Fadhila za mwezi Muharam, siku ya Ashuraa na bidaa zake
Jamii ya vilivyomo
Vyanzo
Full Description
بسم الله الرحمن الرحيم
Fadhila Za Mwezi Wa Muharram, Siku Ya 'Aashuraa Na Bid'ah Zake
Imekusanywa na Abubakari shabani rukonkwa.
Imepitiwa na Yunus Nanuni Ngenda.
AlhamduliLLaah, Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutufikisha tena katika mwaka mwengine mpya wa Kiislamu. Katika mwezi wa Muharram, kuna fadhila zake maalumu juu ya kwamba ni sawa na miezi mitukufu mingineyo. Fadhila nyingi Muislamu anaweza kuzipata atakapotekeleza maamrisho ili aweze kujichumia thawabu nyingi. Mojawapo ni funga ya tarehe 9 na 10 Muharram zinazojulikana kama Taasu'aa na 'Aashuraa. Hivyo ndugu Waislamu tusiache kufunga siku hizi mbili kwani thawabu zake ni kama ilivyotajwa katika mapokezi yafuatayo:
قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم
Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka uliotangulia)) [Muslim].
Fadhila Za Mwezi Huu Khaswa
Ingawa miezi minne yote iliyotajwa katika Aayah ya juu ni mitukufu lakini mwezi huu wa Muharram umefadhilishwa zaidi ya miezi mingine kama ilivyo
Katika Hadiyth zifuatazo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((أَفْضَلُ الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ )) رواه مسلم
Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kasema; Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Funga bora kabisa baada ya Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah wa Muharram)) [Muslim]
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : "مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَتَحَرَّى صِيَامَ يَوْمٍ فَضَّلَهُ عَلَى غَيْرِهِ إِلّا هَذَا الْيَوْمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَهَذَا الشَّهْرَ يَعْنِي شَهْرَ رَمَضَنِان " رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Sijapata kumuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisubiri kufunga siku yoyote kama siku hii ya siku ya 'Aashuraa na mwezi huu yaani mwezi wa Ramadhaan" [Al-Bukhaariy]
Sababu Ya Kufunga Siku Ya 'Aashuraa
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى، قَالَ: ((فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ)) فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ" رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alielekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Aashuraa, akasema: ((Nini hii?)) (yaani kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa Wana wa Israili kutokana na adui wao, na Muusa alifunga siku hii. Akasema (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mimi nina haki zaidi juu ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe"
[Al-Bukhaariy]
Lakini Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa tukhitilafiane na Mayahudi kufunga siku hiyo kwa kuongeza siku moja kabla.
Bid'ah Katika Siku Ya 'Aashuraa
Katika mwezi huu wa Muharram, tarehe kumi ambayo ni siku ya 'Ashuraa, tunawaona baadhi ya watu wakifanya maandamano na kuvaa nguo nyeusi wakidai ni nguo za msiba, na huku wakijipiga vifua kwa ngumi na wengine kujikata kwa visu, kujipiga kwa minyororo na damu kuwamwagika, wakidai wanaomboleza kifo cha mjukuu wa Mtume, Al-Husayn (Allaah Amrehemu). Matendo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kisheria na wanachuoni wote wa Kiislam wanapinga na kulaani anayefanya hivyo kwani ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Amesema Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu):
"Bid'ah zinazofanyika katika siku hii ni kuwa baadhi ya watu wameitenga na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni kwa kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) na kujipiga, kulia wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliharamisha kama ilivyo katika Hadiyth hii sahihi:
عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((ليس منا من لطم الخدود وشق الجيوب ودعا بدعوى الجاهلية)) البخاري .
Imetoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Sio miongoni mwetu atakayejipiga mashavuni na kuchanachana nguo na kupiga mayowe ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy]
Na haitoshi hayo wayafanyao, bali wanatukana na kuwalaani Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo."
Ibn Rajab amesema
"Wanayoyafanya Ma-Rafidhah (Mashia) katika siku hii kuwa ni siku ya huzuni kwa ajili ya kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ni amali ambazo anazopoteza mtu katika uhai wake akadhani kuwa wanafanya amali njema, wala hakuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya siku za misiba na vifo vya Mitume kuwa ni siku za huzuni, sasa vipi iwe siku ya huzuni kwa wasio Mitume?"
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie katika wale ambao husikiliza kauli wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.