NASIHA FUPI KWA WAISLAMU WAPYA
Jamii ya vilivyomo
Vyanzo
Full Description
NASIHA FUPI KWA WAISLMU WAPYA
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
1. kumbuka kwamba Uislamu ni wa Allah, Sub-hanahu wa Ta'ala. kwa hivyo ni muhimu wewe uingie katika Uislamu kwa sababu (na makusudio) ya Allah pekee, na wala sio kwa kutaka manufaa yoyote ya kibinafsi au kwa lengo la yasiyokuwa Twaa (kumtii Muumbaji).
2. Binadamu anapoupata ukweli huwa ni wajibu kwake kuushikilia na kuutetea kwa vyovyote vile, bila kujali yatakavyokuwa matokeo. Zaidi ya hayo, sharti awe na subira ili aweze kuwa na uthabiti katika huo ukweli (ambao amupata).
3. kuwapendelea wenzako mema unayoyapenda wewe, ni sehemu ya shukurani kwa Allah, Aliye juu, Mtukufu aliye mkuu, kwa neema hii ya Uislamu aliyokutunuku (aliyokupa). Kwa hivyo wakaribishe wenzako, ili nao wapate sehemu yao ya Neema hii Tukufu (Uislamu).
4. Uislamu sio mali ya mtu yeyote. Sio Mali ya Waarabu kwa kuwatenga wasiokuwa Waarabu, wala sio Mali ya Matajiri kwa kuwatenga masikini. Kwa hakika ni uwanja ulio wazi kwa wote, na zaidi ni kwamba aliye Mtukufu mbele ya Allah kuwashinda wenzie ni yule anayewazidi wenzake katika kushikamana na mafundisho, kwa kuwa anatenda kama inavyohitajika na ndiye anayetarajiwa zaidi kuwa katika daraja ya juu siku ya kiama (siku ya kufufuliwa).
5. Kumbuka kwamba baada ya wewe kuwa Muislamu utapata marafiki wapya kama watakavyozuka pia maadui - kiongozi wao akiwa Shetwani - na atajaribu kuweka kizuizi baina yako na Uislamu, au kwa kiwango cha chini sana, kukuzuilia maendeleo ndani ya dini yako, ili pia usiwanufaishe wenzako.
6. Allah, mwenye Uwezo wote na Utukufu na Ufalme ndiye Msaidizi wako, asiyekuwa na shaka. kwa hivyo, kumbuka kwamba ikiwa Allah Atatambua kwamba wewe ni muaminifu Rohoni mwako, fahamu naye Atakutendea wema unaofaa Duniani na Akhera.
7. Uislamu ni mfumo wa maisha uliopangwa vizuri, utokao kwa Mola wa ulimwengu. Na pia ni kama vile katiba. Kuhusu waislamu wote, wao ni binadamu tu ambao baadhi ya wakati, wanafanya makosa au wanakosea wakijitahidi kufanya mema. Baadhi yao wanaushikilia Uislamu vyema na hali kunao walio wapungufu, ki-elimu au ki-tabia au ki-ibada. Kwa hivyo yeyote miongoni mwao anayetenda yaliyo sawa, ni kutokana na kuwa anafahamu Uislamu vyema. Na vitendo anavyovitenda vinakuwa ndiyo sawa. Vile vile anayetenda yasiyo sawa, basi makosa yake yatamletea yeye madhara. Haiwezekani kuulaumu Uislamu kwa makosa yanayotendwa na mtu au watu ambao hawakutekeleza vyema mafundisho ya Uislamu.
8. Pengine Waislamu walifurahi sana kwa wewe kujiunga na mila hii (ya Nabii Ibrahim), na pengine walikukaribisha sana pale mwanzo. Haya ni kutokana na wanavyokupenda. pamoja na hivyo ni muhimu Allah, Mwenye Nguvu na Utukufu, aone uaminifu wako katika Roho yako na katika vitendo vyako.
9. Uislamu ni mfumo ulio na mpangilio wa maisha bora, kama vile Mashule yanavyokuwa na mpangilio wa kuwalea wanafunzi (yaani Manhaj au syllabus). Na ni njia ya maisha inayofaa kufuatwa na kufuatiliwa katika maisha yote. Kwa hivyo, kama unavyoamrisha Uislamu Mtu kuswali, kufunga (saum), kutoa zaka na sadaka, na kwenda kuhiji Makka, pia unaamrisha Mtu kuwa muaminifu na mkweli katika maongezi (kauli), mwenye huruma kwa walio wadhaifu na maskini. Aliye na heshima kwa wazee na anaishi na watu vizuri. Vile vile kama unavyokataza Uislamu Mtu kulewa na kuzini (na mke wa watu au binti yao), hivyo hivyo ndivyo unavyokataza Dhulma, Wivu, Uhasidi na Tabia mbaya. Kwa ufupi Uislamu unaamrisha kila wema na maarifa yenye manufaa na unakataza kila ubaya unaodhuru watu (iwe ni Maneno au Vitendo au Itiqadi).
10. Allah Amefanya Maisha ya hii Dunia kuwa pahala pa kufanyiwa Watu Mtihani ili kupambanua Ukweli na Uwongo, na yaliyo sawa na yaliyo makosa. Vile vile Allah, Sub-hanahu wa taala, Ametenga mtihani maalumu kwa Waumini, ili kuchunguza (imani ya) Roho zao. Kwa njaa au umasikini au maradhi au kuondokewa na wapenzi, kwa mauti au mitihani aliyoichagua Allah, ili kuwapandisha ngazi (peponi ikiwa walikuwa na subira na kudumu katika Imani na haki na vitendo vizuri). kwa hivyo kumbuka ukweli huu unapokuwa Maishani mapya.
11. Ni jambo la dharura kuwa Muislamu anahitajika kuwa mwenye nguvu, anayefurahia (kujivunia) Maisha yake mapya. Sio lazima kila wakati kuwa anachukua nafasi ya kujilinda. Badala yake anafaa pia kuwapa watu aliyonayo yeye (yaani Uislamu), akiwa na heshima zake na kujivunia Dini yake. kwa ukweli yeye ndiye aliye na bidhaa tukufu na takatifu zaidi. Wakati huo huo anafaa kuwa mwenye Hikima na mwenye Subira wakati anaongea na kutekeleza lolote na binadamu wenzake.
12. Uislamu sio tu kutamka LA ILAHA ILLA ALLAH, MUHAMMAD RASUULU LLAHI. Kwa kweli mfumo wa amri kutoka mbinguni (SHARIA) ndiyo unaoendesha maisha ya mwanadamu vyema na kikamilifu. Uislamu unazo hukumu (ahkaam), Aadabu (adabu au mpangilio wa kutekeleza mambo), Ibaadat (vitendo vya kuabudia) na Muamalaat, yaani tartibu za kutendeana baina ya Mtu na Watu (katika jamii au biashara). Kwa hivyo inahitaji mtu kujifundisha Uislamu hatua kwa hatua.
13. Mwisho tunakuhimiza ujiunge na chuo cha kufunza Waislamu wapya. vyuo ambavyo huwa vimeanzishwa pahali tofauti tofauti katika vituo vya Da'awa (vituo vya makaribisho), ili upate kuelimika kuhusu mambo yote ya Uislamu.
_____________________________________________________________
المكتب التعاوني للدعوة و توعية الجاليات بالربوة
ISLAMIC PROPAGATION OFFICE IN RABWAH
P.O. BOX 29465 ARRIYADH 11457-TEL 4454900-4916065
FAX 4970126-e-mail: rabwah @ islamhouse.org
NASIHA FUPI KWA WAISLAMU WAPYA
Tafsiri ya : A brief advice for the new Muslim
Mfasiri : Saleh M. Kyambo
mobile No : +966594370352
Lugha : KISWAHILI