

Hali kadhalika ni kama jinsi mtu anaweza kumuomba msaada mwenziwe katika vita au mfano wa hilo kwa kitu ambacho anakiweza kiumbe. Na sisi tumepinga kuomba msaada katika ´Ibaadah kitu ambacho wanakifanya katika makaburi ya mawalii, au katika (ghayb) kutokuwepo kwao katika mambo ambayo hawayawezi isipokuwa Allaah. Likithibiti hilo, kuomba kwao msaada kutoka kwa Mitume siku ya Qiyaamah, wanataka kutoka kwao wamuombe Allaah Awafanyie hesabu watu, ili watu wa Peponi watolewe katika kisimamo cha hali nzito.”

Na hili ni jambo linajuzu duniani na Aakhirah. Ni mfano wa kumuendea mtu mwema aliye hai akakaa na wewe na kusikiliza maneno yako. Halafu ukamwambia: “Niombee kwa Allaah, kama jinsi Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walivyokuwa wakimuomba hilo katika uhai wake.” Ama baada ya kufa kwake, hawakumuomba kamwe kwenye kaburi lake, bali as-Salaf as-Swaalih[3] wamekataza kwa mwenye kukusudia kumuomba Allaah kwenye kaburi lake (Mtume). Vipi iweje kumuomba yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Wana shubuha nyingine. Nayo ni kisa cha Ibraahiym alipotumbukizwa kwenye Moto, Jibriyl akamfunulia na kusema: “Je, una haja ya kitu?” Akasema Ibraahiym: “Ama kama ni kutoka kwako, hapana.” Wanasema: “Lau kama kuombwa msaada Jibriyl ni Shirki, asingejionesha kwa Ibraahiym.” Jibu ni: “Kwa hakika hii ni kama ile shubuha ya kwanza. Kwa hakika Jibriyl alijionyesha kwake ili kumnufaisha kwa kitu ambacho anakiweza, kwani hakika yeye ni kama Allaah Alivyomzungumzia:

شَدِيدُ الْقُوَىٰ

”Mwenye nguvu shadidi.” (an-Najm 53 : 05)

Lau Allaah Angelimruhusu kuchukua Moto wa Ibraahiym, ardhi na milima na kuvitupa mashariki au magharibi, angelifanya hivyo. Na lau Alingelimuamrisha kumuweka Ibraahiym (´alayhis-Salaam) mahali ambapo ni mbali na wao, angelifanya hivyo. Na lau Angelimuamrisha kumpandisha mbinguni, angalifanya. Huu ni kama mfano wa mtu tajiri ana mali nyingi na ameona mtu mwenye kuhitajia. Akajitolea kumpa mkopo au kumpa kitu atatue kwazo haja yake. Lakini yule mwenye kuhitajia akakataa kuzichukua na akasubiria Allaah kumpa riziki yake mwenyewe. Hili lina mafungamano yapi na kuomba msaada katika ´Ibaadah na Shirki, lau wangelikuwa wanafahamu?

 Mlango Wa 16

 Wajibu wa kuitekeleza Tawhiyd kwa moyo, na kwa ulimi na kwa vitendo

Tunakhitimu maneno, In Shaa Allaah, kwa masuala makubwa ambayo ni muhimu sana yanayofahamika kupitia yale tuliyotaja (yaliyotangulia), lakini tutayagawa kutokana na ukubwa wake na kutokana na makosa yanayofanywa kwayo.

Tunasema: “Hakuna tofauti ya kwamba Tawhiyd lazima iwe kwa moyo, ulimi na ´amali. Akiacha mtu kitu katika haya, hawi mtu Muislamu. Akiijua Tawhiyd na asiifanyie kazi, ni kafiri mwenye inadi, kama kufuru ya Fir´awn na Iblisi na mfano wao. Hili hukosea watu wengi. Wanasema: “Kwa hakika hii ni haki. Tunafahamu hili na tunashuhudia ya kwamba ni haki, lakini hatuwezi kulifanya na wala haijuzu (kutofautiana) na watu wa mji wetu isipokuwa kwa yale yanayoafikiana na wao”, au mfano wa nyudhuru kama hizo. Na wala masikini hajui wengi wa maimamu viongozi waliokufuru, wanaijua haki na wanaiacha kwa kitu tu kama udhuru. Kama Alivyosema (Ta´ala):

اشْتَرَوْا بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا

”Wamenunua Aayah za Allaah (Qur-aan) kwa thamani ndogo.” (at-Tawbah 09 : 09)

Na mfano wa Aayah kama hizo. Kama Kauli Yake:

 يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

”Wanamtambua (Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kama wanavyowatambua watoto wao.” (al-Baqarah 02 : 146)

Akiifanyia kazi Tawhiyd kwa ´amali za dhahiri bila ya kuifahamu na wala haiamini ndani ya moyo wake, ni mnafiki na ni (mtu wa) shari kuliko kafiri wa khalisi.

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto." (an-Nisaa 04 : 145)

Na haya ni masuala ambayo ni makubwa na marefu yanakubainikia ukiyafikiria kwenye maneno ya watu. Utaona mtu mwenye kujua haki na anaacha kuifanyia kazi, kwa khofu ya maisha ya dunia au nafasi au anataka kumpaka mafuta mtu. Hali kadhalika utaona wenye kuifanyia kazi kwa nje na si kwa undani. Ukiwauliza nini wanachoitakidi ndani ya moyo, hawajui. Lakini ni juu yako kufahamu Aayah mbili katika Kitabu cha Allaah: ya kwanza ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09 : 66)

Ukihakikisha (elewa) ya kwamba baadhi ya Maswahabah ambao walipigana vita wakiwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikufuru kwa sababu ya maneno ambayo waliyatamka kwa njia ya utani na mzaha, hapo ndipo itakubainikia ya kwamba yule mwenye kutamka kwa neno la kufuru na akalifanyia kazi (akalifanya) kwa kuogopa mali yake isipungue au cheo au kwa sababu anataka kumpaka mafuta mtu, ni baya zaidi kuliko yule ambaye (kakufuru kwa) kuongea kwa maneno ambayo anafanya nayo mzaha. Aayah ya pili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ لِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake (atapata adhabu) isipokuwa yule aliyelazimishwa (kukanusha Dini ya Kiislamu) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan (kwamba yeye ni Muumin; huyu hana makosa akitamka matamshi yenye kufuru). Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao (juu yao ni) ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kubwa. Hivyo kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.” (an-Nahl 16 : 106-107)

Allaah Hakuwapa udhuru watu hawa, isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetua juu ya Imani. Ama mbali na haya, amekufuru baada ya kuamini kwake, sawa ikiwa kafanya hilo kwa khofu au kwa kupaka mafuta au cheo, watu wake, familia yake au mali, au kafanya hilo kwa mzaha au sababu zingine miongoni mwa sababu – isipokuwa aliyelazimishwa.

Aayah inatoa dalili namna hii kwa njia mbili: ya kwanza ni Kauli Yake:

“... isipokuwa yule aliyelazimishwa (kukanusha Dini ya Kiislamu) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan (kwamba yeye ni Muumin... “ (an-Nahl 16 : 106)

Allaah Hakuacha yeyote zaidi isipokuwa tu ya aliyelazimishwa, na ni jambo linalojulikana ya kwamba mtu hakirihishwi isipokuwa katika maneno au kitendo. Ama ´Aqiydah (Itikadi) ndani ya moyo, hakirihishwi yeyote kwayo. Ya pili ni Kauli Yake (Ta´ala):

“... Hivyo kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.” (an-Nahl 16 : 107)

Kaweka wazi ya kwamba kukufuru huku na adhabu sio kwa sababu ya Itikadi, ujinga, kuichukia Dini au kupenda kufuru, isipokuwa sababu yake ni kwa ajili ya (kutaka) kupata sehemu katika mambo ya dunia na kwa ajili hiyo yakamuathiri katika Dini.

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Anajua zaidi. AlhamduliLlaahi Rabbil-´Aalamiyn. Swalah na Salaam zimfikia Mtume wetu Muhammad, na ahli zake na Maswahabah zake ajma´iyn.



[1] Chanzo: Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab Da’watuhuu wa Siyraatuhu - Shaykh Ibn Baaz – Imetolewa Alhidaaya.com

[2] Yaani mtu ambaye yuko mbele yako

[3] Wema waliotangulia